Hot Posts

6/recent/ticker-posts

NHC inajitosheleza kila eneo-Bodi ya Wakurugenzi

-Yajipanga kujenga nyumba za makazi mikoa 20

-Wizara, Bodi ya Wakurugenzi yafurahishwa

-Yataka iendelee kutimiza ndoto ya makazi bora kwa wananchi

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail,com

“Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kukua, linaendelea kukomaa, linajitosheleza kila eneo na sasa linaweza kuaminiwa kutekeleza mradi wowote mkubwa wa ujenzi wa nyumba, tunajivunia kuwa na kiwango bora katika utekelezaji miradi.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk. Sophia Kongela, akizungumza na wanahabari muda mfupi  baada ya kumaliza ziara ya bodi hiyo kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi za Wizara nane  za Serikali, Mtumba Dodoma, Desemba 11, 2024.


Hayo si maneno ya mwandishi wa makala haya, bali ni maneno ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk. Sophia Kongela katika majumuisho yake, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara za Serikali nane, unaotekelezwa na NHC katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma Desemba 11, 2024. 
NHC pia inasimamia ujenzi wa majengo mawili ya Serikali katika eneo hilo.

Katika ziara hiyo Dk.Kongela aliambatana na wajumbe wa Bodi anayoiongoza, ambapo kwa pamoja walishuhudia miradi hiyo ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika, kabla ya kuanza kutumika.

Kupitia mkataba wake na Serikali, NHC inajenga majengo ya Wizara ya Nishati, Wizara Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Wizara ya Madini, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Pia inajenga ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Nishati, huku ujenzi wa miradi hiyo ukifikia asilimia 90.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah akionyesha wanahabari (hawapo pichani), namna wataalam wa ujenzi wa shirika hilo wanavyokamilisha hatua za mwisho za ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maeneleo ya Makazi,wakati Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ilipotembelea na kukagua mradi huo katika Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma Desemba11,2024.
Kwa mujibu wa NHC miradi yote nane inatarajiwa kukamilika  na kukabidhiwa kwa wahusika Januari 31, mwaka 2025.
Dk. Kongela anasema kuwa utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi umeleta picha kubwa kwamba NHC ina hazina ya wataalam.

“Ni fahari kuwa wataalam vijana wanaotekeleza mradi huu, ni hazina kwa NHC na taifa kukamilisha mradi mkubwa bila kuwa na wataalam wa kigeni,” anasema Dk.Kongela.

Kuhusu kukamilika, kukabidhi na kuanza kutumika majengo hayo Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC anasema:

“Ushauri wangu Menejiimenti ya NHC kupambana kwa muda mfupi uliopo kukamilisha mradi ndani ya muda. Hiyo ndiyo fahari yetu, sote tunapambania jambo hilo.”

  • Msimamizi wa ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Nishati, Mhandisi Mary Kaaya wa NHC (Mbele), akiwaonyesha wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, waliomzunguka ramani na hatua za ujenzi wa jengo hilo ulipofikia wakati bodi hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo Desemba 11,2024 Mtumba, Dodoma, 

Akizungumzia mikakati ya baadae ya Shirika la Nyumba laTaifa, Dk, Kongela anasema katika bajeti ya mwaka 2025/26 NHC ina mpango wa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za makazi zikitarajiwa kunufaisha Watanzania wenye uhitaji wa nyumba. 

“Tutakuwa na mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za makazi, nyingi zitajengwa na Dodoma ni kipaumbele, mradi wa Medeli awamu ya pili utaiongezea makao makuu ya Serikali hadhi katika makazi,”anasema Dk, Kongela.

Anaongeza kuwa ujenzi wa nyumba za makazi utawafikia hata wananchi wa Kahama wenye hamu ya kupata nyumba za NHC na kwamba shirika hilo linatambua uhitaji wa nyumba za makazi kila mkoa.

Mkurugenzi wa NHC, Hamad Abdallah, akisikiliza maoni ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo walipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Ofisi naneza Serikali, Mtumba mkoani Dodoma, Desemba 11,2024. 

