Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Tumejihatiti kuboresha huduma

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga katika kuendelea kuimarisha na kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wakati akizungumza kwenye mkutano maalaumu na vyombo vya habari, Machi19, 2025 ofisini kwake Kivukoni Dar es Salaam. 

Hayo yamebainishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wakati akizungumza kwenye mkutano maalaumu na vyombo vya habari, uliofanyika Machi19, 2025 ofisini kwake Kivukoni Dar es Salaam. 

Akizungumza katika mkutano huo, Johari amesema ofisi yake imeandaa mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali nchini yatakayofanyika jijini Arusha Machi  24 hadi 28, 2025 yakiwa na lengo la kuongeza umahiri na utendaji kazi wa mawakili hao. 

Mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali ni sehemu ya kuimarisha utaratibu wa Mafunzo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mawakili hao, pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika Febuari, 2025, ambapo aliiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali.

“Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaboresha na kuimarisha uwezo wa Mawakili wa Serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha," amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Johari ameeleza kuwa mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali yataendeshwa na wakufunzi wabobezi wa ndani na nje ya nchi, ambao watatoa mada mbalimbali zitakazowaimarisha mawakili hao katika uandishi, uingiwaji na majadiliano ya mikataba ya kimataifa, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na uandishi wa sheria.

“Kama mnavyofahamu, Rais anazidi kuifungua nchi, wigo wa uwekezaji unaizidi kupanuka hivyo sisi kama wanasheria ni lazima tuhakikishe tunanyumbulika ili kuendana na kasi hiyo,” ameagiza Johari.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali amesema mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Mawakili wa Serikali kujifunza zaidi majukumu yao katika kuuvaa uzalendo na kulinda maslahi na usalama wa taifa, ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi na usalama wa taifa. 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, mafunzo hayo yatawasaidia Mawakili wa Serikali kujikumbusha sheria zinazohusu fedha za kigeni, hati fungani na dhamana.

“Tunataka kuwa na Wanasheria na Mawakili ambao watakuwa na uelewa mzuri katika masoko ya fedha, masoko ya mitaji," amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali nchi nzima kuhudhuria bila kukosa mafunzo hayo, huku akiziomba wizara, taasisi na halmashauri kuwaruhusu na kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushiriki katika mafunzo hayo kwani yatasaidia kuboresha utendaji kazi wao. 

“Nitoe wito kwa Mawakili wa Serikali ambao hawajajisajili wafanye hivyo haraka sana ili waweze kuhudhuria mafunzo haya ambayo yatawasaida kuimarisha utendaji kazi wao”. amesema Johari.

Sambamba na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitumia Mkutano huo na Vyombo vya Habari kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya uongozi wake pamoja na mafanikio makubwa ambayo Taifa limeyapata.

Chapisha Maoni

0 Maoni