-Awaambia NO uteuzi kwa majungu
Exuperius Kachenjea na Joddet Dominic, daimatznews@gmail.com
Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina jukumu kubwa katika kutekeleza mageuzi ya sekta ya makazi nchini akihimiza kuongeza ufanisi, kufanya maamuzi kwa haraka na kuhakikisha mali za umma zinatumika ipasavyo.
Mchechu pia amesema mafanikio ya mageuzi hayo yanahitaji mshikamano na uwajibikaji wa pamoja kwa wafanyakazi wote, huku akionya watumishi kuacha majungu badala yake kuchapakazi kwani ndiyo njia ya mafanikio.
"Ili tufanikiwe, tunahitaji kuwa na timu inayofanya kazi kwa upendo, siyo kwa majungu. Mimi mwenyewe ninaweza kuwa mmoja wa waathirika wa majungu, lakini nawaombeni sana mfanye kazi kwa upendo," amesema Mchechu.
Amesisitiza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji hautazingatia maneno ya pembeni bali ufanisi na uwezo wa mtu katika kutekeleza majukumu yake.
Ametoa wito kwa wafanyakazi wa taasisi zote za umma kushikamana na kushirikiana kwa karibu katika mchakato wa mageuzi, kwani mshikamano ndiyo msingi wa mafanikio.
![]() |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, wakifuatilia mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili Kibaha, mkoani Pwani Februari 24 hadi 25, 2025. |
"Hatutateua mtu kwa sababu ni bingwa wa kupiga majungu, tutateua kwa ufanisi. Naomba tuwe na mshikamano ili kuhakikisha taasisi zetu zinapiga hatua kubwa katika maendeleo," amesisitiza.
Kuhusu miradi inayotekelezwa na NHC Mchechu ameliambia Baraza la Wafanyakazi wa NHCkwamba maeneo muhimu kama Urafiki na Morogoro tayari yametolewa kwa matumizi ya shirika, huku akitoa angalizo kuwa mali hizo hazipaswi kutumiwa vibaya.
"Hatutaruhusu mali hizi zitumike vibaya. Tunataka kuona ufanisi unaongezeka na kuhakikisha tunasimamia sekta ya makazi kwa weledi," amesema.
Kwa mujibu Msajili huyo wa Hazina, mageuzi katika taasisi za umma ni safari isiyoepukika, ikilenga kuimarisha utendaji, ufanisi na kupunguza utegemezi wa Serikali katika uendeshaji wa mashirika yake.
Mchechu amebainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kuchukua hatua za msingi kuhakikisha taasisi zinazojitegemea zinafanya mageuzi yenye tija.
"Reforms is a journey – mabadiliko ni safari, ni lazima tuyafanye kwa umakini na dhamira ya kweli," amesema Mchechu, akifafanua kuwa mwaka huu Serikali imeanza kutumia mfumo wa ukaguzi wa CAG katika kutathmini vigezo vya utendaji kazi (KPI).
Amesema kuwa taasisi 58 zinazojitegemea zimeanza kupitia mchakato huo ili kuhakikisha zinajiendesha kwa weledi na uwazi.
Katika jitihada za kuimarisha uwajibikaji, Msajili wa Hazina amesema Serikali itateua taasisi maalum kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa viashiria vya utendaji (KPI Monitoring), ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa na utegemezi unapunguzwa.
Mchechu ameweka wazi kuwa changamoto kubwa iliyopo ni jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi, ili taasisi ziweze kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkutano huo wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC unafanyika leo na kesho ukihusisha mijadala yenye lengo la kuimarisha utendaji wa shirika, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha mageuzi yanatekelezwa kwa tija na uwazi.
0 Maoni