Jumamosi, 18 Mei 2024

Majengo, eneo Urafiki vyauzwa kwa NHC

 -NHC yalipa mabilioni

- Ni kupitia mnada wa wazi, sasa mandhari kuboreshwa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limenunua rasmi eneo la Urafiki na majengo yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China (Tanzania - China Friendship Textile CO LTD). 

Sehemu ya majengo ya kilichokuwa la kiwanda cha Urafiki, ambayo sasa ni mali ya NHC.

Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kukagua maeneo mbalimbali, ambayo sasa yatakuwa chini ya miliki ya NHC na kufafanua kuwa eneo hilo linajumuisha nyumba, maghala, viwanja vya wazi, viwanda na mali nyinginezo.

Katika ziara yake, Saguya ameelezea furaha yake na matumaini makubwa kuhusu hatua hiyo, akibainisha kwamba itasaidia kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa maeneo hayo ikiwamo kuboresha mandhari ya Dar es Salaam.

Amesema kuwa NHC, imelinunua eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kutoka kwa mnada wa wazi kikiwa na thamani ya mabilioni ya fedha.

Mkurugenzi wa NHC (Wa kwanza kulia) akionyeshwa  sehemu ya eneo lililokuwa na Kiwanda cha Nguo Urafiki, Ubungo Dar es Salaam. Wa tatu kushoto ni Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya.

Amesema:"Kupitia umiliki huu mpya, Shirika la Nyumba la Taifa limejipanga kuboresha maeneo haya ili kuendana na malengo yetu ya kutoa makazi bora na ya kisasa kwa wananchi. Tumeanza kwa kulipima eneo lote na kutambua mipaka yote inayohusisha eneo hilo."

Kwa mujibu wa Saguya, eneo la Urafiki lina historia ndefu ya kuwa kituo muhimu cha viwanda na makazi, kikitoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania. 

"Hivi sasa, NHC inapanga kufanyia maboresho makubwa eneo hili kwa kujenga miundombinu bora, nyumba za kisasa na maeneo ya biashara ambayo yatavutia wawekezaji na wakazi wapya, "amesema Saguya.

Ameongeza: "Shirika la Nyumba la Taifa linaamini kuwa mradi huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwa ujumla na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya makazi na maendeleo ya kiuchumi nchini. Katika mpango wa maendeleo ya NHC, eneo la Urafiki litawekewa mkazo maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuwa linakuwa mfano bora wa maendeleo ya kisasa na endelevu."

Baadhi ya maghala ya kilichokuwa Kiwanda cha Nguo Urafiki ambayo sasa ni mali ya NHC.Picha zote kwa hisani ya NHC.

Saguya alihitimisha kwa kusema, "Hii ni hatua muhimu kwa NHC na kwa taifa letu. Tunawaomba wananchi na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zetu katika kuboresha na kuendeleza maeneo haya kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China (Tanzania - China Friendship Textile CO LTD). Kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa China na Tanzania na kina historia ndefu na uhusiano wa muda mrefu.

Awali, kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya kampuni iliyokuwa inamiliki kiwanda hicho na wafanyakazi, jambo lililokuwa limewafikisha katika hatua mbalimbali za usuluhishi hadi kiwanda hicho kilipopigwa mnada ili kuweza kuokoa mali za Kampuni.

Hayo yalibainishwa wakati Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC), Hamad Abdallah, alipofanya ziara kutembelea miradi inayotekelezwa na NHC mkoani Dar es Salaam, kukagua na kuona maendeleo. 

Hamad amefanya ziara katika miradi ya Samia Housing, Morocco Square, Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na  eneo la Urafiki  Dar es Salaam.

Alhamisi, 16 Mei 2024

Nape: 2024/2025 tutatekeleza haya

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imebainisha malengo 28 itakayotekeleza katika mwaka wa fedha 2024/25 ikiwamo kujenga Kituo cha kuhifadhi Data Dodoma na Zanzibar, pamoja na kuanzisha kituo kimoja cha Usalama wa Mawasiliano cha Taifa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye akiwasilisha bungeni, makadirio ya bajeti, mapato na matumizi ya wizara yake lo Mei16, 2024.

Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye, amebainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25, bungeni mjini Dodoma leo Mei 16, 2024.

"Serikali pia imepanga kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vyombo vya ulinzi na usalama kama Mahakama, TAKUKURU, Polisi, Magereza, JWTZ, Usalama wa Taifa), pamoja na taasisi 100 za Haki Jinai na Taasisi nyingine za Serikali," amesema Waziri Nape.            

Ametaja mambo mengine yatakayotekelezwa kuwa ni ukamilishaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya Simu 616 ili kufikia minara 758 katika kata 713, pamoja na kuanza ujenzi wa minara mingine mipya 636 ili kuhakikisha maeneo yaliyobaki yanapata mawasiliano.

Waziri Nape amesema, wizara hiyo imepanga kuiongezea nguvu minara 135 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 2G/3G na/au 4G, kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo 70 ya kimkakati mathalan maeneo ya hifadhi na mipakani, kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Wilaya 40 nchini, na katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.

Ametaja mipango mingine kuwa ni  kuendelea kuimarisha mifumo ya kusimamia na kupima ubora wa huduma za mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na usimamizi wa sekta, kuwezesha Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kuunganishwa na mifumo mingine ya kutolea huduma za kijamii.

"Serikali inapanga kufanya ununuzi wa magari mawili maalum ya kurushia matangazo mbashara (OB Van) na magari 15 kwa ajili ya shughuli za utangazaji katika vituo vipya vya kurushia matangazo ikiwemo kuwezesha kutangaza shughuli za Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa," amesema Nape.

Amesema Serikali pia itaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari, kuratibu uanzishaji wa Wakala wa Anga za Juu Tanzania, kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Anga za Juu na kutengeneza na kutumia mfumo wa kukusanya na kusambaza mizigo.

Nape amesema pia Serikali kupitia wizara hiyo, inakusudia kusimamia uundaji wa mfumo wa kidijitali utakaowezesha biashara Mtandao (e-Commerce), kutekeleza mradi wa kujenga kituo cha kikanda kitakachojumuisha maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao.


Mwisho

Waziri Nape, Mhandisi Maryprisca walivyopongezwa bungeni

 Picha mbalimbali zikionyesha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (Mb) na Naibu Waziri wake, Mhandisi Maryprisca Mahundi wakipongezwa baada ya kupitishwa kwa Bajeti, Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma leo, Mei 16, 2024.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa(kulia), akimpongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (Mb), baada ya wabunge kupitisha Bajeti na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo, Mei 16, 2024 bungeni Dodoma. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akimpongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kushoto), baada ya wabunge kupitisha Bajeti na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo, Mei 16, 2024 bungeni Dodoma

Pichani juu na chini;
Mawaziri na wabunge mbalimbali wakimpongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (Mb) na Naibu Waziri wa Wizara, Mhandisi Maryprisca Mahundi baada ya kupitishwa kwa Bajeti na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma, leo Mei 16, 2024.


Wizara ya Habari kukusanya Sh. bilioni 100

Waziri Nape aomba Sh. bilioni 180 za matumizi

Mwandishi Wetu, 

Wazara ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inatarajia kukusanya zaidi Sh. Bilioni 100.7 (100,700,000,000) kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya wizara hiyo ikiwemo mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku ikiliomba Bunge, kuidhinisha kiasi cha Sh. bilioni 180.9 kwa ajili ya matumizi ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mnauye akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni mjini Dodoma leo, Mei 16,2024

Wazara ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameeleza hayo leo Mei 16, 2024 bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.  

Kwa mujibu wa Waziri Nape, makusanyo mengine ya wizara hiyo kwa ujao wa fedha yatatokana na ada ya usajili wa Magazeti, ada ya mwaka ya magazeti, vitambulisho vya waandishi wa habari na machapisho ya picha, mabango na majarida.  

Amesema, mbali na makusanyo hayo, wizara hiyo imeandaa Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2024/25 kwa kuzingatia, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.  

Waziri huyo amesema pia kwamba bajeti ya wizara yake imezingatia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26), na hotuba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu fedha alizoomba kwa ajili ya matumizi ya wizara yake, Waziri Nape amesema, kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh. bilioni 88.9 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, huku Sh. bilioni 142,zikiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba, katika fedha hizo, Sh. bilioni 117.1, ni fedha za ndani na Sh. bilioni 24.8, ni fedha za nje.

Iran yakumbuka mateso ya uzayuni, yalaani

-Ni Siku ya Nakbat, yalaani ubeberu

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

KITUO cha Utamaduni cha Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Mei 16,2024 kinaadhimisha miaka 76 kukumbuka siku ya Nakbat, tangu kuanzishwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi na uvamizi kwenye ulimwengu wa Kiislamu.

Picha ikionyesha Wapalestina wakihangaika kutafuta makazi, baada ya kuanzishwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi na uvamizi wa Kizayuni enzi hizo. Picha kwa hisani ya Ubalozi wa Iran 

Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo, Mtaalamu wa Utamaduni wa Kituo hicho, Maulid Sengi amesema awali wakati wa mzozo, Wazayuni walishambulia kwa ukatili miji na vijiji vya Wapalestina na kuua maelfu ya raia wa Kiislamu na Kikristo.

“Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa tamko kwa ajili ya kuadhimisha tukio hilo *Siku ya Nakba 1403* lililosema; "Siku ya Nakba inaadhimisha kumbukumbu ya kuanzishwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi na uvamizi wa Kizayuni katikati ya ulimwengu wa Kiislamu. Siku hiyo iliratibiwa na ukoloni wa Uingereza, ikiashira iku hii inaashiria mwanzo wa kipindi cha umwagaji damu, mauaji ya kimbari, uhamishaji, uvamizi, na udhalilishaji wa ardhi takatifu ya Palestina, ikiungwa mkono moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja na nguvu za kikoloni, hasa Marekani."amesema Sengi.

Amefafanua kuwa asilimia 80 ya ardhi ya Palestina ilivamiwa na Wazyuni hao, ambapo baadhi ya wananchi wan chi hiyo walilazimika kukimbilia Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na nchi jirani ikiwamo Syria, Jordan na Lebanon. 

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei 

“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani utawala wa Kizayuni kwa kuua zaidi ya watu 35,000 wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, kujeruhi watu 75,000, na kuwahamisha mamia ya maelfu katika miezi saba iliyopita kwa msaada kamili wa kisiasa, kijeshi, kijasusi  na kiuchumi kutoka Marekani,” amesema Sangi kwa niaba ya Serikali ya Iran.

Amesema Utawala wa Kizayuni, unaoonekana kama mfano wa ugaidi uliopangwa rasmi, unaendelea kuongeza rekodi yake ya uhalifu wa kimataifa. Kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki katika hospitali za Nasser na Shifa katika Ukanda wa Gaza kunaonyesha ukubwa wa uhalifu wa utawala huu dhidi ya ubinadamu. 

Sangi amesema vitendo hivyo, ambavyo ni pamoja na uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu, vinakiuka maadili ya msingi ya Umoja wa Mataifa, viwango na kanuni zote zinazotambulika kimataifa na kuunda uwajibikaji wa jinai kwa wahusika, unaoonyesha kuendelea kwa ukwepaji wa adhabu kwa wahalifu wa Kizayuni kama ukiukaji wa sheria za kimataifa.

“ Iran inalaani vikali hatua za Marekani za kuvuruga juhudi za kusimamisha vurugu katika Gaza na upinzani wake wa kutambua taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa, ikiziita hatua hizo kuwa hazikubaliki na zisizo na uwajibikaji,”amesisitiza Sangi.

Wizara ya Mambo ya Nje  ya Iran, pia ilisisitiza kuwa Mei 21, 1403, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililothibitisha kuwa taifa la Palestina linakidhi vigezo vya kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa chini ya Kifungu cha nne cha mkataba wake.

Ikihitimisha Sengi pichani chini amesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza msimamowa thabiti wa taifa hilo kuhusu suala la Palestina na utawala wa Kizayuni wa uongo na haramu na kuunga mkono harakati za ukombozi za watu wa Palestina.

Mtaalamu wa Utamaduni wa Kituo cha Utamaduni wa Iran nchini,Maulid Sangi

Sangi amesema Iran inathibitisha tena mshikamano wake na sababu ya taifa la Palestina, ikisisitiza kuwa Palestina ni suala kuu kwa ulimwengu wa Kiislamu. 

Iran pia inaunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, ikizingatia kuwa ni hatua muhimu katika kushughulikia udhalimu wa kihistoria uliofanyiwa watu wa Palestina kwa uvumilivu na imani.

Jumatano, 15 Mei 2024

Hatifungani Kijani Tanga UWASA zasajiliwa DSE

-Waziri azielekeza taasisi nyingine kutumia utaratibu huo

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Hatifungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji Tanga inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), imesajiliwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE).

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Kushoto),akiteta jambo na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati wa hafla ya kusajiliwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE),kwa Hatifungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji Tanga inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), leo Mei 15,2024.

Zoezi hilo limefanyika katika hafla maalumu iliyofanyika jijini Dodoma katika Ofisi za Hazina, baada ya mauzo ya Hatifungani hiyo kufanya vizuri kwa asilimia 103 ikiwa ni zaidi ya lengo kusudiwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyezungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amezielekeza taasisi nyingine za Serikali kutumia utaratibu huo katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

"Tunatambua michango ya wadau wote walioshiriki katika mchakato huu. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, nazielekeza taasisi nyingine za Serikali kutumia utaratibu huu katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Tanga UWASA kwa ubunifu huo wa kutafuta chanzo mbadala cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Sote tukubaliane kuwa kupitia Tanga UWASA na kupitia Wizara ya Maji, Serikali imeandika historia mpya kwa kufanya jambo kubwa kama hili. Tumeona mwitiko wa wawekezaji, tumepata makusanyo ya Shilingi bilioni 54.72 kati ya hayo wawekezaji wa ndani ni asilimia 65 na wa nje ni asilimia 35.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly aliahidi kusimamia vyema utekelezaji wa miradi lengwa na kuhakikisha kuwa malipo ya faida kwa wawekezaji yanafanyika kwa wakati, huku akiwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha uuzaji wa Hatifungani hiyo na kwa wawekezaji wote walioshiriki ununuzi wa hisa hizo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameipongeza Tanga UWASA kwa uthubutu huo uliofungua njia na kuwashukuru wadau wote na wawekezaji waliofanikisha jambo hilo huku akisisitiza malipo kwa wawekezaji kufanyika kwa wakati.

“Leo nina furaha sana kwa sababu tunaandika historia mpya katika sekta ya maji nchini. Hii ni heshima kubwa kwa Wizara ya Maji na Menejimenti ya Tanga UWASA na hasa kwa kuyaishi maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo,” amesema Aweso.


Jumanne, 14 Mei 2024

CRDB yatajwa orodha benki bora duniani 2024

 -Yatajwa pekee kwa Tanzania

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

CRDB imetajwa kuwa benki bora zaidi nchini, iking'ara Afrika Mashariki na kutajwa miongoni mwa benki bora barani Afrika mwaka 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela

Kwa mujibu wa Mtandao wa Kimataifa Global News, Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), zimeitaja CRDB pia kuwa miongoni mwa benki bora duniani kwa mwaka huu 2024 ukanda wa Afrika.

Kwa mujibu wa mtandao huo uliochapisha habari hizo mapema mwezi huu Mei,2024, kulichoipaisha CRDB kuingia kwenye benki ubora ni uwekezaji wake endelevu wa dola milioni 300 (Tsh 780, bilioni) katika eneo uhifadhi mazingira, kupitia mpango wake wa Kijani Bond.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, nchini Uganda Centenary Bank imetajwa kuwa mshindi wa ubora, wakati ambapo imeadhimisha mika 40 mwaka uliopita 2023 ikiwa na wateja milioni 2.4 huku ikikua kwa kasi.

Kwa mwaka huu, mshindi kutoka nchini Kenya ni Co-operative Bank, inayotajwa kuwa na ongezeko kubwa la mawakala, mtandao wake ukifikia mawakala 17,000 na  kutajwa kuwa na asilimia 91 ya miamala kupitia mfumo wa kidijitali.

Benki hizo tatu za Afrika Mashariki, CRDB, Centenary na Cooperative, zimo miongoni mwa benki 35 bora zilizoainishwa kwa Bara la Afrika na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.

Jumatatu, 6 Mei 2024

Brela, Z’bar zafaidi

 -Faida nne sheria kuzikutanisha, mafanikio lukuki Miliki Bunifu, 
-Ni matunda ya miaka 60 ya Muungano

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wakati taifa likiadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka huu 2024, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umeitaja Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda Sura ya 46, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kuwa ndiyo iliyoleta muungano wa kiutendaji baina yake na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Zanzibar na sasa wote wanafaidi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa.

Nchi hizo huru, ziliungana Aprili 26.1964 ambapo Mwalimu Julius Nyerere akawa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume, akawa Makamu wa Rais.

 Akizungumzia miaka 60 ya muungano, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema kuundwa kwa sheria hiyo kumewezesha pande mbili za muungano kufanya kazi pamoja ambapo sasa inasimamiwa na kutekelezwa kwa pamoja na BRELA kwa pamoja na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.

Nyaisa amesema uanzishwaji wa sheria hiyo ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda, awali ulilenga kusimamia viwanda vya upande wa Tanzania Bara pekee, lakini mwaka 1982, ilifanywa kuwa ya Muungano, baada ya kufanyika kwa marekebisho kwenye Katiba na kuongezwa Leseni za Viwanda na Takwimu kwenye orodha ya mambo ya muungano.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo wa BRELA, marekebisho ya sheria hiyo, yameleta mafanikio manne makubwa katika miaka sitini ya muungano kwa kufanikisha utekelezaji wa usajili na utoaji wa leseni za viwanda nchini.

Mafanikio hayo ni pamoja na  kutungwa kwa Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda ambayo imeendelea kufanyiwa marekebisho kwa  kuifanya ya kisasa zaidi inayozingatia na kuendana na hali halisi ya ufanyaji biashara ya sasa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, anaeleza kuwa mabadiliko yaliyotokea ni pamoja na kuhamisha idhini ya utoaji wa leseni za viwanda kutoka kwa Bodi ya Leseni za Viwanda kwenda kwa Msajili wa Viwanda, kufuta Kamati za Ushauri za Mikoa na jukumu lake la kushauri kuhusu viwanda kuhamishiwa kwa Bodi ya Leseni za Viwanda.

Nyaisa anaeleza kuwa jingine ni kuongezwa kwa kifungu kinachoeleza kuhusu uteuzi, idadi na taratibu za uendeshaji wa Bodi ya Leseni za Viwanda na kuboresha maana ya maneno mbalimbali yanayotumika kwenye Sheria hiyo kama vile maana ya Kiwanda.

“Kujengwa kwa mfumo wa pamoja wa kielektroniki utakaotumika kutolea Leseni za Viwanda na Vyeti vya Usajili kwa pande zote mbili za Muungano ili kusaidia utekelezaji wa Sheria hiyo na kurahisisha upatikanaji wa takwimu za viwanda za nchi nzima ni sehemu ya mabadiliko hayo,” anasema Nyaisa na kufafanua;

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, wakifuatilia mkutano ulioandaliwa na BRELA kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala hiyo. Picha na Mtandao

“Mabadiliko mengine ni kufanyika kwa vikao vya pamoja vya ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano vilivyojadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Sheria hii hasa mfumo ya kielektroniki, ambavyo vilivyotoa ufumbuzi wa pamoja wa changamoto nyingi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.”

Kwa mujibu wa BRELA, kufanyika marekebisho ya jedwali la ada kwa kubadilisha malipo ya ada za leseni na usajili wa viwanda kutoka katika Dola za Kimarekani na kuwa katika shilingi za kitanzania, hivyo kupanua wigo wa urasimishaji wa viwanda, hasa vidogo.

Uratibu miliki bunifu

Katika umri huo wa miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, BRELA kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) zimekuwa na mafanikio makubwa kwenye eneo la Miliki Ubunifu.  

Kupitia BRELA na BPRA ambazo zinasimamia Miliki Ubunifu Tanzania Bara na Zanzibar, mafanikio lukuki yamepatikana yakigawanyika katika ngazi tatu; kitaifa, kikanda na kimataifa ndani ya miaka 60 ya Muungano.

Khamis Juma Khamis

Mkurugenzi Mtendaji BPRA Khamis Juma Khamis

Mafanikio Kitaifa

     Kwa mujibu wa BRELA, ushirikiano mzuri na wa karibu katika ubadilishanaji wa taarifa, kushirikishana ujuzi na uzoefu baina yake na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) umeziwezesha taasisi hizo kupiga hatua kubwa kwenye utendaji kazi wake, lengo likiwa kutoa huduma kwa uharaka, ubora, weledi na ufanisi.

    ii.        Ushirikiano huo umezifanya BRELA na BPRA kuwa na mifumo inayofanana katika uchakataji na ushughulikiaji wa maombi ya Alama za Biashara na huduma pamoja na Hataza.

BRELA inaeleza kuwa mifumo hiyo ya kielektroniki inajulikana kama, Mfumo wa Usajili kwa Njia ya Mtandao (Online Registration System - ORS) pamoja na mfumo wa kuchakata na kuhifadhi maombi ya Miliki Ubunifu (Intellectual Property Automated System (IPAS)).

Mafanikio Kikanda

BRELA inaeleza kuwa mwaka 1976, Tanzania ilijiunga na Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (African Regional Intellectual Property Organization-ARIPO), ambapo kupitia ARIPO taifa limesaini na kuridhia Itifaki katika Usimamizi wa Maeneo Mahsusi ya Miliki Ubunifu.

Itifaki zilizoridhiwa na manufaa yaliyopatikana ni pamoja na Tanzania kusaini na kuridhia Itifaki ya Harare ya Ulinzi wa Hataza na Maumbo Bunifu (Harare Protocol on Protection of Patents and Designs)mwaka 1982, hatua iliyowezesha wabunifu kulinda bunifu zao ikiwa ni Hataza na Maumbo Ubunifu hivyo kuongeza wigo wa ulinzi wa bunifu husika.

Pili, Tanzania kusaini Itifaki ya Banjul ya Ulinzi wa Alama mwaka 1993,(Banjul Protocol on the Protection of Marks 1993), ambayo inatoa fursa kwa Wabunifu wa Alama (nembo) kusajili na kupata ulinzi wa Alama za Biashara na Huduma kwa kupitia ARIPO, hivyo kuongeza wigo wa ulinzi kwa wabunifu husika.

Tatu, Mwaka 2015 Tanzania ilisaini Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Mbegu Mpya za Mimea, itifaki ambayo inatoa fursa kuongeza wigo wa ulinzi kwa wagunduzi wa aina mpya za Mmbegu za mimea.

Vilevile, mwaka 2021 Tanzania ilisaini Itifaki ya Kampala ya Usajili wa Hiyari wa Hakimiliki na Hakishiriki inayotoa fursa kuongeza wigo wa ulinzi wa wabunifu wa kazi za sanaa na uandishi.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2023 Tanzania ilisaini Itifaki ya Ulinzi wa Haki za Miliki Ubunifu chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (Protocol on Protection of Intellectual Property Rights under the African Continental Free Trade Area - AfCFTA).

Kwa kuwa mwanachama wa Shirika hili, Tanzania imenufaika katika mambo mbalimbali ikiwamo kujengewa uwezo na kuongeza ujuzi na utaalam katika eneo la Miliki Ubunifu na kujifunza kutoka Nchi nyingine Wanachama, pia kutoa elimu kwa kuanzisha Shahada ya Umahiri katika Miliki Ubunifu inayotolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadhi ya Wajasiriamali walionufaika na huduma za BRELA, wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wakala hao.

 Kwa upande wa Kimataifa          

Mwaka 1983, Tanzania ilijiunga na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (World Intellectual Property Organization – WIPO), ambapo kupitia Mkataba wa Stockholm, uanachama wa Tanzania WIPO, imeliwezesha taifa kujiunga na mikataba inayohusiana na usimamizi na uratibu wa masuala mbalimbali yanayohusu Miliki Ubunifu.

Mikataba iliyojiunga nayo ni pamoja na ule wa Paris wa Ulinzi wa Mali Ubunifu (Paris Convention for Protection of   Industrial Property of 1883), Mkataba wa Berne wa ulinzi wa  Kazi za Uandishi na Sanaa (The Berne Convention for the Protection of Literary and Artistic Works of 1886), Mkataba wa Nice wa Madaraja ya Alama za Biashara na Huduma (Nice Agreement concerning the International Classification of Goods and Services of 1957) na  Mkataba wa Ushirikiano wa Hataza (The Patents Cooperation Treaty (PCT) of 1970).

Tanzania imejiunga pia na Mkataba wa masuala ya ulinzi wa hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea unaojulikana kwa jina la Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (International Convention for the Protection of New Varieties of Plants chini ya International Union for the Protection of New Varieties of Plants).

Mbali na mikataba hiyo, Tanzania pia mwanachama na Shirika la Biashara Dunia (WTO) ambapo kupitia uanachama huo inatakiwa kutekeleza Mkataba wa Masuala ya Miliki Ubunifu yanayohusiana na Biashara wa mwaka 1994 (Trade-Related Aspects of Intellectual Property Agreement (TRIPS) of 1994 of the World Trade Organization).

BRELA inaeleza kuwa mkataba huo unatoa nafuu na fursa katika eneo la Miliki Ubunifu, ambazo ni pamoja na uwezekano wa kutumia teknolojia za dawa na vifaa tiba ambazo zinapatikana katika Hataza (Patent), unawezesha pia upatikanaji rahisi wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu au kutumia teknolojia hizo pasipo kupata matatizo ya Kkisheria kutoka kwa wamiliki wa teknolojia husika. 

Kwa mujibu wa BRELA kupitia mikataba  hiyo ya kikanda na kimataifa ya uratibu na usimamizi wa Miliki Ubunifu, Tanzania imenufaika kwa kuongeza ujuzi kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu, uhawilishaji wa teknolojia, kubadilishana ujuzi katika masuala ya Miliki Ubunifu na kuwezesha  kuongeza wataalam wa Miliki Ubunifu.

Pia imenufaika kwa kukuza uelewa wa matumizi ya Miliki Ubunifu kwa maendeleo endelevu na kuboresha mifumo ya usimamizi na uratibu wa Miliki Ubunifu kwa pande zote mbili za Muungano.

Ijumaa, 3 Mei 2024

Waziri mstaafu afariki dunia

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Fedha wa zamani Mustafa Mkulo(77), amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.
Marehemu Mustafa Mkulo, enzi za uhai wake, akijibu maswali bungeni. Picha kwa hisani ya Mtandao.
Taarifa za kifo cha Mkulo aliyeshika wadhifa huo kati ya mwaka 2007 hadi 2012, zinamnukuu mke wa marehemu, Julie akitangaza kuwa kimetokea Mei 3.

Kwa mujibu wa tangazo la familia ya Mkulo shughuli za mazishi zitafanyika nyumbani kwake Mikocheni leo Mei 4,2024.

Kwa mujibu familia hiyo mazishi ya Mkulo aliyewahi pia kuwa Mbunge wa Kilosa mwaka 2005 hadi 2015, zitafanyika kesho Jumapili Mei 5, 2024, Kilosa Morogoro.

Marehemu Mkulo pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miaka ya 1990 hadi alipokwenda kugombea ubunge mwaka 2005.



 *Inna lillahi wa inna ilayhi rajioon*

'Elimisheni jamii mabadiliko tabianchi'

Hellen Ngoromera, Dodoma

Wakati leo dunia ikisherehekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka waandishi wa habari nchini kuielimisha  jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Majaliwa amesema hayo leo Mei 3, 2024 mjini hapa, alipokuwa akifunga kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

"Elimisheni jamii na kuielezea kuhusu mabadiliko ya tabiachi, hivi karibuni tumepata mvua nyingi ambazo zilisababisha madhara kwa wananchi hivyo, ninyi kama waelimisha jamii mna wajibu wa kuwakumbusha kujua wajibu wao kuhusu mabadiliko ya tabianchi," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema ikiwa waandishi  wa habari  wataandika habari hizo kwa kueleza kwa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi itawasaidia  wana jamii kufahamu vizuri hivyo kuepuka athari zake mbalimbali.

Majaliwa amewataka pia wana habari kuitangaza nchi na kuijengea taswira chanya kimataifa. 

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu inayosema Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ambapo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Tanzania.