-Waziri azielekeza taasisi nyingine kutumia utaratibu huo
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Hatifungani ya Kijani ya Miundombinu ya Maji Tanga inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA), imesajiliwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE).
Zoezi hilo limefanyika katika hafla maalumu iliyofanyika jijini Dodoma katika Ofisi za Hazina, baada ya mauzo ya Hatifungani hiyo kufanya vizuri kwa asilimia 103 ikiwa ni zaidi ya lengo kusudiwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyezungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amezielekeza taasisi nyingine za Serikali kutumia utaratibu huo katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
"Tunatambua michango ya wadau wote walioshiriki katika mchakato huu. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, nazielekeza taasisi nyingine za Serikali kutumia utaratibu huu katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo,” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Tanga UWASA kwa ubunifu huo wa kutafuta chanzo mbadala cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Sote tukubaliane kuwa kupitia Tanga UWASA na kupitia Wizara ya Maji, Serikali imeandika historia mpya kwa kufanya jambo kubwa kama hili. Tumeona mwitiko wa wawekezaji, tumepata makusanyo ya Shilingi bilioni 54.72 kati ya hayo wawekezaji wa ndani ni asilimia 65 na wa nje ni asilimia 35.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly aliahidi kusimamia vyema utekelezaji wa miradi lengwa na kuhakikisha kuwa malipo ya faida kwa wawekezaji yanafanyika kwa wakati, huku akiwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha uuzaji wa Hatifungani hiyo na kwa wawekezaji wote walioshiriki ununuzi wa hisa hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameipongeza Tanga UWASA kwa uthubutu huo uliofungua njia na kuwashukuru wadau wote na wawekezaji waliofanikisha jambo hilo huku akisisitiza malipo kwa wawekezaji kufanyika kwa wakati.
“Leo nina furaha sana kwa sababu tunaandika historia mpya katika sekta ya maji nchini. Hii ni heshima kubwa kwa Wizara ya Maji na Menejimenti ya Tanga UWASA na hasa kwa kuyaishi maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo,” amesema Aweso.
0 Maoni