Tanzania, Canada kushirikiana kuendeleza sekta ya madini

▪️Balozi wa Canada apongeza mageuzi madini

▪️Wachimbaji wadogo kujengewa uwezo 

Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Balozi wa Canada nchini Tanzania Emily Burns lwamekutana jijini Dodoma na kufanya kikao kuhusu maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde (Kushoto) na Balozi wa Canada nchini Tanzania Emily Burns walipokutana jijini Dodoma na kufanya kikao kuhusu maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Balozi Emily Burns pia ametumia kikao hicho kujitambulisha, amesema Canada ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini kwa kuwajengeza uwezo katika uchimbaji wa matumizi sahihi ya teknolojia, utakaozingatia utunzaji wa mazingira na kuwajengea ujuzi, ili kuongeza tija kwenye uzalishaji madini.

Balozi Burns ameonesha utayari wa Serikali ya Canada kutoa mafunzo maalum (Tailor-made training) kwa wakinamama na vijana kupitia vyuo vya Ufundi-VETA katika maeneo ambayo uzalishaji madini unafanyika kwa wingi.

Ametumia pia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa yanayofanyika kwenye sekta ya madini na kuwezesha mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024.

Kwa upande wake, Waziri Anthony Mavunde ameishukuru Serikali ya Canada kwa dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya madini nchini. 

"Naamini katika  ushirikiano wa utafiti wa kina kwa upatikanaji wa madini nchini ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za wingi wa madini nchini," amesema Mavunde.

Waziri Mavunde pia ameonesha umuhimu wa uwezeshaji kwa akinamama na vijana, kupitia Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow(MBT), yenye lengo la kuyawezesha makundi hayo mawili katika ushiriki wake katika uchumi kupitia sekta ya madini.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi