NHC YACHOCHEA MAPINDUZI YA KIDIJITALI, YAONGEZA KASI YA HUDUMA NA UKUAJI MAPATO

 -Yaja na App inayompa mteja fursa kujihudumia, miradi ya kimkakati ikiimarisha uchumi wa taifa

-Ubunifu wa kifedha, rasilimali watu vyaimarisha nafasi ya shirika kitaifa, yajikusanyia tuzo 

Mwandishi Wetu daimatznews@gmail.com

Katika dunia ambayo matumizi ya teknolojia ya kidijitali yanashika kasi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),  limechukua hatua madhubuti kuendana na mabadiliko hayo kwa kubadili namna linavyotoa huduma kwa wananchi.

Kupitia programu ya kisasa ya simu (App), shirika hilo limefungua zaidi mlango kwa wateja wake, ambao sasa wanaweza kuomba nyumba za kupanga au kununua, kufuatilia maombi yao, na kuwasilisha maoni au malalamiko bila kufika ofisini. 

Mfumo huu umeondoa vikwazo vya urasimu, umeongeza uwazi, na kuboresha kwa kiasi kikubwa uzoefu wa mteja.

Akizungumza katika mahojiano maalum kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya, anasema hatua hiyo inaakisi dhamira ya shirika ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuboresha huduma na kuwafikia Watanzania wengi zaidi, sambamba na dira ya taifa ya uchumi wa kidijitali.

Ukuaji wa mapato, ufanisi wa kiutendaji

Mageuzi hayo ya kidijitali yanaenda sambamba na kuimarika kwa utendaji wa shirika, ikiwemo kuongezeka kwa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa huduma.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa(NHC), Hamad Abdallah.

Kwa mujibu wa Saguya, aliyefanya kazi ndani ya NHC kwa takriban miaka 25 na ambaye sasa amestaafu, mifumo ya kisasa imeongeza uwazi katika michakato ya ndani, kupunguza upotevu wa muda na rasilimali, na kuweka msingi imara wa ukuaji endelevu wa kifedha. 

Hiyo imeiwezesha NHC kujiendesha kwa mtazamo wa kibiashara zaidi, huku ikiendelea kutekeleza majukumu yake ya kijamii ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi, ofisi na biashara.

Miradi NHC inavyochangia uchumi wa Taifa

Mbali na mafanikio ya kiutendaji, NHC imeendelea kuthibitisha uwezo wake kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini kote.

Katika mwaka wa fedha uliopita, shirika limekamilisha miradi muhimu ikiwemo majengo ya Serikali katika eneo la Mtumba, Dodoma, hatua inayochangia kuimarika kwa shughuli za kiutawala katika mji huo ambao ni makao makuu ya nchi. Aidha, NHC limeendelea kutekeleza miradi ya kibiashara na kijamii inayochochea ukuaji wa uchumi. 

Muungano Saguya

Kati ya hayo, inawawezesha wataanzania sasa kupata mikopo ya fedha kutoka benki na taasisi mbalimbali 23 za fedha kwa ajili ya kununua nymba zinazojengewa na NHC. 

Kwa mujibu wa Saguya, mwananchi anaweza kukopeshwa fedha  ambazo atazilipa kwa kati ya miaka 5 hadi 10.

Kwenye sekta ya madini, NHC imechangia kuboresha miundombinu katika eneo la Tanzanite Mererani, ikiunga mkono juhudi za kuongeza thamani ya rasilimali hiyo adhimu duniani. 

Kwa ujumla, miradi ya shirika sasa inatekelezwa katika karibu mikoa yote ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza upungufu wa nyumba unaokadiriwa kuzidi milioni tatu ambao pia huongezeka kila mwaka.

Mfano NHC ina miradi 68 maeneo mbalimbali nchini, kati ya hiyo 38 imeanza kutekelezwa, yote ikiwa na thamani ya Sh 607 bilioni na mingine ipo katika hatua mbalimbali za uandaaji,

NHC pia inakusanya mapato ya zaidi ya Sh10 bilioni ambazo ni kodi kutoka kwa wapangaji wa nyumba zake kwa mwezi, huku ikipunguza deli inalowadai wapangaji hadi kufikia Sh18 bilioni, kutoka Sh27 bilioni.

Imeweka mfumo wa kidijitali unaomtaka kila mpangaji kulipa kodi ya miezi mitatu kama dhamna ya upangaji katika nyumba za NHC, ambazo zitatumika kulipa deni iwapo mteja atashindwa kulipa kodi, au kuafanya haribifu ndani ya nyumba za shirika.

Wafanyakazi nguzo imara mafanikio ya NHC

Pamoja na mafanikio ya teknolojia na miradi, nguvu halisi ya NHC ipo kwa watu wake. Shirika linaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kama sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu.

Saguya anabainisha kuwa wafanyakazi wanapewa mafunzo ya mara kwa mara, ndani na nje ya nchi, ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mbinu za kisasa za ujenzi na usimamizi wa miradi.

Aidha, shirika hilo limeweka mkazo katika maadili ya kazi, uwajibikaji na weledi kupitia mifumo madhubuti ya utendaji. 

Kuhusu viwango vya kazi vinapimwa kwa uwazi, huku nidhamu ikipewa kipaumbele ili kuhakikisha ubora wa huduma na kulinda hadhi ya taasisi.

Licha ya mafanikio haya, NHC inaendelea kubuni mikakati mipya, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa Watanzania wengi zaidi.

Pia, kupitia mpango wa kutoa hati fungani (bond), shirika linatarajia kupanua wigo wa vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba, huku likitoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uwekezaji wa sekta ya makazi.

NHC kesho

Kwa kuunganisha teknolojia, ufanisi wa kifedha, miradi yenye tija na uwekezaji kwa watu, Shirika la Nyumba la Taifa ambalo ni mkandarasi daraja la kwanza. 

Kwa mujibu wa Saguya NHC inaendelea kujijenga kama taasisi kinara katika sekta ya makazi nchini ikiwa na wataalam zaidi ya 200 wa ujenzi katika kada mbalimbali.

Mfano, katika mwaka 2026/27 NHC limepanga kukamilisha miradi mbalimbali ikiwamo wa Kawe, wenye thamani ya Sh169 bilioni wa nyumba 422, Mradi wa Samia Housing na Dodoms Medeli. Imepanga pia kutekeleza miradi mipya ya Ndijengwa, Iyumbu na Dar es Salaam, nyumba 800 za gharama nafuu.

Katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kasi, mwelekeo wa NHC unaonesha wazi kuwa mafanikio ya kweli yanatokana na mchanganyiko wa ubunifu, mifumo imara ya kisasa na rasilimali watu wenye uwezo.

Kwa mtazamo huu, NHC haiishii kujenga nyumba pekee, bali inachangia kujenga uchumi, miji na mustakabali wa maisha bora kwa Watanzania.

Hilo linadhihirishwa na ukweli kwamba tangu kuanzishwa kwake,  mtaji rasilimali wa NHC umepanda kufikia Sh bilioni 6.2 trilioni kutoka Sh5.6 trilioni mwaka 2025.

NHC imepata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka mitano mfululizo, pia imeongeza mapato kwa wingi wa nyumba zake na kuandika rekodi ya kujikusanyia Sh1.5 bilioni kwa miaka mitano.

Si hivyo tu bali imepata tuzo mbalimbali za Rais, ikiwamo ya kuwa mmoja wa wachangiajiwakubwa wa Gawio la Serikali kwa kutoa Sh10 bilioni pamoja na tuo ya Shirika la Umma lililofanikiwa kwa mageuzi makubwa ya kimapato na utawala bora.   

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi