Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mshtakiwa dawa za kulevya adai kuitilia shaka Jamhuri

 -Ni kwa kutotajwa vielelezo vilivyochukuliwa nyumbanil kwake 

MwandishiWetu,daimatznews@gmail.com

MSHTAKIWA katika kesi ya dawa za kulevya, Sharifa Majani amesema anautilia  shaka upande wa Jamhuri, kwani haukutaja mahakamani vielelezo vilivyochukuliwa nyumbani kwake, ikiwemo hati ya nyumba, kadi za Benki na simu zake.

Shughuli za Mahakama ya Mafisadi zikiendelea katika moja ya kesi zilizowahi kusikilizwa na mahakama hiyo.  

Mshtakiwa huyo amekana kujipatia nyumba yenye thamani ya Sh milioni 168 kwa kujihusisha na  biashara ya dawa za kulevya.

Mshtakiwa huyo wa kwanza alidai hayo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati akisomewa mashtaka na maelezo ya awali.

"Mheshimiwa hapa kuna ukakasi, vielelezo vilivyochukuliwa ndani kwangu upande wa Jamhuri hawakuvisema, hati ya nyumba, simu na kadi za Benki,"alidai mshtakiwa.

Sharifa alikana kuwaelezea Polisi kwamba dawa za kulevya zingine zilisafirishwa kwa kutumia basi kwenda Himo.

 Mshtakiwa huyo wa kwanza  pia alidai upekuzi ulifanyika nyumbani kwake lakini hawakukuta dawa za kulevya katika chumba cha kulala.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifa, Chigbo Innocent , Omary Omary na Mandela Masawe, wanadaiwa kati ya Januari mwaka 2019 na Aprili 22 mwaka 2023 maeneo ya Pwani na Kilimanjaro washtakiwa waliongoza genge la Uhalifu kufanya kosa la jinai.

Mshtakiwa wa kwanza na wapili walidaiwa Aprili 20 mwaka 2023 maeneo ya Kiluvya walikutwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 25.

Shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote , ilidaiwa kati ya Aprili 2023 na Aprili 22 mwaka 2023 maeneo ya Kisarawe na Himo walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 45.86.

Shtaka la nne linamkabili mshtakiwa wa kwanza, Sharifa ilidaiwa alitakatisha fedha kati ya Januari 2019 na Aprili mwaka 2023 maeneo ya Kiluvya.

Imedaiwa mshtakiwa huyo alijipatia nyumba yenye thamani ya Sh milioni 168 huku akijua mali hiyo ni mazalia ya kosa la jinai.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na waliposomewa maelezo ya awali mshtakiwa wa kwanza alikubali anaishi Kiluvya Madukani , mshtakiwa wa pili anaishi Goba na mshtakiwa wa tatu na wanne wanaishi Himo mkoani Kilimanjaro.

Mshtakiwa wa 1,2 na 3 walikana kufahamiana lakini walikubali kwamba walifanyiwa upekuzi katika nyumba zao.

Ilidaiwa ni kweli nyumbani kwa mshtakiwa wa pili walikuta gari moja na simu tatu lakini mshtakiwa wa pili alikana kuwapeleka maafisa wa Polisi nyumbani kwa mshtakiwa namba moja Kiluvya.

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo unatarajiwa kuita mashahidi 27, vielelezo vya maandishi 24 na vielelezo halisia tisa.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mruge Karoli alidai washtakiwa katika shauri hilo watajitetea wenyewe na hawatakuwa na vielelezo. Shauri liliahirishwa hadi tarehe nyingine itakayopangwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni