Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
SHAHIDI wa Jamhuri, E7483 Sajenti Pashua (53) ameiambia mahakama kuwa watuhumiwa wawili waliokamatwa bandarini, walikutwa na kiroba cha mchele, chenye kifurushi kilicho na chenga zilizosadikiwa kuwa dawa za kulevya aina ya heroine ndani yake.
Amesema watuhumiwa hao kutoka Ofisi za Azam wanafanya kazi kupakia mizigo kwenye boti ya kwenda Zanzibar .
Shahidi huyo wa Jamhuri ameeleza hayo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Sedikia Kisanya.
Shahidi huyo. aliyesema kwa sasa anafanya kazi Kituo cha Polisi Liwale tangu Desemba 2024, ambapo kabla ya kwenda huko alikuwa Kituo cha Polisi Bandari. Amesema Desemba 24 mwaka 2019 akiwa kazini katika eneo la abiria wanaokwenda Zanzibar, saa kumi jioni aliitwa na Koplo Anna aliyekuwa katika mashine ya ukaguzi wa abiria wanaotoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.
Alidai alipofika alielezwa na Koplo Anna kuwa wakati wa ukaguzi wa mizigo walikuta kiroba cha mchele, ndani yake kulikuwa na kifurushi chenye chenga zilizosadikiwa kuwa dawa za kulevya.
Amedai alimuhoji mtuhumiwa Kasema Muongota kuhusu mzigo, naye akadai kazi yake ni kubeba mzigo kutoka Ofisi za Azam na kuufikisha katika boti.
"Nilimpigia mhusika wa mizigo kwenye Ofisi ya Azam, Ismail Issa na nilimuhoji kuhusu mzigo ambapo alisema uliletwa na mteja wao anayesafirisha mizigo mara kwa mara,"amedai shahidi huyo.
Amesema watuhumiwa wote wawili aliwaweka chini ya ulinzi na kujaza hati ya ukamataji mali ikiwa na kiroba cha mchele, chenye nembo ya Azam, kilichokuwa na jina la Saidi Mohammed, simu mbili za watuhumiwa Kasema na Ismail kisha kuwasainisha katika kielelezo hicho.
Sajenti Pashua alidai kiroba hicho cha mchele ndani kikiwa na kifurushi kinachosadikiwa dawa za kulevya kilikuwa kinasafirishwa kuelekea Zanzibar.
Alidai katika ushahidi wake kuwa majina ya watuhumiwa yaliyopo juu ya bahasha ya kielelezo ni Ismail na Kasema ambao hawapo kizimbani.
Washtakiwa waliopo kizimbani wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina heroine ni Mohammed Ramadhani, Khalid Ally, Said Ngokonda na Said Adinani Ally.
Washtakiwa wanadaiwa Desemba 24 mwaka 2019 katika Ofisi ya Azam Marine walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 997.91.
0 Maoni