Hellen Ngoromera, Dodoma
Wakati leo dunia ikisherehekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka waandishi wa habari nchini kuielimisha jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Majaliwa amesema hayo leo Mei 3, 2024 mjini hapa, alipokuwa akifunga kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
"Elimisheni jamii na kuielezea kuhusu mabadiliko ya tabiachi, hivi karibuni tumepata mvua nyingi ambazo zilisababisha madhara kwa wananchi hivyo, ninyi kama waelimisha jamii mna wajibu wa kuwakumbusha kujua wajibu wao kuhusu mabadiliko ya tabianchi," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema ikiwa waandishi wa habari wataandika habari hizo kwa kueleza kwa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi itawasaidia wana jamii kufahamu vizuri hivyo kuepuka athari zake mbalimbali.
Majaliwa amewataka pia wana habari kuitangaza nchi na kuijengea taswira chanya kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu inayosema Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ambapo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Tanzania.
0 Maoni