-Yalenga kupunguza mgongano ya wanyamapori na wananchi
-Yatoa
kipaumbele maeneo 12
Mwandishi
Wetu, daimatznews@gmail.com
Serikali imeanza kuandaa Kanuni za Kutangaza na Kusimamia
Maeneo 77 Nyeti na Lindwa yaliyoainishwa, inayotarajiwa kukamilika kabla ya
Juni, 2024, ikiwa pia katika hatua ya kupunguza mgongano wa matumizi ya
rasilimali kati ya wanyamapori na wananchi.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo amebainisha
hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma Januari
24, 2024.
![]() |
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo, akizungumza mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya maji na Mazingira Januari 24,2024, jijini Dodoma. |
Amesema Serikali imeyapa kipaumbele maeneo 12
kwa ajili ya kufanyiwa tathmini zaidi kwa kuzingatia umuhimu wake kiikolojia
kutokana na uharibifu wa mazingira.
“Tupo katika
hatua za kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori na
wananchi, kupunguza mgongano wa matumizi ya rasilimali kati ya wanyamapori,
uharibifu wa misitu unaotokana na shughuli za kibinadamu kama vile ukataji miti
kwa ajili ya mkaa na kuni na uchimbaji holela wa madini,” amesema Waziri Jafo.
Akiwasilisha
taarifa ya Hali ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Mipango ya Ulinzi wa Mazingira
katika maeneo Lindwa na Nyeti, Jafo amesema amesema maeneo yaliyo kwenye mpango
huo ni yaliyoko kwenye madakio ya mito, maziwa, shoroba, milima na ardhi oevu
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Dakio la Mto
Kihansi, Ziwa Challa lililoko Wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Mlima
Livingstone na safu ya milima ya Mbeya katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma
na safu ya Milima ya Makonde (Makonde Plateau Mountain Ranges).
Kwa mujibu wa Jafo, mengine ni maeneo nyeti na
lindwa pendekezwa ambayo ni Mlima Mukendo mjini Musoma mkoani Mara, Ziwa
Singidani, Ziwa Kindai na Ziwa Munang yaliyoko mkoani Singida na Ziwa Burunge,
mifumo ikolojia ya hifadhi ya Tarangire na Ziwa Manyara yaliyoko mkoani
Manyara.
Waziri Jafo
amebainisha kuwa faida za kuwa na maneo lindwa na nyeti ni kuimarisha uhifadhi
wa mifumo ikolojia yenye misitu, vyanzo vya maji na wanyamapori iliyopo nje ya
maeneo yanayosimamiwa na sheria nyingine.
Amesema hatua
hiyo itasaidia pia faida nyingine kulinda mazalia, makazi na malisho ya viumbe pia
kuwakinga na madhara yatokanayo na majanga ya asili yanayoweza kutokea katika
maeneo husika kama maporomoko ya ardhi, mafuriko na uvamizi wa wanyamapori.
0 Maoni