Jumanne, 5 Agosti 2025

KUTOPIGA MSWAKI IPASAVYO CHANZO CHA MAGONJWA YA FIZI – DK. KAHAMBA

Kutopiga mswaki ipasavyo kumetajwa kuwa ni chanzo cha magonjwa ya fizi, yanayowakabili watu wengi bila wenyewe kufahamu, huku wakiaswa kupiga mswaki ipasavyo ili kuepuka tatizo hilo.

Dk. Jawadu Kahamba

Rai hiyo imetolewa na Mtaalam wa Kinywa na Meno, Dk. Jawadu Kahamba kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, wakati akitoa elimu ya kinywa na meno kupitia Kitengo cha Habari na Uhusiano cha hospitali hiyo.

Dk. Kahamba amesema kuwa watu wamekuwa wakikumbwa na magonjwa ya fizi kutokana na kutopiga mswaki ipasavyo na kutotumia dawa ya meno yenye madini ya kulinda fizi, yakiwemo fluoride.

“Kutopiga mswakiipasavyo na kutotumia dawa zinazolinda fizi ni tatizo kubwa linalosababisha magonjwa ya fizi. Mtu anatakiwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, yaani asubuhi na usiku kabla ya kulala. Hiyo ndio hali ya kawaida,” amesema Dk. Kahamba.

Ametaja sababu nyingine za watu kupatwa na magonjwa ya fizi kuwa ni uvutaji wa sigara, ulaji wa ugoro pamoja na ulaji hafifu wa vyakula vyenye madini ya Vitamini C, hasa matunda.

Kwa kujibu wa Dk. Kahamba, dalili za maradhi ya fizi ni pamoja na maumivu, kuvimba, vidonda na fizi kutokwa damu na usaha wakati wa kupiga mswaki.

Amewataka itiza wananchi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Bukoba na nyinginezo nchini kwa ajili ya kupata huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya kinywa na meno walau mara mbili kwa mwaka.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni