Waomba kuondolewa vikwazo biashara ya mazao ya kilimo Ikolojia mipakani

Mussa Juma,Arusha

Serikali katika nchi za Afrika ya Mashariki, zimeombwa kuondoa vikwazo vinayoathiri biashara za mazao ya kilimo Ikololojia mipakani, hasa kwa wajasiriamali wadogo, ili kuwezesha kukuza biashara hiyo.

Utafiti uliofanywa kuhusu biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani zimebaini kuwepo kwa changamoto kadhaa ikiwemo viwango vya ubora wa bidhaa,mifumo ya ulipaji kodi,vikwazo vya barabarani,udhibiti wa bidhaa zisizo na ubora na uelewa mdogo wa wajasiriamali katika masuala ya biashara ya mipakani.

Akisoma mapendekezo ya kisera yaliyotokana na  warsha ya wadau kuhusu biashara  ya mipakani kwa mazao ya bidhaa za kilimo Ikolojia, Ofisa wa Utetezi na Ushawishi wa Shirikisho la  Wakulima Tanzania (SHIWAKUTA), Thomas Laizer amesema   wamekubaliana kuwa ni  muhimu, kuchukuliwa hatua madhubuti ili kuondoa au kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs), ikiwemo mazuio yasiyo rasmi ya barabarani, ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri biashara za mipakani (cross-border trade).  

Laizer amesema  vikwazo hivyo  sio tu  vinavuruga mfumo wa kibiashara, bali vinamuumiza mkulima kutokana na ukweli kwamba wafanyabiasha huishia kununua mazao kwa bei ya chini kufidia hasara wanayoitarajia kukumbana nayo wasafirishapo mazao. 

"Hali hii huchochea wafanyabiashara na wazalishaji kutumia njia zisizo rasmi (njia za panya) kusafirisha mazao na bidhaa na hivyo kukosesha serikali mapato ambayo huyatumia kuwaletea wananchi maendeleo,"amesema

Amesema pia wanapendekeza Serikali na wadau, kuchukua hatua ya kuwekeza katika kuwaelimisha wakulima kuhusu mahitaji ya kisera na kisheria yanayohusu uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo ikolojia ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara za mipakani na kukuza uchumi wa kilimo endelevu.

Laizer amesema, pia wanaihimiza Serikali  kuchukua jukumu la msingi katika kuweka miundombinu wezeshi, sera rafiki na mikakati shirikishi ili kuwawezesha Watanzania kufikia masoko ya kimataifa kwa bidhaa ghafi na zilizosindikwa, hivyo kuongeza thamani ya mazao na kukuza pato la taifa.

"Tunatambua na kukubali kuwa uwepo wa wanunuzi na wafanyabiashara toka nje ni fursa kwa wazalishaji wadogo nchini na  Tunatoa wito kwa serikali yetu kuweka mazingira wezeshi na ya uwazi yatakayolinda maslahi ya wazalishaji wa ndani kwa kuhakikisha biashara inayoendeshwa inanufaisha wazalishaji hao, inazingatia haki na usawa, na serikali inapata mapato stahiki ili kuweza kuwaletea wananchi wake maendeleo"alisema

Laizer amesema  , wamekubaliana Serikali ya Tanzania inapaswa kuzijengea uwezo wa kirasilimali, ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na vifaa, mamlaka zinazodhibiti ubora wa mazao ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha walaji wanalindwa dhidi ya mazao yaliyozalishwa kwa kutumia pembejeo zenye viambata hatarishi kwa afya na mazingira.

Ameongeza kuwa wanapendekeza  Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutumia nafasi yake kuzihimiza nchi wanachama kuweka sera na mikakati ya pamoja itakayoielekeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ukanda wa uzalishaji na biashara ya mazao na bidhaa zilizozalishwa kiikolojia, kwa lengo la kulinda afya ya walaji, kuhifadhi mazingira na kuongeza ushindani wa bidhaa za ukanda huu katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Awali, wakizungumzia utafiti huo uliofanywa na Washauri wa Biashara za Kilimo Ikolojia mpakani, kwa udhamini wa  Shirika la Muungano wa Uhuru wa Chakula Afrika(AFSA), Ofisa Miradi wa SHIWAKUTA na MVIWAARUSHA,Damian Sulumo  amesema iwapo vikwazo vya biashara ya mazao ya kilimo Ikolojia vikiondolewa uzalishaji utaongezeka.

Sulumo amesema hata hivyo, bado kunahitajika mafunzo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia  ili kuboresha bidhaa zao na badala kuendelea kuuza nje bidhaa kama  malighafi wanatakiwa kuuza bidhaa zilizosindikwa katika masoko ya kimataifa.

Mshauri wa Biashara za Mazao ya Kilimo Ikolojia wa AFSA , Africa Kiiza  ambaye aliongoza utafiti huo, amesema anaamini mapendekezo waliyoyatoa baada ya utafiti huo, yatafanyiwa kazi.

Amesema AFSA ,kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali, ikiwepo wabunge wa EAC,Wanahabari  na wafanyabiashara wamazao ya kilimo Ikolojia.

Mratibu wa SHIWAKUTA,  Richard Masandika amesema utafiti huo uliofanyika katika mipaka ya  Tanzania na Kenya, Kenya na Rwanda na mipaka mingine katika nchi za Afrika ya Mashariki, umekuwa na manufaa makubwa.

Amesema wanaimani kuna taratibu za kikanda na kiserikali za EAC, zinazoweza kufanywa ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia.

Wadau wa kilimo Ikolojia katika nchi za Afrika ya Mashariki, wakiwepo wakulima, vyama vya wakulima, watafiti na wanahabari za kilimo Ikolojia walishiriki warsha ya siku mbili jijini Arusha, kuhusiana na utafiti uliofanywa wa AFSA  kuhusiana na biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi