-Ni kupitia Sekta ya Madini Kagera
-Waita wawekezaji ndani na nje
Mwandishi Wetu, daimatznews
MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kagera yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/ 2025 ni Shilingi Bilioni 3.2.
![]() |
Wachimbaji madini wadogo wakiwa katika shughuli zao |
Kagera ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5.8 na mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wa 2025 wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kikiwa ni sawa na asilimia 82 ya lengo katika kipindi cha miezi minane.
Akizungumza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema fedha hizo zimekusanywa kutokana na jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa Sekta ya Madini katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera.
“Mkoa wa Kagera kwa maana Sekta ya Madini tunasimamia halmashauri zote saba kwa maana ya wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba, Biharamulo na Ngara, kuna shughuli mbalimbali za uchimbaji madini,”amesema Mkopi (pichani chini) na kuongeza:
“Mkoa huu yanapatikana madini mbalimbali ikiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini Ujenzi."
Kwa mujibu wa Mkopi, maeneo ya Kyerwa yanachimbwa madini ya bati kihalali kwa leseni za uchimbaji mdogo, lakini pia kuna leseni kubwa ya utafiti na yanachangia asilimia 32 ya maduhuli yaliyokusanyawa ya Shilingi Bilioni 3.2 huku fedha nyingine zikitoka kwenye madini mengine ikiwemo dhahabu na ada mbalimbali za vibali na leseni.
Amesema mwenendo wa ukusanyaji maduhuli sio mbaya na hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wana imani watafikia lengo lililokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Mkopi ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Kagera ambao una utajiri mkubwa wa madini mbalimbali yakiwemo Bati, Dhahabu, Nickel, Wolframite (WO3), Madini ya Viwandani na Madini ujenzi
0 Maoni