Selemani Msuya, daimatznews@gmail.com
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewaomba wadau wa sekta ya habari kuwa na imani naye kuhusu vifungu 12 vinavyolalamikiwa katika Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016.
![]() |
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye |
Kauli hiyo ya Waziri Nape imetokana na maazimio sita yaliyosomwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Thobias Makoba, ambapo moja ya azimio lilikuwa ni vifungu 12 vya Sheria ya Huduma ya Habari ambavyo vinalalamikiwa na wadau wa sekta hiyo.
Nape ametoa kauli hiyo wakati akifunga Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari lilifoanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kwa siku mbili na kushirikisha wadau zaidi 1,200 kutoka sekta umma na binafsi kwenye tasnia ya habari.
"Nitatoa mfano, hoja ya umiliki wa vyombo vya habari, ipo kwenye Sera ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2003, mimi sikuwepo, nilikuwa ndio naanza kazi CCM. Jamani naomba tuaminiane, mimi ni mdau wa sekta hii kwa sababu nimeisomea. Sitengenezi kwa ajili yangu au ajili yenu, ni kwa ajili yetu, kwa sababu sijui watoto wangu watafanya kazi gani. Tuaminiane. Tutafika salama;
“Hili suala la vifungu 12 vya Sheria ya Huduma ya Habari mnavyovitaja kila mara, nadhani nimefafanua sana kwamba hoja hizi tutazifanyia kazi, baada ya sera mpya kutungwa na vingine vitaingia kwenye kanuni, najisikia vibaya kwa sababu tumefanya vikao na kukubaliana,” amesema.
Awali, katika maelezo yake, Makoba alitaja maazimio mengine kuwa ni wizara na taasisi za Serikali kulipa madeni ya vyombo vya habari ifikapo Desemba 24 mwaka huu 2024 na wamiliki waweze kulipa mishahara.
Jingine ni Serikali kuangalia uwezekano wawekezaji wakigeni kuwa na asilimia 75 ya umiliki vyombo vya habari, vyombo vya habari kuandika habari za kijamii, vyombo vya habari vitoe fursa sawa kwa vyama vyote na vyombo vya habari vya mtandao viongoze ubunifu na kuandaa maudhui yenye tija na kujijengea uaminifu kwa walaji.
Hata hivyo, Waziri Nape amesema kwamba amekuwa akisikitishwa na mwendelezo wa kulalamikia vifungu 12 vya sheria hiyo, huku akiwa ameelezea kwa nini havikufanyiwa mabadiliko wakati wa mabadiliko yaliyohusisha vifungu tisa pekee vya sheria hiyo.
Amesema kuna vifungu vinavyohitaji mabadiliko ya sera ndipo viweze kubadilika na vingine vitaingizwa kwenye kanuni, hivyo amewataka wadau kuacha kulalamika wakihisi Serikali haitaki.
Nape amesema katika mchakato huo wa kubadilisha sheria aliwashirikisha baadhi ya waandishi na kuwaonesha hali halisi, hivyo anaumia pale ambapo anatiliwa mashaka katika hilo.
Ameeleza kwamba aliwasilisha sheria bungeni na mjadala ukawa mkali kwa wabunge kutaka mabadiliko na alikubali mabadiliko ambayo wabunge walitaka, jambo ambalo halijafanywa na waziri yoyote.
“Sikilizeni mimi naipenda sekta hii, kiasi kwamba 2017 nilikuwa tayari kupoteza uwaziri, kulinda uhuru wa vyombo vya habari wa nchi hii, msisahau rekodi hizi.
:Sekta ya habari ipo ndani ya moyo wangu, siku ile wakina Deudatus Balile, Jesse Kwayu na wengine wanaenda kusoma ripoti nilijua nafukuzwa, waliniambia nitafukuzwa nikawaambia nilipofikia siwezi kurudi nyuma, uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kuliko kazi yangu," amesema Nape Napa.
Ameongeza: "Siwezi kuingi kwenye rekodi ya kuhujumu vyombo vya habari kwa sababu utanifuata maisha yangu yote, kwa sababu ya cheo tu. Si nilitoka, leo nimerudi nasonga mbele na heshima yangu ipo. Wanahabari msisahu, sekta ya habari ipo mikono salama. Na wao wanajua, wasioitakia mema sekta hii wanajua, ilimradi Nape yupo atasimamia na wanahabari wake.”
Nape amewahakikishia wadau wa sekta ya habari kuwa serikali chini ya uongozi Rais Samia Suluhu Hassana ina dhamira ya kweli ya kujenga ushirikiano, ili kuhakikisha kila upande unanufaika.
0 Maoni