Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Katavi, Godfrey Isaya amewasisitiza watumishi wa mahakama kuwa waadilifu, wenye tabia njema, kuepuka hali ya kuwa miungu watu na kila mmoja afanye kazi kwa bidii na umoja.
Jaji Isaya alisema hayo alipofanya ziara ya ukaguzi wa mahakama kuanzia Aprili 28 mwaka huu hadi Mei 7 mwaka huu katika Wilaya ya Mpanda, Mleke na Tanganyika kwa ajili ya kuangalia utendaji kazi wa kila siku wa utoaji huduma za haki kwa wananchi.
Katika ziara hiyo alitembelea vituo vyote vya Mahakama za Mwanzo vinavyoendelea kujengwa ndani ya Mkoa wa Katavi kama vile Sibwesa, Ugalla na Mamba na kupata wasaa wa kuwasisitiza watumishi wa maeneo hayo kuendeleza na mapambano ya matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji haki kwa wananchi wanaowahudumia.
"Kazi ya utoaji haki sio jambo dogo hivyo watumishi wasijiingize katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu taswira ya Mahakama na kupunguza imani kwa wananchi,
“Watumishi nawasisitiza kuwa waadilifu kwa kuwa ndiyo msingi mkubwa wa kutoa haki, muwe na tabia njema kazini na nje ya kazi na tuendelee kuchapa kazi tuwatumikie wananchi.
" Tuepuke ile hali ya kuwa miungu watu kwenye ofisi zetu na kila mmoja afanye kazi kwa bidii na umoja,” alisema Jaji Isaya.
Katika hatua nyingine Jaji Isaya aliwapongeza watumishi wote kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika hususani usikilizwaji wa mashauri kwani katika taarifa zote zilizowasilishwa zimeonyesha kuwa mashauri yanafunguliwa na yanaisha kwa wakati.
Mwisho

Chapisha Maoni