Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Msikiti 'mikononi' mwa RITA Arusha

Mwandishi Wetu, Arusha

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), umeunda kamati ya muda itakayochukua majukumu  ya Bodi ya Udhamini iliyomaliza muda wake ya Taasisi ya Arusha Muslim.
Sanjari na hatua hiyo, RITA imeunda Kamati ya Maalumu ya Uchunguzi itakayofuatilia malalamiko ya wanachama, kuwatuhumu viongozi wa msikiti huo kuhujumu mali za  taasisi hiyo.

Akizitambulisha kamati hizo katika kikao kilichojumuisha uongozi wa RITA, viongozi wa Serikali ya Wilaya ya  Arusha, viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA ), viongozi wa Arusha Muslim pamoja na wanachama wa msikiti huo, Kabidhi Wasii  Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi ameziagiza kamati hizo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu.

 “Nimeiagiza Bodi iliyomaliza muda wake kuwasilisha RITA taarifa ya mapato na matumizi,” amesema Kanyusi na kuiagiza kamati ya mpito kuhakikisha inafanya marekebisho ya katiba na uchaguzi unafanyika ndani ya siku 60, ili kupata viongozi watakaosimamia taasisi kwa mujibu wa katiba.

Kanyusi pia ameaitaka Kamati Maalumu ya Uchunguzi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya siku 14 na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi RITA.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Khamana Simba  ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye kikao hicho, amewataka wanachama wa Arusha Musilim kuwa watulivu na kwamba Serikali ipo pamoja nao kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapata ufumbuzi wa kudumu kwa amani, utulivu na haki.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inafuatilia kila kitu na ninawahakikishia kwamba, ufumumbuzi wa tatizo lenu utapatikana,” amesema katibu tawala huyo na kuwataka waendelee kuwa wamoja na watulivu.

Baadhi ya wanachama  ARUSHA Muslim,  Mustapha Mohamedi na Kassim Collins waliipongeza Serikali  kwa kufuatilia mgogoro huo huku wakiomba hatua zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa wamefanya ubadhirifu.

Naye, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu, Irene Kesulie aliwatoa hofu wanachama wanaoidai taasisi hiyo  kwamba wafuate taratibu ikiwemo kuandika barua na kuziwasilisha RITA ili taratimu za kisheria ziweze kufuatwa na wapate haki yao.

“RITA kama ipo hapa kusimamia haki za wanachama kwa wa sheria na katiba. Tunawasihi endeleeni kuwa watulivu na wavumilivu,” amesema Irene.

Chapisha Maoni

0 Maoni