Miezi 24 ya BRELA kuipigania Sheria ya Umiliki Manufaa

  --Yawafunda wamiliki wa kampuni, mawakili

-  Yaziwezesha taasisi za uchunguzi wa uhalifu kukabiliana na tatizo hilo

Na Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Katika harakati za kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye sekta ya biashara na makampuni nchini, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umechukua hatua thabiti ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kifedha na utambuzi, kuhusu utambuzi wa wamiliki manufaa wa kampuni na majina ya biashara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),  Godfrey Nyaisa akikabidhi Tuzo kwa wafanyakazi wa  taasisi hiyo iliyotunukiwa baada ya kutoa gawio kwa Serikali la Shilingi Bilioni 20.4  kwa mwaka 2024. BRELA imepata Tuzo hiyo katika kipengele cha Taasisi zilizofanya vizuri kwa utoaji gawio kwa wakati kwa mwaka 2025

.

BRELA imeeleza kuwa hatua hizo ni utekelezaji wa Pendekezo Na. 24 la Kundi Kazi la Kimataifa la Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FATF), linalosisitiza uwazi katika umiliki wa kampuni kama njia ya kuzuia matumizi ya kampuni katika uhalifu wa kifedha, kama vile utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.

Ikiwa ni wajibu wake kisheria kwa taifa, lakini pia utekelezaji wa sheria ya kimataifa, BRELA imefanya juhudi hizo kwa takriban miaka miwili, tangu mwaka 2023 yalipofanyika mabadiliko ya kisheria, ikitumia njia mbalimbali kupiga vita wanaokiuka sheria ya umiliki manufaa ambayoni ya kimataifa.

Njia ambazo BRELA imezitumia ni pamoja na kutoa elimu kwa taasisi za kiuchunguzi wa uhalifu, zinazosimamia sheria, wafanyabiashara hata taasisi za elimu ya juu, maeneo mbalimbali nchini.

Katika muda huo wa miaka miwili iliyopita BRELA imetekeleza jukumu hilo kwa kutoa mafunzo hayo, ambayo yalifanyika mikoa mbalimbali nchini yakihusisha taasisi saba muhimu za kitaifa.

Taasisi hizo ni pamoja na TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Nyingine ni Uhamiaji, Mahakama ya Tanzania pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, huku BRELA ikiweka wazi lengo kuu la mafunzo hayo kuwa ni kuwawezesha wadau hao muhimu kutekeleza kwa ufanisi jukumu lao la kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha kwa kushirikiana na wakala hiyo katika kutambua wamiliki halisi wa makampuni na majina ya biashara.

Kitaifa BRELA pia ina dhamana ya kuendesha na kuhifadhi kanzidata za usajili wa makampuni na majina ya biashara, hivyo kuimarisha ushirikiano na taasisi za uchunguzi ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa taarifa hizi nyeti zinatumika kwa ufanisi katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha.

Elimu hiyo pia inatolewa na BRELA kwa mawakili, taasisi binafsi, wamiliki wa kampuni na wafanyabiashara wakubwa, wa kati hata wa chini, ili kuepuka kuingia mikononi mwa sheria kwa kukiuka Sheria ya Umiliki Manufaa.

Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa BRELA, Isdori Nkindi, anaeleza kuwa; ”Kutokana na jukumu hilo, kila nchi mshirika wa FATF inapaswa kuhakikisha taasisi zake zote zinazohusika na kupambana na uhalifu wa kifedha, zinaelewa vyema namna ya kufikia taarifa sahihi za umiliki manufaa, ili kusaidia kuzuia uhalifu kabla haujatokea.”

Isdor Nkindi

Anasisitiza kwamba kutokana na ukweli kuwa BRELA ndiyo msimamizi wa sajili za makampuni na majina ya biashara nchini,  taasisi za uchunguzi zina wajibu wa kutumia taarifa hizo ipasavyo pindi tu vinapojitokeza viashiria vya uhalifu.

BRELA inaeleza kuwa hiyo ni mojawapo ya njia za kuzuia uhalifu kabla haujatokea, kwa kuhakikisha taasisi zote zinazungumza lugha moja na kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu.

Nkindi anawakumbusha maofisa wa taasisi hizo kufuata utaratibu wa kisheria wa kuomba taarifa kutoka BRELA kupitia taasisi zao, badala ya maofisa mmoja mmoja kuomba taarifa binafsi, jambo analosema linaweza kuathiri mchakato mzima wa ukusanyaji wa taarifa na ushahidi.

Mafunzo hayo yamepokelewa kwa mtazamo chanya na wadau walioshiriki, wakiwemo mawakili na wafanyabiashara, ambao walipata fursa ya kuelewa kwa kina dhana ya umiliki manufaa na umuhimu wake katika kusaidia utekelezaji wa haki na sheria nchini.

Kupitia mikakati hii, BRELA inaonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuhakikisha kuwa kampuni na biashara zilizopo nchini zinawajibika kwa mujibu wa sheria na hazitumiki kama kichaka cha kuficha uhalifu wa kifedha. Hii ni hatua muhimu kuelekea kujenga mazingira ya biashara yenye uwazi, uwajibikaji na uadilifu, yanayochochea maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.

Washiriki wa kikao kazi kuhusu Dhana ya Wamiliki Manufaa  iliyotolewa na BRELA kwa wadau, wakiwemo mawakili na wafanya biashara jijini Arusha, wakifuatilia mafunzo hayo mapema Februari 27, 2024.


Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, ndiyo yaliyopitisha marekebisho kwenye Sheria ya Kampuni Sura 212 pamoja na Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni na Kanuni za Majina ya Biashara (Umiliki Manufaa) za Mwaka 2023 pia kanuni zake kupitishwa na Waziri mwenye dhamana na biashara nchini."

Waandishi wa habari pia wana fursa ya kipekee kutumia vyombo vyao kusaidia kufikisha elimu kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa ili wadau na wananchi wote waielewe na kuitii. 

Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa BRELA, Isdori Nkindi, anasisitiza kwamba katika  kuisimamia Sheria ya Umiliki Manufaa, wanaendelea kuelimisha wadau, lakini pia kushirikiana na vyombo vya usalama kudhibiti na kuwasaka wanaovunja sheria hiyo.                                                  

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi