Kaka ambwaga dada kesi ya mirathi Tabora

-Ni ya nyumba ya Zena Jalalkhan - Mahakama yasema Mleta Maombi amedai nyumba ya Zainab si Zena Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com MAHAKAMA ya Wilaya ya Nzega imetupilia mbali maombi ya Salma Kassam aliyetaka mahakama hiyo ichunguze usahihi na uhalali wa kaka yake kuteuliwa kusimamia mirathi ya mama yao Zena Jalalkhan. Jengo la Mahakama,wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora. Uamuzi wa Mahakama hiyo umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi N. Mkadam, baada ya kupitia maombi na majibu ya Mjibu Maombi. Katika shauri hilo, Mleta Maombi ni Salma Kassam na Mjibu Maombi ni kaka yake Karim Samji. Mleta Maombi aliwasilisha maombi yake chini ya hati ya dharura na kuambatanisha hati ya kiapo. Katika maombi yake, Salma alikuwa na hoja tatu, ikiwamo kuiomba mahakama uufanyie marejeo mwenendo wa shauri la mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Nyasa na hukumu iliyotolewa kwenye shauri hilo la mirathi namba 23 na 35 ya mwaka 2023. Aliomba mahakama ichunguze usahihi na uhalali wa Mjibu Maombi...