Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Nape: 2024/2025 tutatekeleza haya

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imebainisha malengo 28 itakayotekeleza katika mwaka wa fedha 2024/25 ikiwamo kujenga Kituo cha kuhifadhi Data Dodoma na Zanzibar, pamoja na kuanzisha kituo kimoja cha Usalama wa Mawasiliano cha Taifa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye akiwasilisha bungeni, makadirio ya bajeti, mapato na matumizi ya wizara yake lo Mei16, 2024.

Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye, amebainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25, bungeni mjini Dodoma leo Mei 16, 2024.

"Serikali pia imepanga kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vyombo vya ulinzi na usalama kama Mahakama, TAKUKURU, Polisi, Magereza, JWTZ, Usalama wa Taifa), pamoja na taasisi 100 za Haki Jinai na Taasisi nyingine za Serikali," amesema Waziri Nape.            

Ametaja mambo mengine yatakayotekelezwa kuwa ni ukamilishaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya Simu 616 ili kufikia minara 758 katika kata 713, pamoja na kuanza ujenzi wa minara mingine mipya 636 ili kuhakikisha maeneo yaliyobaki yanapata mawasiliano.

Waziri Nape amesema, wizara hiyo imepanga kuiongezea nguvu minara 135 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na/au 4G, kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo 70 ya kimkakati mathalan maeneo ya hifadhi na mipakani, kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Wilaya 40 nchini, na katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.

Ametaja mipango mingine kuwa ni  kuendelea kuimarisha mifumo ya kusimamia na kupima ubora wa huduma za mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na usimamizi wa sekta, kuwezesha Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuunganishwa na mifumo mingine ya kutolea huduma za kijamii.

"Serikali inapanga kufanya ununuzi wa magari mawili maalum ya kurushia matangazo mbashara (OB Van) na magari 15 kwa ajili ya shughuli za utangazaji katika vituo vipya vya kurushia matangazo ikiwemo kuwezesha kutangaza shughuli za Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa," amesema Nape.

Amesema Serikali pia itaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari, kuratibu uanzishaji wa Wakala wa Anga za Juu Tanzania, kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Anga za Juu na kutengeneza na kutumia mfumo wa kukusanya na kusambaza mizigo.

Nape amesema pia Serikali kupitia wizara hiyo, inakusudia kusimamia uundaji wa mfumo wa kidijitali utakaowezesha biashara Mtandao (e-Commerce), kutekeleza mradi wa kujenga kituo cha kikanda kitakachojumuisha maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao.


Mwisho

Chapisha Maoni

0 Maoni