Kamati ya Bunge yasifu kazi ya NHC
-Wizara ya Madini kuanza kazi Mtumba Mei 15
Mwandishi Wetu Daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba laTaifa(NHC), limeendelea kung’ara katika utekelezaji miradi mikubwa ya ujenzi likipongezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, huku Wazara ya Madini ikitangaza itaanza utoaji huduma kutoka ofisi yake mpya katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma ifikapo Mei.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetoa pongezi hizo katika ziara yake kwenye Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi za Wizara ya Madini na ule wa Nishati, ambapo Waziri wa Madini,Anthony Mavunde ameutangazia umma kuwa watumishi wote wa wizara akiwamo yeye wataanza kuhudumia wananchi kutoka kwenye jengo hilo jipya kuanzia Mei 15, 2025.
Kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Dk. Mathayo David Mathayo, ilifanya ziara pia katika Jengo la Wizara ya Nishati. Dk.Mathayo ameeleza kuridhishwa kwa kamati na kiwango cha kazi ya NHC katika majengo hayo huku akiipongeza Serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutosha takriban Shilingi Bilion 300 kukamilisha Mji wa Serikali Mtumba.
Katika ziara hiyo, NHC ilieleza kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 92.8, zikibaki kazi chache za ukamilishaji mifumo ya Zimamoto, TEHAMA na rangi.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameeleza kuwa tayari wameshatangaza zabuni ya Samani na kwamba wataanza kutoahuduma ndani ya jengo hilo mwezi Mei mwaka huu.
‘’Mwenyekiti, kukamilika kwa jengo hili kutaiwezesha Wizara kuwahudumia Watanzania na wageni kutokea eneo moja, hivyo kutoa huduma kwa urahisi kuliko ilivyo sasa kwani baadhi ya watumishi wapo maeneo mengine ikiwemo eneo ilipo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na hapa Mtumba,’’ amesema Waziri Mavunde na kuongeza:
“Mwenyekiti nawashukuru kwa usimamizi wenu madhubuti kuhakikisha mradi huu unakamilika, mara zote mlikuwa wakali kwa Serikali ili kuona jambo hili linafanikiwa. Haya ni mafanikio ya kamati. “Tarehe 15, Mei, 2025 watumishi wote wa wizara yangu wakiongozwa na mimi tutaanza kutoa huduma kutoka katika jengo hili.”
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha zilizowezesha kuongeza nguvu ya kukamilisha mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, ambapo imetoa shilingi bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa mji huo.
Waziri Mavunde amesema uwepo wa mji huo utarahisisha nakusaidia kuboresha utoaji huduma wa Serikali akieleza kuwa majengo hayo yameongeza mwonekano mzuri wa mji wa Dodoma.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk. David Mathayo amesema kwa hatua ya ujenzi ilivyofikiwa, kamati yak eina matumaini makubwa ya wananchi kupata huduma bora.
“Uwepo wa Wizara zote katika Mji wa wa Serikali Mtumba,utarahisisha utoaji huduma kwa wawekezaji na Watanzania kama ilivyo kwa nchi ya Brazil,” amesema Dk. Mathayo huku akiusifu uongozi wa Wizara ya Madini kwa unavyosimamia shughuli za Sekta ya Madini.
“NHC imefanya kazi nzuri, jengo ni zuri, Tunaiomba Serikali iendelee kutoa fedha kwa NHC ikamilishe jengo hili na ya Wizara nyingine yaliyopo hapa Mji wa Serikali Mtumba,” amesema Dk. Mathayo.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa NHC, Mhandisi Peter Mwaisabula amesema: “Tunamshukuru Mshauri Mshitiri wa wa mradi huu ambao ni Wizara ya Madini,imekuwa ikitupa fedha kwa wakati kutekeleza mradi huu, Ujenzi sasa umefikia asilimia92.8, tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, imekuwa ikitupa ushirikiano wa kutosha,”
Jengo hilo na mengine saba ya wizara mbalimbali, yanajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambapo Mshauri Elekezi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). NHC inatekeleza ujenzi wa majengo ya ofisi nane za Wizara katika Mji wa Serikali wa Mtumba, Dodoma uliokamilika kwa asilimia 96.
0 Maoni