Bilioni 30 za TANAPA kwa wananchi zapunguza ujangili

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kutekeleza miradi ya ujiranii mwema katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, ikitekeleza maombi na mahitaji ya jamii husika. kwenye hifadhi hiyo ya tatu kwa ukubwa nchini.

Bweni la wasichana lililojengwa naTANAPA katika moja ya Shule za Sekondari wilayni Serengeti mkoani Mara, kupitia Miradi ya Ushirikiano ya Ujirani Mwema. Picha zote na Exuperius Kachenje)

Miradi hiyo ya ujirani mwema (SCIPs) inayotekelezwa na TANAPA, kwenye hifadhi hiyo ya tatu kwa ukubwa nchini,  imetajwa kuwa chachu ya kupunguza vitendo vya ujangili na uingizaji mifugo kwenye hifadhi, ambavyo vilikuwa tishio kwa uhai wa wanyamapori na mazingira yanayowazunguka.

Ofisa Uhusiano wa Jamii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Abed Mwesigwa amebaisha hayo akitaja wanufaika ni Wilaya za Serengeti, Bunda, Tarime, Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Ngorongoro katika mikoa ya Mara, Arusha na Simiyu.

“Takriban Shilingi  bilioni 34 za TANAPA  zimetekeleza miradimbalimbali pamoja na miundombinu ya afya, elimu, maji, barabara na madaraja huku pia wakitekeleza mradi wa matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na wadau wengine,”amesema Mwesigwa na kuongeza:

 Katika miradi hiyo,TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, imejenga shule, kuchimba mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo, nyumba za madaktari katika baadhi ya zahanati, nyumba za walimu, bweni la wanafunzi wa kike, barabara, madaraja pamoja na ujenzi wa vituo vya askari ili kuvihami vijiji na wanyama wakali katika vijiji jirani na hifadhi.

Mzee John Marwa mkazi wa Kijiji Pake, Rubanda wilayani Serengeti, mkoani Mara akizungumzia mradi wa barabara waliyojengewa  na TANAPA.

Amebainisha kuwa Hifadhi ya Serengeti imezungukwa na vijiji 248, vikiwa katika wilaya nane za mikoa mitatu ambayo ni Mara, Arusha na Simiyu.      

Mwesigwa ametanabainisha kuwa tayari vijana katika vijiji hivyo wameanza kupatiwa ajira kwenye kampuni za ulinzi na uwindaji, ili kuwainua kiuchumi, hivyo kushiriki ulinzi wa raslimali za taifa.

Hata hivyo, amesema TANAPA limeweka masharti kadhaa ya utoaji miradi hiyo likiwamo linalotaka vijiji vinavyoomba miradi kutokomeza ujangili na kuacha kuingiza mifugo kwenye hifadhi kwa ajili ya malisho ili kulinda ikolojia ya Serengeti ili kukidhi vigezo vya kupata miradi ya maendeleo.

Daraja lililojengwa na TANAPA kati ya miradi ya ujirani mwema iliyotekeleza kwenye vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Serengeti 

“Kijiji kinachoshiriki vitendo vya ujangili na uingizaji mifugo kwenye hifadhi, hicho kinakosa sifa ya kupewa miradi hiyo. Kutokana na kigezo hicho, wanavijiji wamekuwa wanadhibitiana wenyewe na kupunguza ujangili, hali inayoleta manufaa zaidi kwa hifadhi na wananchi.

“Majangili wanaotoka mbali na maeneo ya hifadhi hawawezi kutekeleza uhalifu huo bila kushirikiana na wenyeji,”amesema Mwesigwa.

Mzee John Marwa mkazi wa Kijiji Pake, Rubanda wilayani Serengeti anaishukuru TANAPA kwa kuwajengea barabara ya Nyigoti Nyichoka inayopita katika Kijiji chao kuwaunganisha na maeneo mengine, hali inayowarahisishia usafiri na kupunguza gharama za maisha. 

“Awali tulilazimika kwenda hadi Mugumu ili kupata usafiri kwenda Bunda, lakini sasa tunakwenda moja kwa moja,” amesema Mzee Marwa.   

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bokore, Nelson James alikiri Kijiji chake kujengewa zahanati ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya milioni 400 na barabara yenye urefu wa kilometa 12, ambayo awali ilikuwa haipitiki hasa wakati za masika.

Mganga Mfawidhi wa Zahati ya Koreri, Kijiji cha Koreri, Kata ya Mbarimbari, Serengeti mkoani Mara, Dk.Eliud Kanagwa akiwa mbele ya nyumba anayoishi iliyojengwa na TANAPA kwa ajili ya watumishi wa zahanati hiyo

"Sasa tuna uhakika wa kupata huduma saa 24, zahanati hii ni mkombozi mkubwa kwa wajawazito,” amesema Nyabikwabe Nyerera mkazi wa Kijiji cha Bokore.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi