Jumamosi, 21 Desemba 2024

Serikali inavyoendelea kuimarisha miundombinu ya bandari

-Utendaji wa Bandari nchini waimarika kwa kipindi cha miezi saba (Mei-Novemba 2024) ikilinganishwa na (Mei-Novemba 2023)

Na Mwandishi Weti, daimatznews@gmail.com.           Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Mtwara,Tanga na zile zilizopo kwenye maziwa hali iliyochangia kuongeza ufanisi katika kuhudumia shehena. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumzia kuimarika kwa utendaji wa bandari nchini.

Katika kipindi cha mwezi Mei 2024 hadi Novemba 2024, kiwango cha shehena kilichohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ni tani milioni 16.5 ambayo ni zaidi kwa asilimia 5.92 ya shehena milioni 15.6 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023). 

Kwa upande wa idadi ya Makasha yaliyohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania katika kipindi cha Mei 2024 hadi Novemba 2024 ilifikia makasha 621,584 sawa na ongezeko la asimilia 3.29 ya makasha 601,805 yaliyohudumiwa katika mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).

Utendaji Bandari Dar es Salaam                            Katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 hadi Novemba 2024, kiwango cha shehena kilichohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam ni tani milioni 14.4 ambayo ni zaidi ya asilimia 5.6 ya shehena milioni 13.7 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).    

Shehena ya Makasha (Containers-TEUs)                Idadi ya Makasha yaliyohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam katika kipindi cha Mei 2024 hadi Novemba 2024 ilifikia makasha (TEUs) 598,672 sawa na ongezeko la asimilia  0.2 ya makasha  (TEUs) 597,613 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023). 

Shehena za nchi jirani Bandari Dar es Salaam  Katika kipindi cha Mei, 2024 hadi Novemba 2024  ilihudumia shehena ya nchi jirani (Transit) tani milioni 6.3 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 19.3 ya shehena ya nchi jirani iliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023) ambayo ilikua tani milioni 5.3. ikiwa kubwa kuliko ya kipindi kama hicho mwaka 2023.

Mafanikio uwekezaji DP World                       Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilisaini mikataba mitatu ya uwekezaji na Kampuni ya DP World (Dubai) Oktoba 22, 2023.

Mkataba huo ulihusisha uendeshaji wa shughuli za bandari katika uhudumiaji wa makasha, mizigo mchanganyiko na shehena ya magari.  

Ili kutoa huduma hizi kwa kuzingatia sheria za nchi yetu, Kampuni ya DP World ilifungua kampuni ya Tanzania inayoitwa DP World Dar es Salaam iliyokabidhiwa rasmi shughuli za uendeshaji wa bandari 15 Aprili, 2024.

Tangu kampuni hii ianze uendeshaji wa shughuli za bandari mafanikio mbalimbali yamepatikana kama ifuatavyo: Kwa mujibu wa mkataba, Kampuni ya DPW inapaswa kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 250 (Sh. Bilioni 675) katika kipindi cha miaka mitano.

 Katika kipindi cha miezi mitano tayari wameshawekeza Sh.214.425 Bilioni (31%) kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa; ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA; na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa bandari.

Wastani wa muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 mwezi Mei 2024 hadi kufikia wastani wa siku saba (7) ikiwa ni siku 0 kwa meli za makasha; siku 12 kwa meli za kichele; na siku 10 kwa meli za mizingo mchanganyiko.

Kutokana na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo, muda wa kuhudumia meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3), hivyo kupunguza idadi ya meli zinazosubiri kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.

Katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni.

Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya Sh. Billioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrahaba (royalty), na Ardhia (warfage).

Kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika, Serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya Sh. 1.922 Trilioni (USD 686.628 milioni) kwa kutumia makusanyanyo yanayopatikana. 

Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupakulia Mafuta (SRT); Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara); na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow Wharf) Dar es Salaam.

Kuunganishwa kwa mifumo ya Forodha (Tanzania Customs Integrated System - TANCIS) na ile ya bandari (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS). 

Hii imewezesha kupunguzwa na kuondolewa kwa mifumo iliyokuwa inafanana, hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.

Mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka hadi kufikia Sh. Trilioni 1 mwezi Septemba 2024 ikilinganishwa na wastani wa Sh. 850 bilioni kwa mwezi. Hii imetokana na TRA kuweza kuchakata mizigo mingi zaidi ndani ya muda mfupi.

Kwa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa kwa DP World na kampuni nyingine kuiendesha, yanaonesha kuwepo faidi kubwa kiuchumi kwa kuchochea kuongezeka kwa biashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Uwekezaji huu ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa azima ya Serikali ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa Lango Kuu la usafirishaji mizigo katika ukanda wa Afrika.   Bandar ya Tanga                                                         Kwa upande wa Bandari ya Tanga , Serikali  imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi Bilioni 429 kwa awamu mbili kuboresha bandari ya Tanga hatua ambayo imeongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutokana na wingi wa shehena inayopita katika bandari hiyo.         

Katika kipindi cha miezi mitatu ya robo ya kwanza  ya mwaka huu wa fedha 2024/25, Bandari ya Tanga imevuka lengo kwa kukusanya mapato kiasi cha Sh. Bilioni 18.6 ambayo ni zaidi ya lengo lililowekwa la kukusanya Sh. Bilioni 11. Mapato hayo ni zaidi ya mapato yote  yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2019/2020 ya kiasi cha Sh. Bilioni 16.        

 Amesema meli zenye ukubwa tofauti zimekua zikitia nanga katika bandari hiyo, hatua inayoongeza kiwango cha  bidhaa na shehena ambazo awali zilikua hazipiti katika bandari hiyo zikiwemo shaba (copper) tani 33,000, Ammonium nitrate tani 41,000 na Sulphur tani 100,004

Sheria Bodi ya Uchukuzi yaja

Na Hussein Ndubikile,daimatznews@gmail.com

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya uchukuzi inandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Bodi ya Uchukuzi kwa lengo la kuwatambua na kuwasajili wana taaluma hao.

Kauli hiyo imetolewa jijini humo na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile pichani juu, katika Mahafali ya 40 ya Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji  (NIT), mkoani Dar es Salaam, Desemba 22,2024.
"Bodi hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia weledi na maadili ya watalaam wa uchukuzi Tanzania Bara," amesema Kihenzile na kuongeza;

"Uanzishwaji wa bodi hiyo una lengo la kuhakikisha  kazi zote za usafirishaji zinasimamiwa na watu wenye taaluma stahiki."

Akizungumzia kuhusu NIT, Naibu Waziri.  Kihenzile amesema Serikali itaendelea kukiwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kwa kukiboreshea miundombinu yake ya kufundishia ili kuhakikisha  kinatimiza majukumu yake ya kuandaa wataalam, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika sekta ya uchukuzi kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Kihenzile ametoa rai kwa  wadau mbalimbali wa usafiri na usafirishaji  kuunga mkono jitihada za Chuo katika kuwapatia nafasi za mafunzo kwa vitendo wanafunzi na kuendeleza bunifu zinazozalishwa chuoni ili zitumike kwa maendeleo ya nchi.

Ametoa rai kwa wadau na wafaidika wa shughuli za chuo, taasisi za umma na binafsi kuunga mkono jitihada za chuo hicho katika kupata nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kuendeleza bunifu zinazozalishwa chuoni hapo ili ziweze kutumika kwa maendeleo ya nchi.

“Serikali  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo NIT ipo katika hatua za kuandaa mapendekezo ya kutunga sheria ya Bodi ya usajili wa wataalam wa uchukuzi lengo likiwa ni kuwa tambua,  kuwasajili na kusimamka weledi wa maadili  ya wataalam wa uchukuzi Tanzania Bara ili kuhakikisha  kazi zote za usafirishaji zinasimamiwa na watu wenye taaluma stahiki” amesema Naibu Waziri huyo.

Awali, Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi  Dk. Prosper Mgaya amesema katika mahafali hayo  wahitimu 4,176  wametunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali kati yao wanaume  ni 2,581 na wanawake 1,595.

Akizungumzia  changamoto amesema, chuo hicho kimekuwa na mikakati ya kukabiliana nazo  zikiwemo za miundombinu, upungufu wa rasilimali watu na ongezeko la udahili wa wanafunzi kwa kuweka mikakati mbalimbali.

Amesema pamoja na mabweni chuo kinajenga ofisi,madarasa na karakana ambapo jumla ya majengo matatu yanajengwa na yanatarajiwa kukamilika Februari 2025 ambapo ujenzi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa EASTRIP.

Amesema chuo pia kinaanzisha kampasi mpya mkoani Lindi na Kilimanjaro ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika kampasi ya Dar es Salaam na kuhusu rasilimali watu ili kukabiliana nalo  wanaendelea kuomba vibali vya ajira Serikalini  ili kupunguza matumizi ya wahadhili wa muda.

Jumatano, 18 Desemba 2024

15 Mbaroni uhujumu miundombinu ya SGR

 -Wamo wachina, wakenya

-Wakutwa na tani Kilo 14,264.1 za nyaya za shaba


Na Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail,com

Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli linawashikilia watuhumiwa zaidi ya 15, wakiwemo raia wa China na Kenya kwa tuhuma za kuhusika na uharibifu wa miundombinu ya njia ya Reli ya Kisasa (SGR).
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli, Gallus Hyera akiungumza na  wanahabari .


Hayo yamebainishwa jijini humo, na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Gallus Hyera wakati akizungumza na waandishi wa habari Desemba 17/2024.

Kamanda Hyera amesema watuhumiwa hao waliwakamata wakiwa na kilo 14,264.1 (zaidi ya tani 14) za nyaya za shaba zilizokatwa kwenye njia hiyo ya SGR kwenye maeneo mbalimbali na kuuzwa kama chuma chakavu.

"Watuhumiwa hawa na nyaya za shaba, tuliwakamata kupitia misako na operesheni tulizofanya maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama," amesema Hyera na kuongeza,

"Kati ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo, wamo mafundi walioshiriki ujenzi wa miundombinu ya SGR, fundi umeme na wafanyabishara wanaojishughulisha na uuzaji na ununuzi wa chuma chakavu,".
Sehemu ya shehena ya nyaya za shaba waliokamatwa nazo watuhumiwa


Hyera amebainisha kuwa Novemba 28, 2024 maeneo ya Mdaula mkoani Pwani, walikamatwa watuhumiwa wakiwa na nyaya za shaba kilo saba.

"Mmoja kati ya watuhumiwa ni fundi umeme, mwajiriwa wa kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza ujenzi wa miundombinu ya SGR. Huyu ndiye anayekata nyaya maeneo mbalimbali. Jumla ya watuhumiwa watatu wamekamatwa," amesema.

Amefafanua kuwa Novemba 30, 2024 katika eneo la Visiga mkoani Pwani kwenye kampuni ya The African Light Investment Ltd inayomilikiwa na raia wa kigeni (China na Kenya) zilikamatwa nyaya za shaba zenye uzito wa kilo 882.5.

"Desemba 2, 2024 huko maeneo ya Visiga, Pwani ulifanyika upekuzi kwenye nyumba inayomilikiwa na The African Light Investment Ltd (Raia wa China na Kenya), katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa na nyaya mbalimbali za shaba zenye kilo 3687.9.

"Nyaya hizi zimetambuliwa kuwa zimetokana na uharibifu kwenye miradi ya SGR na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania). Jumla wamekutwa na nyaya kilo 4,570.4 na raw copper bars (vipande vya shaba) 44 zenye uzito wa kilo 971.5," amesema.

Kupitia taarifa za kiintelijensia, amesema eneo la Kisemvule zilikamatwa nyaya za shaba kilo 608.6 za Tanesco, kilo 37.6 (za SGR) na vipande vya shaba zilizozalishwa kwa kuyeyushwa nyaya za shaba kilo 5,517.4 kwenye kiwanda cha chuma chakavu cha Metal Chem International Co. Ltd. Watuhumiwa wawili wamekamatwa.

Desemba 5, 2024 eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti amesema walikamata kilo 65.5 za nyaya hizo kutoka kwa wanunuzi wa chuma chakavu. Pia walikamatwa watuhumiwa wakiwa na waya wa shaba kilo 6.5 wakiwa katika harakati ya kuuza.

Amesisitiza kuwa Desemba 13, 2024 mkoani Pwani walikamatwa wamiliki wa kiwanda cha Balochistan Group of Industrial (BGI) kutokana na taarifa za kiintelijensia wakiwa na waya wa shamba kilo 61, vipande vya shaba 19 vyenye uzito wa kilo 141 kutoka kwenye gari lenye namba T 141 DQG aina ya Fuso.

Amesema kuwa upekuzi ulipofanyika kiwandani zilikamatwa nyaya za shaba kilo 67 na vipande 426 vyenye uzito wa kilo 7,728 ambavyo ni zao la waya wa shaba.

Amesema shaba hiyo imetoka kwenye miundombinu ya miradi ya SGR na Tanesco na kwamba watuhumiwa wawili wamekamatwa.

Ameongeza kuwa jumla ya watuhumiwa 13 wamefikishwa mahakamani, kati yao wanane wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha kwa makosa ya uhujumu uchumi na watano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa makosa sawa na hayo.

"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote anayejipanga kufanya uhalifu huu wa kukata nyaya za shaba kwenye miradi ya SGR na Tanesco, watasakwa kwa nguvu zote, kukamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria," amesema.

Kwa upande wake,Meneja Ishara na Umeme kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Felix Mutashobya amesema uharibifu wa miundombinu unaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo hitilafu katika mfumo wa mawasiliano na umeme katika SGR.

"Matokeo yake inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa," amesema.

Mafia Boxing Promotions yaja na Knouck Out ya Mama

Ni Boxing Day

Na Hussein Ndubikile,daimatnews@gmail.com


Kampuni ya Mafia Boxing Promotions inatarajia kufanya Mapambano 13 ya Kimatatifa ya Mchezo wa Masumbwi yaliyopewa jina la Knouck Out ya Mama yatakayofanyika Disemba 26 mwaka huu katika Ukumbi wa Superdom Masaki jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa Kampuni ya Mafia Boxing Promotions, Jimmy Mafuvu akizungumza nawanahabari kuhusu  Mapambano 13 ya Kimatatifa ya Mchezo wa Masumbwi yaliyopewa jina la Knouck Out ya Mama yanayotarajiwa kufanyika Desemba 26,2024 katika Ukumbi wa Superdom Masaki jijini Dar es Salaam.Wengine pichani ni baadhi ya mabondia naviongoi wa kampuni hiyo

Akizungumza na wanahabari leo jijini humo Msemaji wa kampuni hiyo, Jimmy Mafuvu amesema lengo la kuyapa mapambano hayo jina la Knouck Out ya Mama ni kusapoti na kuunga mkono juhudi za kukuza sekta ya michezo zinzofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kwamba amechangia vijana kujiajiri kupitia michezo.

" Tanzania inakwenda kupambana na mabondia mikanda mitano itapiganiwa kwa wakati mmoja hii ni mara ya kwanza mikanda hii kupiganiwa hapa nchini," amesema Mafuvu.

Amebainisha kuwa mabondia watakaopigana na mabondia wa Tanzania  wnatoka nchi za Ghana, Afrika ya Kusini na Malawi na kwamba mabondia wote wamefanya maandalizi mazuri.

Amesisitiza kuwa mabondia wa Tanzania watakaopanda ulingoni waliweka kambi ya wiki mbili nchini Afrika Kusini hivyo anaamini watashinda mapambano yao.

Ameitaja mikanda itakayopiganiwa ni WBO, WBC Africa, WBF na IBA huku akiwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo kushuhudia historia ikiandikwa.

Ameongeza kuwa viingilio vya mapambano hayo ni Sh 100, 000 kwa VIP,   VIP B Sh 50,000 na kawaida Sh 20,000 huku watakaohitaji kuchukua meza ya watu 10 watalipa Sh Milioni 1.5.

Kwa upande wake, Muigizaji wa Filamu, Wema Sapetu amewaomba wananchi kjitokeza kwa wingi kuunga juhudi za Rais Dkt. Samia na kwamba anategemea mabondia wa Tanzania watafanya vizuri.

Nae, Msanii wa Filamu Chuchu Hans amewahimiza Watanzania kujitokeza ili kushiriki kuandika historia katika mchezo wa masumbwi.

Muigizaji FIlamu Shamsa Ford amempogeza Rais Dkt. Samia kwa kutoa sapoti katika sekta ya michezo hasa mchezo wa ngumi na kwamba kupitia mchezo mabondia wanawake wanashiriki.

Mtangazaji wa Kituo cha Runinga cha Clouds, Sakina Lyoka amesema kuwa Rais Dkt. Samia anatambua thamani ya michezo kwani amesaidia vijana wanawake kwa wanaume kujiajiri kupitia mchezo wa ngumi.

Tanzania, Korea Kusini zasaini Makubaliano Ujenzi wa Mradi wa Maji Taka Dar

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini kwa ajili ya Ujenzi wa Mradi Mfumo wa Uchakataji Maji taka Mkoa wa Dar es Salaam mradi utakaotumia zaidi ya Dola za Marekani Milioni 90 sawa takriban Sh220 bilioni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kushuhudia utiaji saini makubaliano hayo, Desemba 17,2024, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema tukio hilo ni matokeo ya ziara ya Rais Dk. Samia kutembelea Korea Kusini na kwamba mradi huo utatekelezwa kwenye wilaya za Kinondoni na Ilala kwa miezi 36.
Waziri waMaji, Jumaa Aweso (Wa kwanza kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila(Katikati) na  Balozi wa Korea Kusini nchini, Ann Ewunju wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa pande hizo, baada ya kutia saini makubalianohayoDesemba17,2024

Waziri Awesu ametumia mkutano huo kuwataka watendaji wa DAWASA kuhakikiaha wananchi wa mkoa huo wanapata maji safi na salama bila kuleta visingizio kwani kwa sasa maji yapo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo amezungumzia changamoto ya mtandao wa maji kutofika kwenye baadhi ya maeneo, huku akiomba kupungua kwa muda wa mgao wa maji na kumaliza changamoto ya mfumo wa maji taka.

Naye Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema mradi huo wenye thamani ya dola milioni 90 kutoka Korea kusini kupitia benki ya Exim ujenzi wake utatumia muda wa miezi 36 lengo likiwa ni kukabiliana na kiwango kikubwa cha maji yanayozalishwa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania ,Ann Ewunju, ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kwamba mradi huo unakwenda kutekelezwa kwa ubora na utakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Bwana harusi akimbia na gari aliloazima, aliuza

Adaiwa kutapeli Mil 90

Ajificha kwa mganga Pemba, polisi wamnasa

 
Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam tarehe 15 Desemba, 2024 linamshikilia Vicent Peter Massawe, mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi wa kuaminiwa.

Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutenengeza hisia kwa umma kuwa ametekwa na baadae kwenda kujificha Chakechake,Pemba visiwani Zanzibar nyumbani kwa mganga wa kienyeji aliyetajwa jina na polisi kuwa ni Hamis khalid.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam Desemba 17/2024, Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema ufutiliaji na mahojiano ya kina kati ya Polisi na mtuhumiwa {Baba harusi}, baada ya kupatikana alikiri kutenda makosa hayo, ambapo alilichukua pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shilingi milioni.55 na gari namba T 642 EGU aina Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa Sylivester Beda Massawe.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, Massawe alichukua tena Shilingi milioni 10 kwa kutumia udanganyifu kutoka kwa Ramadhani mkazi wa Magomeni, pia alichukua pesa pia kwa udanganyifu Shilingi milioni15 kutoka kwa Ramadhani Bakari mkazi wa Temeke.

"Mtuhumiwa amechukua pesa pia kwa udanganyifu Shilingi milioni tano kutoka kwa Resma Mbuguni Ofisa Rasilimali Watu CBE. Alichukua tena kiasi cha shilingi milioni nne kutoka kwa Asia Mohamed mkazi Madale," amesema Muliro na kuongeza:

"Kwa udanganyifu Massawe alichukua tena Shilingi milioni moja na laki tano kutoka kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Ngoma, mkazi wa Kibaha na aliendelea tena kwa udanganyifu kuchukua Sh milioni 8 kutoka kwa Fauz Suleimani Mussa, mkazi wa Tabata baada ya kumuuzia gari ambalo sio lake  bali aliazima siku ya harusi yake likiwa na namba za usahili T642 EGU aina ya Ractis mali ya Sylivester Beda Massawe.".

Kamanda Muliro amesema Novemba,18 mwaka huu Polisi Kigamboni ilipokea taarifa ya kupotea kwa Vicent Peter Massawe, Mfanyabiashara, iliyedaiwa hakuonekana tangu Novemba 18, 2024 baada ya harusi yake na alipotea huku akitumia gari hiyo.

"Baadae ilibainika mtuhumiwa aliiuza gari hiyo badala ya kuirudisha kwa mwenyewe, baada ya harusi yake Novemba 16, 2024 katika ukumbi wa Golden Jubilee,: amesema Kamanda Muliro..

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi kuhusu tuhuma  hizo unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limetoa onyo na tahadhari kwa kikundi cha watu wanne aliowaelezea kuwa kazi yao ni kujenga taharuki kwa umma kuwa kila anayepotea au kutoonekana, wao hujitokeza na kuandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa watu hao wamechukuliwa na gari hard top nyeupe na kulazimisha hisia kuwa ni vyombo vya dola vimehusika.

Amesema malengo makubwa ya kundi hilo kutoa taarifa za uzushi zenye taharuki ni kuichonganisha Serikali, Polisi na Wananchi. Jeshi halitasita kuwachukulia hatua kali na za kisheria wahusika ili kukomesha tabia hizo.


Jumanne, 17 Desemba 2024

Waandishi wataka Dudley Mbowe aende gerezani

-Kuuanza mwaka 2025 mahakamani 
-Ni kwa kushindwa kuwalipa
-Adaiwa kuvunja makubaliano mara mbili

Na Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Jengo la Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi Dar es Salaam 

MAHAKAMA Kuu Divish.eni ya Kazi, Januari 6,2025  inatarajia kuanza kusikiliza maombi ya waandishi wa habari Maregesi Paul na wenzake 9 wanaotaka Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe aamriwe kwenda gerezani kama mfungwa wa madai kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya misharaha yao.

Mbele ya Naibu Msaiji wa Mahakama Kuu, Mary Mrio mahakamahiyo imetoa uamuzi huo leo Desemba 17,2024 wakati shauri hilo lilipokuwa likitajwa.

Akiwakilisha wenzake, Maregesi aliieleza Mahakama kwamba hati ya wito ilimfikia Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliahidi kufika lakini hakutokea bila kuwepo taarifa zozote.

Msajili Mrio amesema kwa kuwa Dudley alishapelekewa wito, shauri hilo litaendelea Januari 6 mwakani 2025 na pande zote zinatakiwa kuwepo mahakamani.

Wanahabari hao waliamua kuwasilisha maombi ya kumkamata na kumweka gerezani Dudley kwa  kushindwa kuwalipa  tuzo yao waliopatiwa na mahakama na hata walipoingia kwenye makubaliano nje ya mahakama Aprili 22, 2024 ya kulipa misharaha mitano hadi Mei mwaka huu hakufanya hivyo hadi leo.
Dudley Mbowe

Waandishi hao walishinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) Julai 17, 2023 mbele ya Msuluhishi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114, lakini baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja walikubaliana kiwango hicho cha fedha kishuke hadi Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari, 2024, hata hivyo hakulipa na walipoingia katika makubaliano nje ya Mahakama pia akayavunja kwa kushindwa kutekeleza makubaliano.

Tanzania, Oman zasaini kuondoa utozaji kodi mara mbili

 Benny Mwaipaja, Oman

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetiliana saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi wakionyesha hati za makubaliano kuondoa utozaji kodi mara mbili kati ya nchi hizo.

Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut, Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Nchemba amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Samia Suluhu Hassan za kufungua uchumi wa taifa kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

"Mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi wa biashara kwa pande zote mbili." amesema Dk.Nchemba..

Kwa mujibu waziri huyo wa fedha, mkataba huo pia unalenga kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hasa kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sanjari na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda na kuongezeka ajira kwa wananchi.

"Wawekezaji wa Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili," amesema k. Nchemba.. 

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.

Dk. Nchemba amefafanua kwamba mkataba huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi na mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.


Jumatatu, 16 Desemba 2024

Serikali yatangaza mkakati wa kuendeleza ubunifu wananfunzi Sekta ya Usafirishaji

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Serikali ya Tanzania imeanzisha mkakati wa kutambua ubunifu na mchango wa wanafunzi katika sekta mbalimbali, hususan sekta ya usafirishaji, kwa lengo la kutumia ubunifu huo kuchangia maendeleo ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, akizungumza na  wanahabari, baada ya kufungua Kongamano la 11 la Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam Desemba 16,2024.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, wakati akizungumza kwenye Kongamano la 11 la Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ambapo pia wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao walitunukiwa zawadi.

Amesema kuwa wanafunzi wameonyesha uwezo mkubwa wa kubuni vifaa muhimu kwa sekta ya usafirishaji na kwamba serikali itafuatilia vifaa hivyo kwa kina ili kuona jinsi vinavyoweza kusaidia maendeleo ya sekta hiyo. Alisisitiza kuwa mchango wa wanafunzi unapaswa kuanza kutumika kwa ngazi ndogo na kupanda taratibu hadi kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi wa nchi.

Amebainisha kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni chuo muhimu kwa sekta ya usafirishaji, kikitoa mafunzo kwa marubani, mafundi wa ndege, na wataalamu wa fani nyingine muhimu. Alihimiza wanafunzi kutumia fursa za kiubunifu walizonazo ili kuingia sokoni na kuongeza thamani kwenye sekta.

“Wanafunzi watambue kuwa elimu wanayopata ni fursa kubwa. Ubunifu ni njia muhimu ya kujipatia nafasi katika soko la ajira na serikali iko tayari kusaidia juhudi hizi kufanikisha maendeleo,” amesema Prof. Kahyarara.

Kwa upande wake,Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Lutangilo, ameishukuru serikali kwa kuwekeza katika miundombinu ya chuo hicho, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni, madarasa, na ununuzi wa vifaa kupitia mradi wa Benki ya Dunia.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Zacharia Mganilwa, ametoa wito wa kuweka mipango thabiti na utekelezaji wenye uthubutu ili kuhakikisha nchi inanufaika na maendeleo haya.

“Mipango ikifanywa kwa umakini na utekelezaji ukawa wa bidii, changamoto zilizopo zinaweza kushughulikiwa kwa mafanikio makubwa,” amesema Mganilwa.

Hatua hiyo ya Serikali inalenga kukuza talanta za wanafunzi na kuimarisha sekta ya usafirishaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi endelevu.


Waziri Dk. Jafo: Serikali, Sekta Binafsi kuendelea kushirikiana kuongeza ajira

Na Hussein Ndubikile,daimatznews@gnail.com

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuboresha iundombinu kwa lengo la kuongeza ajira kwa Watanzania.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo akizungumza jijini Dar es Salaam leo Desemba16,2024 katika Uzinduzi wa Muonekano na chupa mpya ya lita moja ya juisi ya African Fruti inayozalishwa na Kompuni ya Bakhresa Food Products Limited (BFPL) 


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Desemba16,2024 katika Uzinduzi wa Muonekano na chupa mpya ya lita moja ya juisi ya African Fruti inayozalishwa na Kompuni ya Bakhresa Food Products Limited (BFPL), Dk. Jafo amesema sekta binafsi inategemewa kubeba jukumu la kuongeza ajira nchini.

“Serikali haiwezi kuwaajiri watu wote; sekta binafsi ndio nguzo ya kutengeneza ajira. Uwekezaji kama huu unasaidia vijana na wakulima kuongeza uzalishaji,” amesema Dk. Jafo, akitoa mfano wa uwekezaji wa zaidi ya Sh 700 bilioni wa Bakhresa.

Ameongeza kuwa miundombinu kama reli ya Standard Gauge inayotumia umeme (SGR) na barabara inaimarishwa ili kuchochea uzalishaji viwandani na kuhimiza Watanzania kupenda bidhaa za ndani.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufian, amesema bidhaa zinazotumia malighafi za ndani huchangia kukuza uchumi.

Amebainisha kuwa kiwanda hicho kimeongeza uwezo wa kuchakata matunda kutoka tani 50,000 hadi 100,000 kwa mwaka na bidhaa hizo zinauzwa katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Kenya, China na Mashariki ya Kati, zikichangia pato la fedha za kigeni kwa taifa na ajira kwa vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tetra Pak, Jonathan Kinisu, amesifu ushirikiano wa miaka 17 baina ya kampuni hizo, akisema umeleta teknolojia rafiki kwa mazingira na bidhaa bora zisizo na kemikali.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa BFPL, Salim Aziz, amesema kuwa malengo ya kampuni hiyo yanaendana na ajenda ya Serikali ya kukuza uchumi kupitia bidhaa za ndani na uundaji wa ajira.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo (Mbele kushoto) akipiga makofi baada ya kuzindua mwonekano  na chupa mpya ya lita moja ya juisi ya African Fruti inayozalishwa na Kompuni ya Bakhresa Food Products Limited (BFPL)Jijini Dar es Salaam leo Desemba16,2024. Wengine pichani ni watendaji wa BFPL.

Jumamosi, 14 Desemba 2024

NHC inajitosheleza kila eneo-Bodi ya Wakurugenzi

-Yajipanga kujenga nyumba za makazi mikoa 20

-Wizara, Bodi ya Wakurugenzi yafurahishwa

-Yataka iendelee kutimiza ndoto ya makazi bora kwa wananchi

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail,com

“Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kukua, linaendelea kukomaa, linajitosheleza kila eneo na sasa linaweza kuaminiwa kutekeleza mradi wowote mkubwa wa ujenzi wa nyumba, tunajivunia kuwa na kiwango bora katika utekelezaji miradi.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk. Sophia Kongela, akizungumza na wanahabari muda mfupi  baada ya kumaliza ziara ya bodi hiyo kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi za Wizara nane  za Serikali, Mtumba Dodoma, Desemba 11, 2024.


Hayo si maneno ya mwandishi wa makala haya, bali ni maneno ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk. Sophia Kongela katika majumuisho yake, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara za Serikali nane, unaotekelezwa na NHC katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma Desemba 11, 2024. 
NHC pia inasimamia ujenzi wa majengo mawili ya Serikali katika eneo hilo.

Katika ziara hiyo Dk.Kongela aliambatana na wajumbe wa Bodi anayoiongoza, ambapo kwa pamoja walishuhudia miradi hiyo ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika, kabla ya kuanza kutumika.

Kupitia mkataba wake na Serikali, NHC inajenga majengo ya Wizara ya Nishati, Wizara Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Wizara ya Madini, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Pia inajenga ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Nishati, huku ujenzi wa miradi hiyo ukifikia asilimia 90.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah akionyesha wanahabari (hawapo pichani), namna wataalam wa ujenzi wa shirika hilo wanavyokamilisha hatua za mwisho za ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maeneleo ya Makazi,wakati Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ilipotembelea na kukagua mradi huo katika Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma Desemba11,2024.
Kwa mujibu wa NHC miradi yote nane inatarajiwa kukamilika  na kukabidhiwa kwa wahusika Januari 31, mwaka 2025.
Dk. Kongela anasema kuwa utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi umeleta picha kubwa kwamba NHC ina hazina ya wataalam.

“Ni fahari kuwa wataalam vijana wanaotekeleza mradi huu, ni hazina kwa NHC na taifa kukamilisha mradi mkubwa bila kuwa na wataalam wa kigeni,” anasema Dk.Kongela.

Kuhusu kukamilika, kukabidhi na kuanza kutumika majengo hayo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC anasema:

“Ushauri wangu Menejiimenti ya NHC kupambana kwa muda mfupi uliopo kukamilisha mradi ndani ya muda. Hiyo ndiyo fahari yetu, sote tunapambania jambo hilo.”

  • Msimamizi wa ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Nishati, Mhandisi Mary Kaaya wa NHC (Mbele), akiwaonyesha wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, waliomzunguka ramani na hatua za ujenzi wa jengo hilo ulipofikia wakati bodi hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo Desemba 11,2024 Mtumba, Dodoma, 

Akizungumzia mikakati ya baadae ya Shirika la Nyumba laTaifa, Dk, Kongela anasema katika bajeti ya mwaka 2025/26 NHC ina mpango wa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za makazi zikitarajiwa kunufaisha Watanzania wenye uhitaji wa nyumba. 

