- Usajili wapaa
- Miliki Bunifu 7 zasajiliwa kila siku ndani ya siku 365
- Hataza 30
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),
umejidhatiti kutoa elimu kwa wananchi, wasanii, wabunifu, watafiti na taasisi
mbalimbali nchini kuhusu umuhimu wa kulinda na kusajili bunifu, sambamba na
kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Miliki Bunifu.
 |
Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo(aliyeketi kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa kuhusu utendaji BRELA. |
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wabunifu wananufaika na
kazi zao, kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Miliki Bunifu nguzo ya maendeleo
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya
Miliki Bunifu Duniani yaliyofanyika Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Dk. Selemani Jafo amesisitiza umuhimu wa wabunifu,
wajasiriamali na wasanii kusajili bunifu zao ili kulinda haki zao kisheria.
Waziri Jafo amesema kauli mbiu ya mwaka huu, “Miliki
Bunifu na Muziki: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu,” imelenga kuhamasisha
wasanii na wabunifu wa sekta mbalimbali kutambua kwamba bunifu ni mali kama
mali nyingine.
“Usajili wa bunifu ni hatua muhimu ya kuhakikisha wabunifu
wananufaika na kazi zao wakiwa hai, na hata baada ya kufariki warithi wao
watanufaika. Serikali imeweka mifumo thabiti ya ulinzi ili kuhakikisha ubunifu
unaleta tija kwa Taifa,” amesema Jafo.
Aidha, ameuelezea mpango mkubwa wa Serikali wa kujenga
viwanda 9,048 nchini kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwishoni mwa 2025 hadi
mwaka 2031, akisema unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya vijana milioni 6.5, ambapo
bunifu na miliki bunifu vitakuwa nyenzo muhimu katika ustawi wa viwanda hivyo.
Elimu ya Miliki Bunifu vyuo vikuu, taasisi za utafiti
BRELA imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa vyuo
vikuu, vyuo vya ufundi na taasisi za uzalishaji kuhusu umuhimu wa kulinda
bunifu kupitia usajili wa hataza na alama za biashara.
Akizungumza Aprili 16, 2024 katika Chuo cha Waislamu
Morogoro (MUM), Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa BRELA, Loy Mhando, alieleza:
“Bunifu nyingi katika vyuo zinatokana na tafiti
za wanafunzi na wahadhiri. Tunahimiza bunifu hizi zisajiliwe ili walinziwe
kisheria na ziweze kuwanufaisha wabunifu na jamii kwa ujumla.”
BRELA imetoa elimu katika vyuo mbalimbali vikiwemo;Chuo
Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), TaSUBa – Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni Bagamoyo,Chuo cha Mafunzo ya Ufundi VETA, SIDO na Innovation
Hub ya Taasisi ya Afya Ifakara (TAOTIC).
Lengo la BRELA kutoa elimu hiyo ni kuwajengea wabunifu
uwezo wa kulinda bunifu zao, kupanua masoko na kupata manufaa ya kifedha
kupitia tafiti na uvumbuzi.
 |
Loy Mhando |
Sauti za Wanufaika
Mmoja wa walionufaika na usajili wa Miliki Bunifu kutoka Kampuni ya TALANTA, Ronald Nakaka anasema kwa kusajili wa ubunifu unamwezesha kufanya kazi zake hadi nje ya Tanzania bila kikwazo kwani sheria ya kimataifa inampa ulinzi wa kazi zake hasa za sanaa ya muziki.
Anawahimiza watanzania hasa wajasiriamali vijana kusajili bunifu zao hatua inayoweza kuwafikisha kwenye ndoto zao kimaisha.
Siku ya Kimataifa ya Miliki Bunifu
Kila mwaka, BRELA hushiriki kuadhimisha Siku ya Kimataifa
ya Miliki Bunifu lengo likiwaa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na
kusajili bunifu.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, wadau kutoka COSOTA, BPRA,
COSOZA, vyuo vikuu, wajasiriamali na wasanii walishirikishwa, huku BRELA ikiendesha
warsha na mikutano ya wadau kujadili mikakati ya kukuza uelewa wa usajili wa
bunifu na kuongeza ubunifu wenye tija kwa Taifa la Tanzania.
Ushirikiano na wadau
 |
BRELA ilivyotoa elimu kwa wadau wake, taasisi za elimu na wajasiriamali kuhusu Miliki Bunifu. |
Katika eneo hilo BRELA imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali
ikiwemo; COSOTA (Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, BPRA (Wakala wa Usajili wa
Biashara na Mali Zanzibar) COSOZA, Taasisi ya Utafiti wa Mbegu, taasisi za
teknolojia na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO).
Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inaendelea kuimarisha
mifumo ya kitaifa na kimataifa ya ulinzi wa bunifu, ikiwemo rasimu ya Mkataba
wa Sheria ya Maumbo na Michoro Bunifu iliyojadiliwa Novemba 2024 jijini Riyadh,
Saudi Arabia.
Mchango wa vyombo vya habari
Vyombo vya habari nchini vimekuwa mshirika muhimu wa BRELA
katika kutoa elimu kwa umma.
 |
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile |
Katika warsha iliyoandaliwa na BRELA kwa wahariri,
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliwataka
wahariri kuwa mabalozi wa elimu ya miliki bunifu:
“Baada ya kupata elimu hii, tunapaswa
kuwafikishia Watanzania taarifa sahihi kuhusu miliki bunifu, umuhimu wa usajili
na namna ya kunufaika na kazi zao,” ameeleza Balile.
BRELA inahimiza vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu
na taasisi hiyo kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Faida za kusajili bunifu
Kwa mujibu wa BRELA, usajili wa bunifu unatoa manufaa
kadhaa, ikiwa ni pamoja na:
- Ulinzi
wa kisheria dhidi ya wizi au uvunjaji wa haki.
- Fursa
ya kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha.
- Kuongeza
thamani ya bidhaa na huduma kwa kutumia alama za biashara.
- Kupanua
masoko ya kitaifa na kimataifa.
- Kuwezesha
wabunifu kufaidika kifedha na kazi zao.
Kupitia mikakati yake ya utoaji elimu, ushirikiano na
wadau, na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa bunifu, BRELA imejidhatiti kuhakikisha
wabunifu, wasanii, watafiti na wajasiriamali nchini wanatambua thamani ya
bunifu na kunufaika nazo.
Serikali imesisitiza kuwa, ifikapo mwaka 2030, miliki
bunifu itakuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha
ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.
Changamoto
Hata hivyo, zipo changamoto zinazowakabili watanzania katika kulinda Miliki Bunifu na Hataza. Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Miliki Bunifu na Hataza(WIPO) , baadhi zikiwa ni ukosefu wa uelewa kuhusu Miliki Bunifu, Kushindwa kutekeleza Sheria ya Miliki Bunifu na Udhibiti mdogo wa matumizi yasiyo rasmi ya Miliki Bunifu na Hataza.
Msaada kwa wajasiriamali, wabunifu, wasanii
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa,(Pichani chini), amewataka
wasanii, wabunifu na wajasiriamali kusajili majina ya bidhaa na huduma
wanazotoa kupitia brand zao ili kuyalinda kisheria.
 |
Godfrey Nyaisa |
Kwa mujibu wa Nyaisa, usajili unawawezesha wabunifu kupata
haki ya kipekee ya kutumia bunifu zao na kuzuia mtu mwingine kuziiga au
kuzitumia kibiashara bila ridhaa yao. Aidha, unatoa fursa ya kukopesheka katika
taasisi za kifedha kwa kuwa BRELA inatoa vyeti vinavyotambulika kisheria. BRELA inavyoboresha mifumo
Nyaisa anabainisha kwamba BRELA imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaboresha mifumo ya usajili Miliki Bunifu na Hataza kwa kuanzisha mfumo wa usajili mtandaoni, Kuwezesha maombi wa njia rahisi na kutoa mwongozo wa watumiaji.
Naye Dk. Ashatu Kijaji, Waziri wa zamani wa Viwanda na
Biashara, amewataka wanawake wajasiriamali kusajili bunifu na biashara zao ili
kuongeza thamani ya bidhaa na kulinda haki zao kisheria.
“BRELA inazilinda bunifu na biashara kisheria.
Iwapo mtu ataiga kazi yako, una haki ya kumshtaki na BRELA itasimama
kukutetea,” amesema Nyaisa kwa niaba ya Dk. Kijaji.
Wadau kulinda bunifu kimataifa
BRELA, kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Ubunifu
Duniani (WIPO), imeandaa rasimu ya Mkataba wa Sheria ya Maumbo na Michoro
Bunifu inayolenga kuweka mfumo wa kimataifa wa kulinda bunifu.
Nyaisa, anasema kuwa sheria hiyo itakapopitishwa, wabunifu
wa maumbo, vifungashio, mavazi na michoro mbalimbali watapata fursa ya kulinda
bunifu zao katika nchi nyingi kwa kutumia ombi moja tu kupitia WIPO.
“Hii itapunguza gharama za ulinzi wa bunifu na kuongeza
ushindani wa bidhaa na huduma za wabunifu wa Kitanzania katika soko la
kimataifa,” anasema.
