-Ni ya nyumba ya Zena Jalalkhan
- Mahakama yasema Mleta Maombi amedai nyumba ya Zainab si Zena
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
MAHAKAMA ya Wilaya ya Nzega imetupilia mbali maombi ya Salma Kassam aliyetaka mahakama hiyo ichunguze usahihi na uhalali wa kaka yake kuteuliwa kusimamia mirathi ya mama yao Zena Jalalkhan.
![]() |
Jengo la Mahakama,wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora. |
Uamuzi wa Mahakama hiyo umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi N. Mkadam, baada ya kupitia maombi na majibu ya Mjibu Maombi.
Katika shauri hilo, Mleta Maombi ni Salma Kassam na Mjibu Maombi ni kaka yake Karim Samji.
Mleta Maombi aliwasilisha maombi yake chini ya hati ya dharura na kuambatanisha hati ya kiapo.
Katika maombi yake, Salma alikuwa na hoja tatu, ikiwamo kuiomba mahakama uufanyie marejeo mwenendo wa shauri la mirathi katika Mahakama ya Mwanzo Nyasa na hukumu iliyotolewa kwenye shauri hilo la mirathi namba 23 na 35 ya mwaka 2023.
Aliomba mahakama ichunguze usahihi na uhalali wa Mjibu Maombi kuteuliwa kusimamia mirathi namba 23 inayohusu marehemu Asha Jalal na mirathi namba 35 inayomuhusu marehemu Zena Jalalkhan.
Pia aliomba mahakama itoe amri kwa mjibu maombi kulipa gharama za kesi na amri nyingine itakayoona inafaa.
Hakimu Mkadam alisema kwa kifupi kwamba Mleta Maombi aliteuliwa katika shauri la mirathi namba 24 la mwaka 2023 kusimamia mali za Zainab Jalalkhan maarufu Zena Jalal na Mahakama ya Mwanzo Nyasa.
Ilidaiwa kuwa marehemu aliacha watoto wawili na nyumba moja namba 38 iliyopo Nzega, Barabara ya Singida ambayo awali ilikuwa namba 10.
Mleta Maombi alidai alikuja kubaini kwamba Mjibu Maombi alifungua mirathi namba 35/2023 kwenye Mahakama ya Nyasa na akateuliwa kuwa msimamizi wa mali za marehemu huyo huyo.
Katika majibu yake aliyowasilisha kupitia kiapo kinzani, Mjibu Maombi alidai hakuna mahakama yoyote Tanzania iliyomteua kusimamjia mali za marehemu Zainabu Jalalkhan maarufu Zena na hakuna maombi namba 35/2023 katika Mahakama ya Nyasa ya kuomba kusimamia mirathi ya Zainabu.
Alidai aliteuliwa kusimamia mirathi namba 23/2023 ya marehemu Asha na mirathi namba 35/2023 ya marehemu Zena na sio Zainabu.
Hakimu Mkadam alisema Mleta Maombi ameiomba mahakama isimamie maslahi yake katika mirathi ya Zainabu Jalal shauri namba 24/2023, akaomba marejeo dhidi ya Mjibu Maombi aliyeteuliwa kusimamia mirathi ya Zena Jalal kwenye shauri namba 35/2023 na Asha shauri namba 23/2023.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili Mahakama iliona maombi ya marejeo yalikosa miguu ya kusimamia, Mleta Maombi (Salma),alikosea kuwasilisha maombi hayo wakati aliteuliwa kusimamia mirathi ya Zainabu Jalalkhan kwenye shauri namba 24/2023.
"Mleta Maombi alikosea pia kumshtaki Mjibu Maombi wakati Mjibu Maombi aliteuliwa kusimamia mirathi ya Asha Jalal katika shauri namba 23/2023 na Zena Jalal kwenye shauri namba 35/2023.
Kuendelea na maombi ya Mleta Maombi ni kupoteza muda wa mahakama na kupoteza muda wa wadaawa pande zote mbili,"amesema Hakimu Mkadam nakuendelea;
"Kutokana na mazingira hayo, mahakama inatupilia mbali maombi ya marejeo kutokana na sababu nilizoeleza hapo juu, hakuna amri nyingine inayotolewa na mahakama hii kuhusu gharama."
Mahakama ya Mwanzo Nyasa ilimteua Karim kuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya marehemu Zena, ambayo ni nyumba iliyopo wilayani Nzega mkoani Tabora yenye namba NTC/NMSH/NTI/81..
Mahakama hiyo pia ilimteua Salma Kassam kuwa msimamizi wa mirathi ya Zainabu Jalalkhan, inayohusisha nyumba hiyo hiyo iliyopo wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Hata hivyo, katika nyaraka mbalimbali za nyumba hizo ikiwemo risiti za kodi ya pango iliyowasilishwa mahakamani, zinasomeka kwa jina la Zena Jalalkhan na si Zainabu Jalalkhan.
Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Azaz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto wa marehemu.
0 Maoni