Saa 144 za CCM kutaja kikosi chake bungeni

-Wagombea presha inapanda, presha inashuka

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Saa 148 zimesalia kuanzia leo Agosti 18, kabla ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutangaza majina ya wateule wake kwa nafasi za ubunge watakaochuana na wagombea vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba 29, 2025 ili kuingia bungeni. 

Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan

Muda huo ambao ni sawa na siku sita, unawaacha wagombea waliopita kwenye kura za maoni ngazi ya jimbo, presha zao zikipanda na kushuka, wakisubiri kwa hamu uamuzi wa vikao vya kitaifa vya CCM vya uteuzi, ambavyo uamuzi wake ni wa mwisho.

Vikao hivyo vinafanyika huku kukiwa na kumbukumbu ya baadhi ya wagombea majina yao kutorudi kwenye mchujo wa awali mwaka huu, lakini pia kuwepo waliokatwa kwenye uteuzi wa mwisho katika vikao kama hivyo, mwaka 2020 ambapo CCM ilikuwa chini ya uenyekiti wa hayati John Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Agosti 17, 2025, CCM kimetangaza ratiba ya vikao vyake vya kitaifa, kikieleza vitafanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa ya CCM, iliyotolewa na kusainiwa na  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla Agosti 17, 2025, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itafanya kikao chake Agosti 21 Agosti 2025, kikifuatiwa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).Taifa kitakachofanyika Agosti 23, 2025.

"Ajenda ya vikao hivyo itakuwa ni uteuzi wa; Wagombea Ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Viti Maalum, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalum," imeeleza taarifa hiyo ya CCM..

Taarifa hiyo imehitimisha kwamba, viikao vyote vitafanyika jijini Dodoma, yalipo makao makuu ya chama hicho

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi