Hospitali ya Shifaa yawshukuru wananchi
- Yasema haibagui ipo kwa ajili ya Watanzania wote
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Uongozi wa Hospitali ya Shifaa ya Dar es Salaam umewashukuru wananchi wanaofika hapo kupata huduma za afya, tiba na ushauri katika miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, ikieleza kwamba inaunga mkono juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya kwa watanzania wote wenye changamoto za kiafya na maradhi mbalimbali, ikiwamo wanaojigharamia kwa fedha taslimu hata walio na bima mbalimbali za afya ikiwamo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
![]() |
Sehemu ya Jengo la Hospitali ya Shifaa iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam linavyoonekana. |
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Bashir Haroun ameeleza katika miaka miwili tangu kuanza kazi kwa hospitali hiyo bado msimamo wao ni kushikamana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwahudumia wnanchi wote bila kubagua.
Hospitali hiyo ya kisasa ya Shirika la Shifaa Pan African Hospitals Limited chini ya Kundi la Makampuni ya Oil Com, ipo maeneo ya Kinondoni, Barabara ya Msese, ikiwa na kauli mbiu ya kuboresha huduma za afya nchini, uwekezaji wake ukigharimu Dola za Marekani milioni 60, takriban Shilingi bilioni 162.
“Hospitali ya Shifaa inatoa huduma kwa wote bila kubagua hali ya maisha, tunapokea na kuwatibu, wapo wanaogharamia matibabu kwa fedha taslimu, pia wapo wananchi wanaotumia bima za kampuni mbalimbali ikiwamo Bima ya Afya ya NHIF, ingawa wapo wenye mtazamo kuwa hatupokei wenye bima za NHIF jambo ambalo si kweli. Hao wana lengo la kuwakosesha wananchi huduma bora na za kisasa za hospitali yetu," anasema Bashir.
![]() |
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Shifaa, Bashir Haroon |
Anaongeza: "Hata wale wanaosita kuja kwa kuogopeshwa na mazingira bora ya jengo la hospitali, wasiogope kuja hilo ni moja ya lengo letu kutoa huduma bora za afya katika mazingira bora, tunaamini hilo pia ndio lengo la Serikali. Hospitali ya Shifaa imejengwa kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote bila ubaguzi.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mtendaji, ujenzi wa Shifaa Hospitali umezingatia mambo matatu muhimu ambayo ni pamoja na miundombinu bora ya kisasa, vifaa tiba bora na vya kisasa ikiwamo vipimo na watoa huduma wenye viwango bora vya taaluma.
![]() |
Moja ya maeneo ya kuhudumia wananchi katika Hospitali ya Shifaa, Dar es Salaam. |
Bashir amesisitiza; “Tupo kwa ajili ya Watanzania, tunaunga mkono juhudi za Serikali kutoa huduma bora za afya. Hapa hatubagui bima ya afya, pia tuna kitengo cha ustawi wa jamii. Muhimu Watanzania wapate huduma bora za afya.”
Maoni
Chapisha Maoni