Hali ilivyo, muda na hatua za usajili
Akizungumzia hali ya usajili miliki bunifu ilivyo kwa sasa,
Ofisa Usajili kutoka BRELA, Stanlaus Kigosi anaeleza kuwa kadiri siku
zinavyokwenda, ndivyo mwamko wa watu kusajili kazi zao unavyoongezeka.
“Usajili sasa unachukua nafasi, mwamko unaongezeka kila
siku. Hii inatokana na BRELA inavyoendelea kujitahidi kuwafikia wajasiriamali,
vikundi vya wanawake, hata kutoa elimu kwenye vyuo vikuu na taasisi
mbalimbali,” anasema Kigosi, huku akibainisha kwamba takwimu kamili za Miliki
Bunifu zilizosajiliwa zipo nje ya uwezo wake.
Anafafanua kuwa katika usajili wa Miliki Bunifu, usajili wa
Alama za Biashara unafanyika zaidi kuliko usajili wa Hataza, jambo linalotokana
asili ya maeneo hayo mawili.
Wakati Alama za Biashara huweza kuchukua muda mfupi
kubuniwa na kuwasilishwa BRELA kwa usajili, HATAZA uhitaji muda zaidi kutokana
na kuhusisha zaidi Teknololojia ya Habari(IT), hivyo pia kuhitaji kuidhinishwa
na taasisi au bodi husika kabla kuziombea usajili w Miliki Bunifu.
Kuhusu muda wa usajili Miliki Bunifu, Kigosi anabainisha
kuwa usajili hufanyika na kukamilika ndani ya siku 90, ukijumuisha masuala
mbalimbali ya kisheria na kanuni ndani nan je ya nchi, ikiwemo kufanyia
uchunguzi Miliki Bunifu inayoomba kusajiliwa, kuitangaza kwa siku 60 ndipo
husajiliwa ikiwa haikuwekewa kipingamizi.
Gharama usajili Miliki Bunifu
Akihitimisha maelezo yake, Kigosi anasema usajili wa Miliki
Bunifu unaenda sanjari na kulipia gharama kwa mujibu wa sheria.
“Miliki Bunifu
husajiliwa kwa kulipiwa gharama ambayo ni Shilingi 130,000. Gharama hiyo ni
nafuu ikilinganishwa na zinazotozwa na nchi nyingi za Ukanda wa Afrika
Mashariki,” anasema Kigosi.
Takwimu Miliki
Bunifu
Akizungumza na mwandishi wa Makala haya, Mkuu wa Kitengo
cha Habari na Mawasiliano ya Jamii wa BRELA, Joyce Mgaya ameeleza kuwa mamlaka
hiyo ina Idara maalum inayokusanya na kuhifadhi takwimu za masuala mbalimbali
yanayosimamiwa na kutekelezwa na BRELA
ikiwemo Miliki Bunifu na Hataza.
“Katika mwaka mmoja uliopita, BRELA imesajili Miliki Bunifu
takriban 2,615. Lakini pia Hataza
zilizosajiliwa katika muda huo ni 30,” anasema Joyce.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara, wajasiriamali kuzingatia
sheria za nchi kwa kusajili Miliki Bunifu zao na Hataza, ili kuendana na
matakwa ya kisheria, lakini pia kunufaika ya usajili huo ambao ni ulinzi kwa
ubunifu na ugunduzi wao.
Serikali na Sera mpya ya Miliki Bunifu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi
Mwinjuma (Mwana FA), anasema Serikali ipo mbioni kukamilisha Sera ya Miliki Bunifu
itakayotoa mwongozo mpya wa ulinzi na usimamizi wa haki za wabunifu nchini.
“Maendeleo ya taifa yanategemea bunifu. Miliki bunifu
zitaongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja
mmoja na taifa kwa ujumla,” anasema Mwinjuma.
Sera hiyo itatoa mwanga kwa wabunifu kupata mikopo, kufikia
masoko makubwa zaidi na kunufaika na ubunifu wao kikamilifu.
Kwa jitihada zake na kujitambua, BRELA inaendelea kujidhatiti
na kuwa nguzo ya ulinzi na uendelezaji wa bunifu nchini. Inafanya hivyo kupitia
elimu, ushauri, sera na ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi.
 |
Ushindi wa BRELA katika kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Miliki Bunifu ni Ushindi wa Watanzania |
Taasisi hiyo inalenga kuweka mfumo imara wa kuhakikisha
wabunifu, wajasiriamali, wasanii na vyuo vikuu wananufaika na ubunifu wao.
Kwa usajili wa bunifu, Tanzania inalenga kuongeza kipato
cha wabunifu, kukuza sekta ya viwanda, kupanua soko la kimataifa na kuchochea
maendeleo ya taifa kwa ujumla.