“NHC ina orodha ya mahitaji ya nyumba za makazi, sio Kahama peke yake, mikoa 20 itaanza kuongezewa nyumba za makazi,” anasema Mwenyekiti huyo wa Bodi ya NHC huku akitoa maagizo;

“Kwa Menejimenti tunaelekeza,ndoto yetu ni kuona NHC inatimiza haja ya uhitaji wa nyumba za makazi kwa wananchi, wafanye yote ndani ya muda, itekeleze hayo.”

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Mhandisi Anthony Sanga aliyefika kwenye eneo hilo ameipongeza Bodi ya NHC kwa kukagua maendeleo ya ujenzi huo akiwasihi NHC kuongeza kasi kukamilisha kazi hiyo.

“Nimewasihi waongeze kasi, ujenzi ukamilike ili Januari 2025 tuingie na kufanyia kazi humu. 

Hatuna shaka na ubora wa kazi ya NHC. Sasa wanamalizia, Bodi na Menejimenti ya NHC wanafanya kazi nzuri, sisi wasimamizi wa Wizara tumeridhika,” anasema Mhandisi Sanga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthon Sanga na Mkurugenzi wa NHC,Hamad Abdallah wakiingia katika jengo la wizara hiyo lililo katika hatua za mwisho kukamilishwa na NHC,wakati Bodi ya Wakurugenzi ilipotembelea nakukagua mradi huo Desemba 11, 2024, Mtumba jijini Dodoma,  

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah anasema wamejipanga mwaka ujao kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa ofisi za Wizara za Serikali na kwa kuwa wapo hatua za mwisho kukamilisha. 

Anasema wameona ni vyema Bodi ya Wakurugenzi itembelee mradi huo na kuona maendeleo ya mradi, thamani halisi ya fedha zinazotumika na gharama kulinganisha na ufanisi na kiwango cha mradi. 

“Kwa ujumla ziara imekwenda vizuri, Bodi imechangia ufanisi wakazi hii kwani ndiyo inatusimamia hasa katika miradi ya Serikali nao wamekuwa wakitaka kuona maendeleo ya miradi mara kwa mara, bila usimamizi wa Bodi maana yake hakuna usimamizi mzuri,” anasema Hamad na kuongeza; 

“Sisi menejimenti kila miezi mitatu tunapeleka taarifa kwa Bodi, bahati nzuri Bodi ya NHC inafanya maamuzi yenye tija. Maamuzi yao mazuri, usimamizi wao unatuwezesha kukamilisha kazi hii kwa wakati.”

Anasema mbali ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti ya NHC ina Kamati za Utekelezaji zinazofanya kazi katika miradi ya Serikali ikiwamo huo wa Ujenzi wa Ofisi za Wizara nane za Serikali Mtumba, Dodoma na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa kila mwezi na yeye (Mkurugezi) huziwasilisha kwa Bodi. 

Ametaja moja ya faida ya mradi huo ni kuzalisha ajira hasa kwa vijana  na kupata fursa za kujifunza umahiri wa taaluma mbalimbali zinazoendana na fani ya ujenzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mhandisi Anthon Sanga (aliyevaa suti), akiwa pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC,Dk. Sophia Kongela (wa kwanza kushoto), wajumbe na wake na Menejimenti ya NHC wakati bodi hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo.  

“Tumetoa ajira hapa, asilimia mia moja tumeajiri vijana wa kitanzania,hapa wapo wataala vijana tunajivunia,wapo ambao wanafanya kazi na wanapata mafunzo na kuwa mahiri mfano katika eneo la kupiga rangi,” anasema Hamad. 

Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHC, anaweka wazi gharama za kazi hiyo kuwa ni shilingi bilioni 186.8 akichanganua kwamba  mradi wa ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.30, Wizara ya Viwanda unajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 22.99, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo utagharimu shiingi bilioni 22.84 na jengo la Wizara ya Madini ukigharimu shilingi bilioni 22.84.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ujenzi wake unagharimu shilingi bilioni 23.94 huku Wizara ya Nishati likigharimu shilingi bilioni 23,68 na la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 24. 98.

Jengo la ofisi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi linalojengwa na NHC katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, likiwa hatua za mwisho kukamilika,

 

   

Chapisha Maoni

0 Maoni