Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Brela, Z’bar zafaidi

 -Faida nne sheria kuzikutanisha, mafanikio lukuki Miliki Bunifu, 
-Ni matunda ya miaka 60 ya Muungano

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wakati taifa likiadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka huu 2024, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umeitaja Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda Sura ya 46, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kuwa ndiyo iliyoleta muungano wa kiutendaji baina yake na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Zanzibar na sasa wote wanafaidi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa.

Nchi hizo huru, ziliungana Aprili 26.1964 ambapo Mwalimu Julius Nyerere akawa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume, akawa Makamu wa Rais.

 Akizungumzia miaka 60 ya muungano, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema kuundwa kwa sheria hiyo kumewezesha pande mbili za muungano kufanya kazi pamoja ambapo sasa inasimamiwa na kutekelezwa kwa pamoja na BRELA kwa pamoja na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.

Nyaisa amesema uanzishwaji wa sheria hiyo ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda, awali ulilenga kusimamia viwanda vya upande wa Tanzania Bara pekee, lakini mwaka 1982, ilifanywa kuwa ya Muungano, baada ya kufanyika kwa marekebisho kwenye Katiba na kuongezwa Leseni za Viwanda na Takwimu kwenye orodha ya mambo ya muungano.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo wa BRELA, marekebisho ya sheria hiyo, yameleta mafanikio manne makubwa katika miaka sitini ya muungano kwa kufanikisha utekelezaji wa usajili na utoaji wa leseni za viwanda nchini.

Mafanikio hayo ni pamoja na  kutungwa kwa Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji wa Leseni za Viwanda ambayo imeendelea kufanyiwa marekebisho kwa  kuifanya ya kisasa zaidi inayozingatia na kuendana na hali halisi ya ufanyaji biashara ya sasa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, anaeleza kuwa mabadiliko yaliyotokea ni pamoja na kuhamisha idhini ya utoaji wa leseni za viwanda kutoka kwa Bodi ya Leseni za Viwanda kwenda kwa Msajili wa Viwanda, kufuta Kamati za Ushauri za Mikoa na jukumu lake la kushauri kuhusu viwanda kuhamishiwa kwa Bodi ya Leseni za Viwanda.

Nyaisa anaeleza kuwa jingine ni kuongezwa kwa kifungu kinachoeleza kuhusu uteuzi, idadi na taratibu za uendeshaji wa Bodi ya Leseni za Viwanda na kuboresha maana ya maneno mbalimbali yanayotumika kwenye Sheria hiyo kama vile maana ya Kiwanda.

“Kujengwa kwa mfumo wa pamoja wa kielektroniki utakaotumika kutolea Leseni za Viwanda na Vyeti vya Usajili kwa pande zote mbili za Muungano ili kusaidia utekelezaji wa Sheria hiyo na kurahisisha upatikanaji wa takwimu za viwanda za nchi nzima ni sehemu ya mabadiliko hayo,” anasema Nyaisa na kufafanua;

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, wakifuatilia mkutano ulioandaliwa na BRELA kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala hiyo. Picha na Mtandao

“Mabadiliko mengine ni kufanyika kwa vikao vya pamoja vya ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano vilivyojadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa Sheria hii hasa mfumo ya kielektroniki, ambavyo vilivyotoa ufumbuzi wa pamoja wa changamoto nyingi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.”

Kwa mujibu wa BRELA, kufanyika marekebisho ya jedwali la ada kwa kubadilisha malipo ya ada za leseni na usajili wa viwanda kutoka katika Dola za Kimarekani na kuwa katika shilingi za kitanzania, hivyo kupanua wigo wa urasimishaji wa viwanda, hasa vidogo.

Uratibu miliki bunifu

Katika umri huo wa miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, BRELA kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) zimekuwa na mafanikio makubwa kwenye eneo la Miliki Ubunifu.  

Kupitia BRELA na BPRA ambazo zinasimamia Miliki Ubunifu Tanzania Bara na Zanzibar, mafanikio lukuki yamepatikana yakigawanyika katika ngazi tatu; kitaifa, kikanda na kimataifa ndani ya miaka 60 ya Muungano.

Khamis Juma Khamis

Mkurugenzi Mtendaji BPRA Khamis Juma Khamis

Mafanikio Kitaifa

     Kwa mujibu wa BRELA, ushirikiano mzuri na wa karibu katika ubadilishanaji wa taarifa, kushirikishana ujuzi na uzoefu baina yake na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) umeziwezesha taasisi hizo kupiga hatua kubwa kwenye utendaji kazi wake, lengo likiwa kutoa huduma kwa uharaka, ubora, weledi na ufanisi.

    ii.        Ushirikiano huo umezifanya BRELA na BPRA kuwa na mifumo inayofanana katika uchakataji na ushughulikiaji wa maombi ya Alama za Biashara na huduma pamoja na Hataza.

BRELA inaeleza kuwa mifumo hiyo ya kielektroniki inajulikana kama, Mfumo wa Usajili kwa Njia ya Mtandao (Online Registration System - ORS) pamoja na mfumo wa kuchakata na kuhifadhi maombi ya Miliki Ubunifu (Intellectual Property Automated System (IPAS)).

Mafanikio Kikanda

BRELA inaeleza kuwa mwaka 1976, Tanzania ilijiunga na Shirika la Miliki Ubunifu la Kanda ya Afrika (African Regional Intellectual Property Organization-ARIPO), ambapo kupitia ARIPO taifa limesaini na kuridhia Itifaki katika Usimamizi wa Maeneo Mahsusi ya Miliki Ubunifu.

Itifaki zilizoridhiwa na manufaa yaliyopatikana ni pamoja na Tanzania kusaini na kuridhia Itifaki ya Harare ya Ulinzi wa Hataza na Maumbo Bunifu (Harare Protocol on Protection of Patents and Designs)mwaka 1982, hatua iliyowezesha wabunifu kulinda bunifu zao ikiwa ni Hataza na Maumbo Ubunifu hivyo kuongeza wigo wa ulinzi wa bunifu husika.

Pili, Tanzania kusaini Itifaki ya Banjul ya Ulinzi wa Alama mwaka 1993,(Banjul Protocol on the Protection of Marks 1993), ambayo inatoa fursa kwa Wabunifu wa Alama (nembo) kusajili na kupata ulinzi wa Alama za Biashara na Huduma kwa kupitia ARIPO, hivyo kuongeza wigo wa ulinzi kwa wabunifu husika.

Tatu, Mwaka 2015 Tanzania ilisaini Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Mbegu Mpya za Mimea, itifaki ambayo inatoa fursa kuongeza wigo wa ulinzi kwa wagunduzi wa aina mpya za Mmbegu za mimea.

Vilevile, mwaka 2021 Tanzania ilisaini Itifaki ya Kampala ya Usajili wa Hiyari wa Hakimiliki na Hakishiriki inayotoa fursa kuongeza wigo wa ulinzi wa wabunifu wa kazi za sanaa na uandishi.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2023 Tanzania ilisaini Itifaki ya Ulinzi wa Haki za Miliki Ubunifu chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (Protocol on Protection of Intellectual Property Rights under the African Continental Free Trade Area - AfCFTA).

Kwa kuwa mwanachama wa Shirika hili, Tanzania imenufaika katika mambo mbalimbali ikiwamo kujengewa uwezo na kuongeza ujuzi na utaalam katika eneo la Miliki Ubunifu na kujifunza kutoka Nchi nyingine Wanachama, pia kutoa elimu kwa kuanzisha Shahada ya Umahiri katika Miliki Ubunifu inayotolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baadhi ya Wajasiriamali walionufaika na huduma za BRELA, wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wakala hao.

 Kwa upande wa Kimataifa          

Mwaka 1983, Tanzania ilijiunga na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (World Intellectual Property Organization – WIPO), ambapo kupitia Mkataba wa Stockholm, uanachama wa Tanzania WIPO, imeliwezesha taifa kujiunga na mikataba inayohusiana na usimamizi na uratibu wa masuala mbalimbali yanayohusu Miliki Ubunifu.

Mikataba iliyojiunga nayo ni pamoja na ule wa Paris wa Ulinzi wa Mali Ubunifu (Paris Convention for Protection of   Industrial Property of 1883), Mkataba wa Berne wa ulinzi wa  Kazi za Uandishi na Sanaa (The Berne Convention for the Protection of Literary and Artistic Works of 1886), Mkataba wa Nice wa Madaraja ya Alama za Biashara na Huduma (Nice Agreement concerning the International Classification of Goods and Services of 1957) na  Mkataba wa Ushirikiano wa Hataza (The Patents Cooperation Treaty (PCT) of 1970).

Tanzania imejiunga pia na Mkataba wa masuala ya ulinzi wa hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea unaojulikana kwa jina la Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (International Convention for the Protection of New Varieties of Plants chini ya International Union for the Protection of New Varieties of Plants).

Mbali na mikataba hiyo, Tanzania pia mwanachama na Shirika la Biashara Dunia (WTO) ambapo kupitia uanachama huo inatakiwa kutekeleza Mkataba wa Masuala ya Miliki Ubunifu yanayohusiana na Biashara wa mwaka 1994 (Trade-Related Aspects of Intellectual Property Agreement (TRIPS) of 1994 of the World Trade Organization).

BRELA inaeleza kuwa mkataba huo unatoa nafuu na fursa katika eneo la Miliki Ubunifu, ambazo ni pamoja na uwezekano wa kutumia teknolojia za dawa na vifaa tiba ambazo zinapatikana katika Hataza (Patent), unawezesha pia upatikanaji rahisi wa dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu au kutumia teknolojia hizo pasipo kupata matatizo ya Kkisheria kutoka kwa wamiliki wa teknolojia husika. 

Kwa mujibu wa BRELA kupitia mikataba  hiyo ya kikanda na kimataifa ya uratibu na usimamizi wa Miliki Ubunifu, Tanzania imenufaika kwa kuongeza ujuzi kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu, uhawilishaji wa teknolojia, kubadilishana ujuzi katika masuala ya Miliki Ubunifu na kuwezesha  kuongeza wataalam wa Miliki Ubunifu.

Pia imenufaika kwa kukuza uelewa wa matumizi ya Miliki Ubunifu kwa maendeleo endelevu na kuboresha mifumo ya usimamizi na uratibu wa Miliki Ubunifu kwa pande zote mbili za Muungano.

Chapisha Maoni

0 Maoni