Safari ya Mradi wa 2H wa NHC Morogoro

 -Kutoka mchanga hadi mnara wa matumaini katikati ya Moro

-NHC yawekeza bil 2.5, yapandisha hadhi Mji kasoro bahari

-Ni jengo linalobadilisha sura ya Morogoro

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Hakika sasa Morogoro ni mjini kasoro bahari, kwani katikati ya mji huo uliobeba historia ya kusifika ya milima inayotiririsha maji, utawala wa Chifu Kingalu wa Waluguru, wasanii wakongwe wa muziki nchini hata chimbuko la vipaji vya mpira nchini imesimikw alama mpya ya matumaini na maendeleo.

Ukitaja historia ya Morogoro, huwezi kuwaweka kando wasanii maarufu wa muziki kuwataja wachache kama marehemu Mbaraka Mwishehe na Moro Jazz, lakini pia huiweki kando Cuban Marimba Band na marehemu Juma Kilaza.

Lakini kwa mpira wa miguu huwezi kuwaacha Gibson Sembuli (marehemu), Husein Ngulungu(marehemu), Hamisi Gaga(marehemu) na Zamoyoni Mogella, tukiwataja kwa uchahe.

Jengo hilo linaloongeza thamani ya Morogogro linajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia Mradi wa 2H-Morogoro, lipo katika Mtaa maarufu wa Lumumba, likionekana ni ghorofa la kisasa lakini pia likiupa mji huo sura mapya.

Hata hivyo, kwa macho ya mpita njia, jengo hilo linaonekana ni ghorofa la kisasa; lakini kwa wale wanaofahamu undani wa Mji wa Morogoro, jengo hilo ni sehemu ya hadithi nzuri ya mabadiliko makubwa yanayotekelezwa na NHC, si kwa Morogoro pekee, bali katika miji mbalimbali Tanzania nzima.

Hadithi hiyo ilianza Juni mwaka 2024, wakati jiwe la msingi la ujenzi huo lilipowekwa, huku ukamilifu wake ukiakisi bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 2.5.

Bajeti hiyo ilitoa taswira kwamba jambo kubwa linaekea kutekelezwa, ambalo sasa Oktoba 2024 ujenzi wake umefikia zaidi ya  ya asilimia 97, huku kila sakafu iliyoongezwa ikimama kama ukumbusho wa bidii na nidhamu ya watendaji wa NHC kuibadili taswira ya Mji wa Morogoro.

Hata Meneja wa NHC Mkoa wa Morogoro, Eliaisa Keenja, ameipokea sehemu kubwa ya kazi kutoka kwa wakandarasi kwa tabasamu la ushindi, akijua kwamba mwisho wa safari uko karibu.

Eliaisa anasema kuwa ndani ya jengo hilo kuna hadithi nyingine ya kuvutiai. Kuna nyumba za makazi zenye ukubwa wa mita za mraba 39, zilizobeba ndoto ya wanafunzi wa vyuo na wataalamu wachanga wanaotafuta makazi ya bei nafuu yenye mwonekano wa kisasa.

Meneja wa NHC Mkoa wa Morogoro, Eliaisa Keenja

Kwa mujibu wa meneja huyo, kuna nyumba za chumba kimoja za kati ya mita za mraba 47 hadi 66, zikitoa faraja kwa familia ndogo au watu wanaopenda utulivu. Kwa familia kubwa zaidi, kuna nyumba za vyumba viwili vya kulala zenye mita za mraba 100 zinaong’aa zikiwa ni suluhisho la makazi yenye nafasi, mwonekano wa kuvutia na mpangilio makini wa ndani.

Katika jengo hilo la Mradi wa 2H-Morogoro, kila ghorofa si tu makazi, bali pia ni jukwaa la kijamii. Eneo la pamoja lenye zaidi ya mita za mraba 86 limewekwa kwa ajili ya hewa safi, mazungumzo ya jirani na mshikamano wa kijamii.

Mradi wa 2H-Morogoro ni mahali ambapo watoto wanacheka, watu wazima wanabadilishana mawazo, na majirani wanakuwa marafiki.

Ukitembea ndani ya jengo hilo la kisasa, unakutana na lobby yenye mwanga mkali wa kisasa, mlango wa mapokezi unaowapa wageni na wakazi hisia ya heshima.

Si hivyo tu, bali pia nyumba zina maeneo ya jiko yaliyobuniwa kisasa, sebule zilizochangamka na vyoo vilivyowekwa kwa ustadi.

Balcony za nyumba hizo zinakupeleka moja kwa moja kwenye anga la Morogoro, zikikupa mandhari ya kuvutia ya milima na mji.

Kwa Dk. Godwin Maro, Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC, hilo si jengo tu, bali ni ushahidi wa dhamira ya shirika hilo kuwapatia Watanzania makazi bora ya kisasa.

Maro anasema kwa msisitizo kwamba 2H Morogoro limejengwa kwa viwango vya kimataifa, likijali uimara, usalama na uendelevu.

“Jengo hili ni kielelezo cha Tanzania mpya, inayohimili mabadiliko ya sekta ya makazi na ongezeko la watu katika miji yake,” anasema.

Maro anaeleza kuwa matokeo chanya ya mradi huo ni zaidi ya muonekano wake kwani kiuchumi, jengo hilo la Mradi wa 2H-Morogoro linafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira.

Anasema kijamii, jengo hilo linaimarisha ubora wa maisha kwa wakazi wa Morogoro, linawapa makazi bora na salama, lakini kimkakati, linainua hadhi ya mji huo na kuupa nafasi ya pekee kwenye ramani ya maendeleo ya kitaifa.

Sehemu ya jengo la Mradi wa 2H-Morogoro inavyoonekana.

Maro anabainisha kuwa wakati jengo hilo linapokaribia kukamilika sasa, watu wa Morogoro wanaliona kama ishara ya zama mpya.

“Linapendeza kwa macho, lakini zaidi ya hapo, linaibeba ahadi ya taifa linalosonga mbele kuelekea ustaarabu wa miji wa kisasa,” anasema.

Kwa hakika, 2H – Morogoro si ghorofa tu; ni simulizi ya ustahimilivu, ndoto na uthubutu. Ni almasi mpya inayoangaza katika moyo wa Mji wa Morogoro, ikiweka kumbukumbu ya kizazi hiki na kuandaa njia ya vizazi vijavyo.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi