-Mkurugenzi ataja mambo10 atakayosimamia kufikia malengo
Joddet Dominic na Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Kibaha, Pwani. Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dk. Sophia Kongela, amewapongeza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa mijadala yenye tija.
Amesema ameguswa hasa na mjadala kuhusu bajeti ya shirika hilo kwa mwaka 2025/26, inayolenga kuboresha utendaji kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa nyumba.
![]() |
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)Dk.Sophia Kongela, akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC,Kibaha Pwani,Februari 25,2025. |
Dk. Kongela ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha Pwani, Februari 24 na 25, 2025 ambapo aliwahimiza wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu, waaminifu, na kujituma katika majukumu yao, akisisitiza kuwa mshikamano na maadili bora ndio nguzo ya mafanikio ya shirika.
Katika hotuba yake Dk. Kongela alieleza kuwa NHC imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa akitaja awamu ya kwanza ya Mradi wa Samia Housing Scheme, inahusisha ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe, Dar es Salaam, pamoja na majengo ya ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.
"Mafanikio haya yamewezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hasa katika kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa miradi ya kimkakati ya ujenzi,"amesema Dk. Kongela.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa rasilimali za shirika,akitoa wito kwa wafanyakazi kuhakikisha ukusanyaji wa madeni ya kodi ya pango unaimarishwa ili kuongeza mapato ya Shirika.
Dk.Kongela pia amehimiza kila mfanyakazi wa NHC kufanya kazi kwa uwazi, bidii na mshikamano, akiunga mkono kauli ya Msajili wa Hazina,Nehemia Mchechu katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo na sisitiza kuwa majungu na makundi hayana nafasi ndani ya NHC linalojizatiti kufanikisha malengo yake.
Mkutano huo umejadili masuala mbalimbali muhimu ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya NHC, ambapo wajumbe wametakiwa kuhakikisha kuwa shirika hilo linaendelea kutoa gawio kwa Serikali, ambalo kwa mwaka huu linakadiriwa kufikia shilingi bilioni 6.5.
Awali,akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Hamad Abdallah amesema kuwa dhamira yake ni kuongoza NHC kwa weledi, uadilifu na bidii ili kuhakikisha ongezeko la ufanisi na tija katika utoaji wa huduma bora za makazi nchini akitaja mambo kumi atakayosimamia utekelezaji wake.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo,Kibaha Pwani Februari,2025 |
"Kwa msingi huo, NHC itaendelea kutekeleza yafuatayo; Kuongeza ufanisi, kuboresha mifumo ya usimamizi wa miradi, rasilimali watu na huduma kwa wateja, ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama zisizo za lazima,"
Amteaja mengine kuwa ni kufanya kazi kwa weledi,kuhakikisha kuwa kila hatua inazingatia viwango vya kitaalamu na ubora wa hali ya juu,kujenga uadilifu na uwajibikaji, kusimamia rasilimali kwa umakini na kuongeza uwazi na uwajibikaji wa wafanyakazi kwa maslahi ya umma.
Mkurugenzi huyo pia ametaja kuhamasisha ubunifu na ushirikiano,kushirikiana na wadau wa sekta ya ujenzi, taasisi za kifedha, na wawekezaji ili kuongeza upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu, kusimamia miradi ya kimkakati, kutekeleza miradi mikubwa ya makazi na biashara katika mikoa mbalimbali ili kusaidia kupunguza uhaba wa makazi na kuchochea maendeleo ya miji.
"Kwa kushikamana na maadili ya kazi, bidii, na mshikamano, wafanyakazi wa NHC wataendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya sekta ya makazi nchini," amesema Hamad.
0 Maoni