Tume ya Madini yakusanya bilioni 690
Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com
TUME ya Madini imefanikiwa kukusanya takriban Shilingi Bilioni 690, 763 ndani ya miezi nane sawa na asilimia 69.08 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/2025.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, akizungumza na wanahabari leo Machi 4, 2025
Akielezea mafanikio ya Tume ya Madini kwa kipindi cha miaka minne, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo leo Machi 4, 2025 amesema ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na rasilimali umepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
“Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Tume imefanikiwa kukusanya shilingi 690, 763, 401,639.06 sawa na aslimia 69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025,”amesema Mhandisi Lwamo.
Amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023.
“Hii ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini, ukuaji wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023,”amesema.
Amefafanua kwamba ili kuendelea kuimarika kwa sekta ya madini, mwenendo wa mchango wa sekta ya madini na ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 10 mwaka huu wa 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Wadau wa Sekta ya Madini wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, alipozungumza na wanahabari leo Machi 4, 2025
Lwamo ameongeza kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini, imeendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini, ambapo hadi kufikia mwezi Februari, 2025 Tume ya Madini kwa kushirikiana na TAMISEMI imefanikiwa kuanzisha masoko 43 na vituo vya ununuzi wa madini 109.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lwamo jumla ya mipango 1,076 ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini imepokelewa na kufanyiwa uchambuzi.
“ Kati ya mipango iliyowasilishwa, 1,047 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na mipango 29 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho;”amesema Lwamo.
Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye kampuni mbalimbali za uchimbaji, ambapo kampuni zimeweza kuzalisha ajira 19,874, kati ya hizo 19,371 ni Watanzania sawa na asilimia 97.5 na 503 ni wageni sawa na asilimia 2.5 ya ajira zote zilizozalishwa.
“Vilevile, jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini, ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini,”amesema.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Lwamo amesema Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo imefanikiwa kutenga maeneo 58 katika mikoa mbalimbali.
Maoni
Chapisha Maoni