“Tutakuwa na mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za makazi, nyingi zitajengwa na Dodoma ni kipaumbele, mradi wa Medeli awamu ya pili utaiongezea makao makuu ya Serikali hadhi katika makazi,”anasema Dk, Kongela.

Anaongeza kuwa ujenzi wa nyumba za makazi utawafikia hata wananchi wa Kahama wenye hamu ya kupata nyumba za NHC na kwamba shirika hilo linatambua uhitaji wa nyumba za makazi kila mkoa.

Mkurugenzi wa NHC, Hamad Abdallah, akisikiliza maoni ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo walipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Ofisi naneza Serikali, Mtumba mkoani Dodoma, Desemba 11,2024. 

“NHC ina orodha ya mahitaji ya nyumba za makazi, sio Kahama peke yake, mikoa 20 itaanza kuongezewa nyumba za makazi,” anasema Mwenyekiti huyo wa Bodi ya NHC huku akitoa maagizo;

“Kwa Menejimenti tunaelekeza,ndoto yetu ni kuona NHC inatimiza haja ya uhitaji wa nyumba za makazi kwa wananchi, wafanye yote ndani ya muda, itekeleze hayo.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Mhandisi Anthony Sanga aliyefika kwenye eneo hilo ameipongeza Bodi ya NHC kwa kukagua maendeleo ya ujenzi huo akiwasihi NHC kuongeza kasi kukamilisha kazi hiyo.

“Nimewasihi waongeze kasi, ujenzi ukamilike ili Januari 2025 tuingie na kufanyia kazi humu. 

Hatuna shaka na ubora wa kazi ya NHC. Sasa wanamalizia, Bodi na Menejimenti ya NHC wanafanya kazi nzuri, sisi wasimamizi wa Wizara tumeridhika,” anasema Mhandisi Sanga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthon Sanga na Mkurugenzi wa NHC,Hamad Abdallah wakiingia katika jengo la wizara hiyo lililo katika hatua za mwisho kukamilishwa na NHC,wakati Bodi ya Wakurugenzi ilipotembelea nakukagua mradi huo Desemba 11, 2024, Mtumba jijini Dodoma,  

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah anasema wamejipanga mwaka ujao kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa ofisi za Wizara za Serikali na kwa kuwa wapo hatua za mwisho kukamilisha. 

Anasema wameona ni vyema Bodi ya Wakurugenzi itembelee mradi huo na kuona maendeleo ya mradi, thamani halisi ya fedha zinazotumika na gharama kulinganisha na ufanisi na kiwango cha mradi. 

“Kwa ujumla ziara imekwenda vizuri, Bodi imechangia ufanisi wakazi hii kwani ndiyo inatusimamia hasa katika miradi ya Serikali nao wamekuwa wakitaka kuona maendeleo ya miradi mara kwa mara, bila usimamizi wa Bodi maana yake hakuna usimamizi mzuri,” anasema Hamad na kuongeza; 

“Sisi menejimenti kila miezi mitatu tunapeleka taarifa kwa Bodi, bahati nzuri Bodi ya NHC inafanya maamuzi yenye tija. Maamuzi yao mazuri, usimamizi wao unatuwezesha kukamilisha kazi hii kwa wakati.”

Anasema mbali ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti ya NHC ina Kamati za Utekelezaji zinazofanya kazi katika miradi ya Serikali ikiwamo huo wa Ujenzi wa Ofisi za Wizara nane za Serikali Mtumba, Dodoma na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa kila mwezi na yeye (Mkurugezi) huziwasilisha kwa Bodi. 

Ametaja moja ya faida ya mradi huo ni kuzalisha ajira hasa kwa vijana  na kupata fursa za kujifunza umahiri wa taaluma mbalimbali zinazoendana na fani ya ujenzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhandisi Anthon Sanga (aliyevaa suti), akiwa pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC,Dk. Sophia Kongela (wa kwanza kushoto), wajumbe na wake na Menejimenti ya NHC wakati bodi hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo.  

“Tumetoa ajira hapa, asilimia mia moja tumeajiri vijana wa kitanzania,hapa wapo wataala vijana tunajivunia,wapo ambao wanafanya kazi na wanapata mafunzo na kuwa mahiri mfano katika eneo la kupiga rangi,” anasema Hamad. 

Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHC, anaweka wazi gharama za kazi hiyo kuwa ni shilingi bilioni 186.8 akichanganua kwamba  mradi wa ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.30, Wizara ya Viwanda unajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 22.99, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo utagharimu shiingi bilioni 22.84 na jengo la Wizara ya Madini ukigharimu shilingi bilioni 22.84.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ujenzi wake unagharimu shilingi bilioni 23.94 huku Wizara ya Nishati likigharimu shilingi bilioni 23,68 na la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 24. 98.

Jengo la ofisi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa na NHC katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, likiwa hatua za mwisho kukamilika,