Shahidi: Pakiti 16 zilizokamatwa Charambe Sekondari ni kilo 15 za heroin

 Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com 

SHAHIDI wa kwanza upande wa mashtaka,mchunguzi kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Leonidas Michael amedai pakiti16 zilizokamatwa maeneo ya Shule ya Sekondari Charambe ni dawa za kulevya aina ya heroine.


Shahidi amedai hayo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Dar es Salam, mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati akitoa ushahidi wake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Suleiman Thabiti, Sharifa Bakari na Faridi Saidi ambao wanashtakiwa kuwa Novemba 30 mwaka 2022 walikutwa maeneo ya Mbagala Charambe wakifanya biashara ya kusafirisha dawa za kulevya, aina heroine kilo 15.19.

Shahidi akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Diana Lukondo alidai kuwa Novemba 30,2022 alikuwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alipokea sampuli kutoka kwa ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Selemani Mbwambo.

Alidai sampuli moja ulikuwa mfuko wa salfeti ndani ulikuwa na pakiti 16 zenye chenga zilizosadikiwa kuwa dawa za kulevya na sampuli ya pili ilikuwa bahasha ya kaki iliyokuwa na vifungashio vyenye masalia yaliyosadikiwa kuwa dawa za kulevya.

Leonidas alidai alipima uzito wa chenga na kubaini ilikuwa kilogramu 15.19 na alipofanya uchunguzi wa awali alibaini zilikuwa dawa za kulevya aina ya heroine.

Alidai kuwa Januari 13 mwaka 2023, alifanya uchunguzi wa uthibitisho kwa kuchukua sampuli na kuzipeleka kwenye mitambo.

Alidai pakiti zilipewa alama A1 hadi A16 na katika uchunguzi wa uthibitisho ilibainika kuwa ni heroine na vifungashio vilipewa alama B1na B2.

Alidai uchunguzi ulibaini masalia yaliyokuwemo kwenye vifungashio hivyo yalikuwa ni heroine na cocaine.

Baada ya kumaliza uchunguzi wa uthibitisho aliandaa taarifa Januari 16 mwaka 2023 , alisaini na kuipeleka kwa Mkuu wake wa idara.

Wakili Diana alitaka shahidi aeleze ataitambua vipi taarifa ya uchunguzi aliyoiandaa.

Shahidi alidai ataitambua kwa kuwa ina jina lake, sahihi yake , kuna maelezo ya mfuko wa salfeti wenye pakiti 16 zenye Alama A1 hadi A16 na bahasha ya kaki yenye vifungashio vya masalia ya dawa za kulevya.

Baada ya kuitambua aliomba kutoa kielelezo hicho kama sehemu ya ushahidi wake, upande wa utetezi haukuwa na pingamizi na Mahakama ilipokea.

Mawakili wengine walioiwakilisha Jamhuri ni Edith Mauya, Titus Aron na John Kaongo. Mawakili wanaowawakilisha washtakiwa ni Nehemiah Nkoko na Josephat Mabula.

Hadi tunatoka kwenye viunga vya Mahakama shauri hilo linaendelea kusikilizwa.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi