Jumatano, 26 Februari 2025

Dk. Kongela awapongeza wafanyakazi NHC

-Mkurugenzi ataja mambo10 atakayosimamia kufikia malengo

Joddet Dominic na Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Kibaha, PwaniMwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk. Sophia Kongela, amewapongeza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa mijadala yenye tija.

Amesema ameguswa hasa na mjadala kuhusu bajeti ya shirika hilo kwa mwaka 2025/26, inayolenga kuboresha utendaji kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa nyumba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)Dk.Sophia Kongela, akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC,Kibaha Pwani,Februari 25,2025.

 
Dk. Kongela ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha Pwani, Februari 24 na 25, 2025 ambapo aliwahimiza wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu, waaminifu, na kujituma katika majukumu yao, akisisitiza kuwa mshikamano na maadili bora ndio nguzo ya mafanikio ya shirika.

Katika hotuba yake Dk. Kongela alieleza kuwa NHC imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa akitaja awamu ya kwanza ya Mradi wa Samia Housing Scheme, inahusisha ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe, Dar es Salaam, pamoja na majengo ya ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba. 

"Mafanikio haya yamewezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hasa katika kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa miradi ya kimkakati ya ujenzi,"amesema Dk. Kongela.

Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiimba wimbo wa Mshikamano Daima kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo uliofanyika kwa siku mbili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha Pwani.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa rasilimali za shirika,akitoa wito kwa wafanyakazi kuhakikisha ukusanyaji wa madeni ya kodi ya pango unaimarishwa ili kuongeza mapato ya Shirika.

Dk.Kongela pia amehimiza kila mfanyakazi wa NHC kufanya kazi kwa uwazi, bidii na mshikamano, akiunga mkono kauli ya Msajili wa Hazina,Nehemia Mchechu katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo na sisitiza kuwa majungu na makundi hayana nafasi ndani ya NHC  linalojizatiti kufanikisha malengo yake.

Mkutano huo umejadili masuala mbalimbali muhimu ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya NHC, ambapo wajumbe wametakiwa kuhakikisha kuwa shirika hilo linaendelea kutoa gawio kwa Serikali, ambalo kwa mwaka huu linakadiriwa kufikia shilingi bilioni 6.5.

Awali,akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Hamad Abdallah amesema kuwa dhamira yake ni kuongoza NHC kwa weledi, uadilifu na bidii ili kuhakikisha ongezeko la ufanisi na tija katika utoaji wa huduma bora za makazi nchini akitaja mambo kumi atakayosimamia utekelezaji wake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa  shirika hilo,Kibaha Pwani Februari,2025

"Kwa msingi huo, NHC itaendelea kutekeleza yafuatayo; Kuongeza ufanisi, kuboresha mifumo ya usimamizi wa miradi, rasilimali watu na huduma kwa wateja, ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama zisizo za lazima,"

Amteaja mengine kuwa ni kufanya kazi kwa weledi,kuhakikisha kuwa kila hatua inazingatia viwango vya kitaalamu na ubora wa hali ya juu,kujenga uadilifu na uwajibikaji,  kusimamia rasilimali kwa umakini na kuongeza uwazi na uwajibikaji wa wafanyakazi kwa maslahi ya umma.

Mkurugenzi huyo pia ametaja kuhamasisha ubunifu na ushirikiano,kushirikiana na wadau wa sekta ya ujenzi, taasisi za kifedha, na wawekezaji ili kuongeza upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu, kusimamia miradi ya kimkakati, kutekeleza miradi mikubwa ya makazi na biashara katika mikoa mbalimbali ili kusaidia kupunguza uhaba wa makazi na kuchochea maendeleo ya miji.

"Kwa kushikamana na maadili ya kazi, bidii, na mshikamano, wafanyakazi wa NHC wataendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya sekta ya makazi nchini," amesema Hamad.

Jumatatu, 24 Februari 2025

Msajili Hazina ataka kasi zaidi NHC, akionya majungu

-Awaambia NO uteuzi kwa majungu

Exuperius Kachenjea na Joddet Dominic, daimatznews@gmail.com

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina jukumu kubwa katika kutekeleza mageuzi ya sekta ya makazi nchini akihimiza kuongeza ufanisi, kufanya maamuzi kwa haraka na kuhakikisha mali za umma zinatumika ipasavyo.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linalofanyika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kibaha, mkoani Pwani Februari 24,2025.

Mchechu pia amesema mafanikio ya mageuzi hayo yanahitaji mshikamano na uwajibikaji wa pamoja kwa wafanyakazi wote, huku akionya watumishi kuacha majungu badala yake kuchapakazi kwani ndiyo njia ya mafanikio.

"Ili tufanikiwe, tunahitaji kuwa na timu inayofanya kazi kwa upendo, siyo kwa majungu. Mimi mwenyewe ninaweza kuwa mmoja wa waathirika wa majungu, lakini nawaombeni sana mfanye kazi kwa upendo," amesema Mchechu.

Amesisitiza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji hautazingatia maneno ya pembeni bali ufanisi na uwezo wa mtu katika kutekeleza majukumu yake.

Ametoa wito kwa wafanyakazi wa taasisi zote za umma kushikamana na kushirikiana kwa karibu katika mchakato wa mageuzi, kwani mshikamano ndiyo msingi wa mafanikio.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, wakifuatilia mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili Kibaha, mkoani Pwani Februari 24 hadi 25, 2025.  

"Hatutateua mtu kwa sababu ni bingwa wa kupiga majungu, tutateua kwa ufanisi. Naomba tuwe na mshikamano ili kuhakikisha taasisi zetu zinapiga hatua kubwa katika maendeleo," amesisitiza.

Kuhusu miradi inayotekelezwa na NHC Mchechu ameliambia Baraza la Wafanyakazi wa NHCkwamba maeneo muhimu kama Urafiki na Morogoro tayari yametolewa kwa matumizi ya shirika, huku akitoa angalizo kuwa mali hizo hazipaswi kutumiwa vibaya.

"Hatutaruhusu mali hizi zitumike vibaya. Tunataka kuona ufanisi unaongezeka na kuhakikisha tunasimamia sekta ya makazi kwa weledi," amesema.

Kwa mujibu Msajili huyo wa Hazina, mageuzi katika taasisi za umma ni safari isiyoepukika, ikilenga kuimarisha utendaji, ufanisi na kupunguza utegemezi wa Serikali katika uendeshaji wa mashirika yake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Hamad Abdallah akizungumza katika Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linalofanyika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kibaha, mkoani Pwani Februari 24 na 25,2025.

Mchechu amebainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kuchukua hatua za msingi kuhakikisha taasisi zinazojitegemea zinafanya mageuzi yenye tija.

"Reforms is a journey – mabadiliko ni safari, ni lazima tuyafanye kwa umakini na dhamira ya kweli," amesema Mchechu, akifafanua kuwa mwaka huu Serikali imeanza kutumia mfumo wa ukaguzi wa CAG katika kutathmini vigezo vya utendaji kazi (KPI). 

Amesema kuwa taasisi 58 zinazojitegemea zimeanza kupitia mchakato huo ili kuhakikisha zinajiendesha kwa weledi na uwazi.

Katika jitihada za kuimarisha uwajibikaji, Msajili wa Hazina amesema Serikali itateua taasisi maalum kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa viashiria vya utendaji (KPI Monitoring), ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa na utegemezi unapunguzwa.

Msajili wa Hazina, NehemiaMchechu (Katikati), Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah(Kushoto) na Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC Muungano Saguya  wakishikana mikono walipoimba wimbo wa Mshikamano Daima wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linalofanyika ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kibaha, mkoani Pwani Februari 24,2025

Mchechu ameweka wazi kuwa changamoto kubwa iliyopo ni jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi, ili taasisi ziweze kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi.
 

Mkutano huo wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC unafanyika leo na kesho ukihusisha mijadala yenye lengo la kuimarisha utendaji wa shirika, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha mageuzi yanatekelezwa kwa tija na uwazi.


Ijumaa, 21 Februari 2025

Mshtakiwa dawa za kulevya adai kuitilia shaka Jamhuri

 -Ni kwa kutotajwa vielelezo vilivyochukuliwa nyumbanil kwake 

MwandishiWetu,daimatznews@gmail.com

MSHTAKIWA katika kesi ya dawa za kulevya, Sharifa Majani amesema anautilia  shaka upande wa Jamhuri, kwani haukutaja mahakamani vielelezo vilivyochukuliwa nyumbani kwake, ikiwemo hati ya nyumba, kadi za Benki na simu zake.

Shughuli za Mahakama ya Mafisadi zikiendelea katika moja ya kesi zilizowahi kusikilizwa na mahakama hiyo.  

Mshtakiwa huyo amekana kujipatia nyumba yenye thamani ya Sh milioni 168 kwa kujihusisha na  biashara ya dawa za kulevya.

Mshtakiwa huyo wa kwanza alidai hayo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati akisomewa mashtaka na maelezo ya awali.

"Mheshimiwa hapa kuna ukakasi, vielelezo vilivyochukuliwa ndani kwangu upande wa Jamhuri hawakuvisema, hati ya nyumba, simu na kadi za Benki,"alidai mshtakiwa.

Sharifa alikana kuwaelezea Polisi kwamba dawa za kulevya zingine zilisafirishwa kwa kutumia basi kwenda Himo.

 Mshtakiwa huyo wa kwanza  pia alidai upekuzi ulifanyika nyumbani kwake lakini hawakukuta dawa za kulevya katika chumba cha kulala.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifa, Chigbo Innocent , Omary Omary na Mandela Masawe, wanadaiwa kati ya Januari mwaka 2019 na Aprili 22 mwaka 2023 maeneo ya Pwani na Kilimanjaro washtakiwa waliongoza genge la Uhalifu kufanya kosa la jinai.

Mshtakiwa wa kwanza na wapili walidaiwa Aprili 20 mwaka 2023 maeneo ya Kiluvya walikutwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 25.

Shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote , ilidaiwa kati ya Aprili 2023 na Aprili 22 mwaka 2023 maeneo ya Kisarawe na Himo walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 45.86.

Shtaka la nne linamkabili mshtakiwa wa kwanza, Sharifa ilidaiwa alitakatisha fedha kati ya Januari 2019 na Aprili mwaka 2023 maeneo ya Kiluvya.

Imedaiwa mshtakiwa huyo alijipatia nyumba yenye thamani ya Sh milioni 168 huku akijua mali hiyo ni mazalia ya kosa la jinai.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na waliposomewa maelezo ya awali mshtakiwa wa kwanza alikubali anaishi Kiluvya Madukani , mshtakiwa wa pili anaishi Goba na mshtakiwa wa tatu na wanne wanaishi Himo mkoani Kilimanjaro.

Mshtakiwa wa 1,2 na 3 walikana kufahamiana lakini walikubali kwamba walifanyiwa upekuzi katika nyumba zao.

Ilidaiwa ni kweli nyumbani kwa mshtakiwa wa pili walikuta gari moja na simu tatu lakini mshtakiwa wa pili alikana kuwapeleka maafisa wa Polisi nyumbani kwa mshtakiwa namba moja Kiluvya.

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo unatarajiwa kuita mashahidi 27, vielelezo vya maandishi 24 na vielelezo halisia tisa.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mruge Karoli alidai washtakiwa katika shauri hilo watajitetea wenyewe na hawatakuwa na vielelezo. Shauri liliahirishwa hadi tarehe nyingine itakayopangwa.

Jumatano, 19 Februari 2025

Kesi ya 'Mkurugenzi' wa NIC yaelekea patamu

-Ni ya kuchepusha Sh, Bilioni 1.8 

-Mashahidi 119 kutoa ushahidi

Na Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Kesi ya kuchepusha shilingi bilioni1.8 inayoyomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Shirika la Bima la Taifa (NIC), Sam Kamanga na wenzake wawili inaelekea patamu, baada ya mahakama kuelezwa kuwa mashahidi 119 na vielelezo 200 vinatarajiwa kutolewa kuthibitisha mashtaka hayo na upande wa Jamhuri.

Mfano wa noti  za Shilingi Elfu Kumi (10,000/=) za Benki Kuu  ya Tanzania

Ushahidi huo unatarajiwa kutolewa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Karen Mrango akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edgar Bantulaki, umeeleza hayo leo Februari 18, 2025 mahakamani hapo .

Wakili Bantulaki aliwataja washtakiwa katika shauri hilo kuwa ni Kamanga, Tabu Selemani na Peter Nzunda ambao wanadaiwa kati ya Mwaka 2013 na 2018 waliongoza genge la Uhalifu maeneo tofauti tofauti Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Arusha , Mbeya, Morogoro na Kigoma.

Inadaiwa kwa nyakati tofauti kwa njia ya ulaghai walijipatia Sh 1,863,017,400.75 kutoka Shirika la Taifa la Bima.

Washtakiwa wanadaiwa walijipatia fedha hizo kwa kughushi hundi  na mshtakiwa wa nne Nzunda anadaiwa kwa kutumia fedha hizo alinunua mashamba matano maeneo tofauti tofauti.

Washtakiwa waliposomewa maelezo ya awali walikana kuhusika kuchepusha fedha hizo.

Walidai wanafahamu kulikuwa na fedha zilizochepushwa lakini hawakuhusika.

Washtakiwa walikana kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha na walikana pia kushirikiana na maafisa wa Benki kutenda kosa hilo.

 Kamanga alikana Kuzuia ukaguzi kufanyika na kwamba wizi ulifanyika ndani ya miaka minne bila kubainika na Wakuu wa idara.

Mshtakiwa Tabu alidai kwa nafasi yake ya uhasibu alifanya uchunguzi wake mwenyewe na kugundua fedha zilichepushwa na alitoa ripoti ya fedha hizo.

Tabu alidai Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alikuwa anafanya ukaguzi kila mwaka lakini hakumbuki kama uliwahi kufanyika ukaguzi maalum katika Shirika la Taifa la Bima.

Walishtakiwa walikana kujipatia fedha hizo kwa kughushi hundi  na mshtakiwa Nzunda alikana kutumia fedha hizo kununua mashamba matano maeneo tofauti tofauti na garu huku akijua ni mazalia ya Makosa ya jinai.

Jumapili, 9 Februari 2025

80% muziki wa kitanzania kusikia viwanja vya ndege Tx

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Hamis Mwinjuma na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile, wameshuhudia utiaji saini makubaliano ya matumizi ya asilimia 80 ya muziki wa wasanii wa kitanzania, kupigwa katika viwanja vya ndege nchini, ili kuwawezesha kufaidi matunda ya kazi zao yatokanayo na malipo ya mirabaha.
 
Naibu Waziri wa Sanaa,Michezo na Utamaduni,(Kulia) na  Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile, (kushoto)wakishuhudia utiaji saini mikataba itakayowezesha muziki wa Kiswahili kupigwa viwanya vya ndege.katikahfla iliyofanyika hivi karibuni


Makubaliano hayo yamesainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa na Msimamizi wa Haki Miliki (COSOTA) Doreen Sinare, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)  Abdul Mombokaleo, ambapo katika makubaliano hayo, imependekezwa muziki wa wasanii wa kitanzania kusikilizwa zaidi, lengo likiwa ni kulinda kazi za sanaa za watanzania pamoja na kuutangaza muziki huo ndani ya nchi na nje kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini kila siku.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwinjuma amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya wasanii.

“Rais alionyesha nia ya kuboresha mazingira ya wasanii kwa kutambua mchango wa sanaa katika Taifa letu na umuhimu wa kazi zao, na pia kutafuta njia za ziada za kukuza kipato chao pamoja na uchumi, leo tumefikia hatua muhimu ambapo COSOTA imefikia Makubaliano ya Ushirikiano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhusu suala la kulipia leseni (mirabaha) kwa matumizi ya muziki katika viwanja vya ndege. Makubaliano haya, ambayo ni sehemu ya Mkataba kati ya TAA na COSOTA, yatasaidia wasanii wa muziki wanapata haki yao ya malipo kutokana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini.” Amesema Mhe. Mwinjuma.

Amesema hiyo ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao, na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao, na kwamba haki zao zinaheshimiwa kikamilifu.

Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha Septemba 2023 hadi Novemba 2024, COSOTA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya zaidi ya shilingi Bil. 1.1

“Itakua vema pia nikisema kuwa katika kipindi cha Septemba 2023 hadi Novemba 2024, COSOTA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya jumla ya shilingi bil. 1.1 ambazo zitagawanywa kwa wanufaika ambao ni Wasanii, Waandishi wa muziki, filamu, sanaa za maonesho, na sanaa za ufundi.

Nae,Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema taasisi za COSOTA na TAA zimekuwa za kwanza kuingia makubaliano ya namna hiyo na kutoa wito kwa taasisi zingine za usafirishaji zilizopo kwenye wizara yake, kuiga mfano huo ili kuwanufaisha wasanii kupitia kazi zao.

“Kwa taarifa nilizonazo katika taasisi zetu zote za wizara ya uchukuzi, TAA inakuwa ya kwanza kuingia makubaliano haya, natoa wito kwa taasisi zingine hususan Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHIKO) kuwasiliana na COSOTA na kuiga mfano mzuri uliowekwa na TAA” amesema  Kihenzile

Ommy Dimpoz azindua Tuzo za Komedi Tanzania, kutolewa Februari 14

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Msanii Maarufu wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz, amezindua Tuzo za Komedi Tanzania (TCA), zinazojulikana kama 'Tanzania Comedy Awards', zinazotarajiwa kutolewa Februari 14, mwaka huu.
MsaniiOmmy Dimpozakizungumza wakati wa kutangaza tuzo hizo

 
Hafla yautangazaji tuzo hizo imefanyiks katika Ukumbi wa Superdom Masaki, jijini Dar es Salaam, zikihusisha wasanii wote wa uchekeshaji nchini.


Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk. Gervas Kasiga, ametangaza vipengele 17 vya tuzo hizo, ambapo washindi wa tuzo tatu kubwa watajinyakulia zawadi za fedha kama ifuatavyo:
- Mchekeshaji Bora wa Kike atapewa zawadi ya Sh20 milioni
- Mchekeshaji Bora wa Kiume atanyakua Sh20 milioni
- Mchekeshaji Bora wa Mwaka atabeba Sh30 milioni

Washindi wa vipengele vingine vya tuzo hizo watapata zawadi ya Sh milioni 5 kila mmoja.

Hafla ya uzinduzi wa tuzo hizo ilifanyika usiku wa kuamkia Januari 16, 2025, katika Ukumbi wa Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
 

Kama unamtaka Shilole, 'mfuate Mafuta ya Korie'

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com


Msanii na mfanyabiashara Zuwena Mohammed maarufu Shilole, ametangazwa kuwa Balozi wa Mafuta ya Kupikia Korie, katika kilichoelezwa ni kuongeza mvuto wake kwa chapa hiyo iliyoboreshwa kwa mwonekano mpya na vifungashio vipya

Msanii Shilole(Katikati), akiongea baada ya kutambulishwa kuwa Balozi wa Mafuta ya Kupikia ya Korie  jijini Dar es Salaam.

Shilole aliongoza uzinduzi wa vifungashio vya nusu lita na robo lita vya mafuta ya Korie, hatua inayolenga kuwafanya Watanzania wengi zaidi kupata mafuta hayo ya kupikia yenye ubora kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo kubwa, Shilole alionyesha furaha yake na kusema:

"Korie Kipochi kimefika kwa mikono sahihi na kwa wakati sahihi! Hata unapomaliza mafuta ghafla, Korie Kipochi ni suluhisho la haraka—kamili kwa dharura za jikoni."

Vifungashio hivi vipya, vilivyotengenezwa kwa mifuko laini ya plastiki chini ya jina "Kipochi", vimebuniwa kwa bei nafuu ili kuwafikia walaji wa kipato cha chini" amesema Shilole

Lengo ni kusaidia familia kupunguza gharama za chakula bila kuathiri ubora wa bidhaa wanazotumia.

Kwa zaidi ya miaka 20, mafuta ya Korie yamekuwa sehemu ya familia nyingi nchini Tanzania, na hatua hii mpya inathibitisha dhamira yake ya kuwafikia watumiaji wote.

Meneja wa Mauzo wa Murzah Wilmar, watengenezaji wa mafuta ya Korie, Steven Ford, alisisitiza kuwa kampuni hiyo inajali afya za walaji wake:
"Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata mafuta bora na salama kwa bei nafuu, hasa wale wanaohitaji chaguo rafiki kwa mfuko wao."

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa walaji kununua bidhaa zilizoidhinishwa na TBS, akirejelea tukio lililotokea Yombo Dovya, ambapo mafuta yasiyo salama yalileta madhara makubwa kwa afya za watu.
"Kwa kutumia mafuta yaliyoidhinishwa, mnalinda afya zenu na kuepuka bidhaa bandia hatari," Ford alionya.

Ingawa masharti ya Mkataba wa  ushirikiano wa Shilole na Murzah Wilmar yamebaki kuwa siri, jambo moja liko wazi—ushawishi wake utaisaidia Korie Kipochi kufika katika kila nyumba Tanzania, kuhakikisha kila familia inapika kwa mafuta salama na yenye ubora wa hali ya juu

Jumamosi, 8 Februari 2025

Mnigeria wa dawa za kulevya waachiwa huru

 DPP asema hana nia kuendeleza kesi 

Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP) ameiomba Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imwachie huru raia wa Nigeria Emmanuel Chiabo na mwenzake wanaoshtakiwa kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine Kilogramu 29.71 sababu hawana nia ya kuendelea na shauri hilo.


Mahakama mbele ya Jaji Godfrey Isaya imepokea maombi hayo na kukubali kuondoa shtaka dhidi ya Chiabo na Goodness Remy.

Wakili wa Serikali Glory Kilawe akiwakilisha Jamhuri aliwataja washtakiwa kuwa ni Chiabo na Goodness Remy ambao walishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.

"Mheshimiwa shauri lilikuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa mashtaka na usikilizwaji wa awali lakini Jamhuri tunaomba kuondoka shtaka chini ya kifungu namba 91(1) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022,"alidai.

Alidai kuwa washtakiwa wanadaiwa Aprili 19 mwaka 2023 maeneo ya Salasala, Mtaa wa Upendo wilayani Kinondoni walisafirisha heroine kilogramu 29.71.

Wakili Glory aliomba Mahakama ikubali kuondoka shtaka kama walivyoomba.

 Wakili wa utetezi Hardson Mchau akijibu alidai hana pingamizi isipokuwa anaomba endapo Serikali itaamua kuwashtaki tena iwarudishwe mahakamani mapema.

Jaji Isaya baada ya kusikiliza maombi ya Jamhuri na majibu ya upande wa utetezi alikubali kuwaachia huru washtakiwa.

"Mahakama inawaachia huru washtakiwa wote wawili , tunawajulisha kuachiliwa kwenu  huru chini ya kifungu cha 91(1) hakuzuii kushtakiwa tena kwa kosa mliloachiwa,"alisema Jaji Isaya.

Washtakiwa wote wamwachiwa huru.

Alhamisi, 6 Februari 2025

'Kocha wa makipa Simba', wenzake wakana mashtaka dawa zakulevya

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MSHTAKIWA Saidi Matwiko na mkewe Sarah Joseph wamekana kukutwa na dawa za kulevya wakati upekuzi ulipofanyika nyumbani kwao Kivule katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.


Matwiko na Sarah wamekana maelezo hayo waliposomewa mashtaka na maelezo ya awali katika mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na wenzao wanne pamoja na aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Timu ya Simba Muharami Sultani.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu mbele ya Jaji Godfrey Isaya  Februari 5,2025.

Watuhumiwa hao wanashtakiwa wakidaiwa kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 34.89.

Pia mmiliki wa Ktuo cha Michezo cha Cambianso, kilichoko Tuangoma, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Kambi Zubery anashtajiwa kwa kutakatisha fedha ambapo anadaiwa kujipatia magari matano aina ya Tata huku akijua Mali hiyo inatokana na zao la kuongoza genge la Uhalifu.

 Akiwasomea mashtaka watuhumiwa hao, Wakili wa Serikali Tully Helela amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane ambapo inadaiwa, wote kati ya Mwaka 2016 na Novemba 2022 maeneo ya Dar es Salaam na Mkuranga waliongoza genge la Uhalifu na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.

Imeadaiwa mahakamani hapo kwamba Oktoba 27, 2022  maeneo ya Kivule , Ilala mkoani  Dar es Salaam, washtakiwa wote walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilogramu 27.10. 

Pia ilidaiwa kwamba Novemba 4, 2022, eneo la Kamegele Mkuranga, wote kwa pamoja walikutwa wakisafirisha kilogramu 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroine.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Kambi anakabiliwa na mashtaka  matano ya kutakatisha fedha, alijipatia magari matano aina ya Tata wakati akijua mali hizo zimetokana na mazalia ya kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Kambi, Sultani, Maulid Mzungu, maarufu Mbonde, Said Matwiko, John Andrew maarufu Chipanda ambaye ni mfanyakazi wa Cambiasso na Sara Joseph ambaye ni mke wa Matwiko. 

Katika usikilizwaji wa awali  wa shauri  hilo, Wakili Tully alidai maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya wakiwa kwenye doria maeneo ya Kivule walipata taarifa ya watu wanasafirisha dawa za kulevya.

Alidai maofisa walikwenda  nyumbani kwa mshtakiwa Saidi Matwiko na kundi lingine lilielekea Kitunda Magole kwa mshtakiwa John.

Ilidaiwa katika upekuzi nyumbani kwa Saidi walikuta pakiti 27 zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya, mshtakiwa Saidi na Sarah walikamatwa na vielelezo vilipelekwa kwa mkemia kwa ajili ya uchunguzi ambako ilibainika ni dawa za kulevya aina ya heroine.

Ilidaiwa pia upekuzi ulifanyika nyumbani kwa washtakiwa wengine wote na nyumbani kwa Maulid walikuta pakiti nane za dawa za kulevya.

Akijibu, mshtakiwa Kambi alidai upekuzi ulipoanyika nyumbani kwake hakuwepo na zilichukuliwa Sh milioni tisa na gari.

Alidai hakukamatwa katika mpaka wa Horohoro Tanga akitaka kukimbilia Kenya, bali alikamatwa maeneo karibu na Horohoro.

Naye mshtakiwa Kambi alikana kuwafahamu washtakiwa wengine wote, lakini mshtakiwa wa pili na watatu walikubali kwamba wao ni ndugu na mshtakiwa wa nne alikubali kwamba mshtakiwa wa sita ni mke wake.

Mshtakiwa wa nne katikashauri hilo Saidi alidai upekuzi ulipofanyija nyumbani kwake hawakukuta kitu chochote.

Kwaupande mwingine mke wa Saidi, Sara alidai wakati wa upekuzi hakuwepo nyumbani na kwamba alikamatwa mchana, wala hakukamatwa pamoja na mumewe kama inavyodaiwa.

Upande wa Jamhuri una jumla ya mashahidi  30 na vielelezo 90 kwa ajili ya kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.