FCC, ZFCC 'zafunga ndoa' kulinda haki za mlaji

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Tume ya Ushindani Tanzania Bara -FCC na Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar -ZFCC, zimeingia mkataba wa makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine, zinalenga kujielekeza katika kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa feki.

Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam,  ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Hashil Abdallah aliyeshuhudia tukio hilo, amezielekeza FCC na ZFCC kufanyia kazi mambo yote yaliyokusudiwa ili ziweze kuongeza ufanisi kwa maslahi mapana ya Tanzania.

Amesema makubaliano hayo yanapaswa kujikita katika kutatua changamoto za ushindani ikiwemo kwenye sekta ya biashara na viwanda lengo ni kuleta uhimilivu toshelezi wa uchumi.

Kwanza, FCC na ZFCC zinapaswa kuteua watu au timu maalum kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya. Pia, ndani ya kipindi cha miezi mitatu—au hata chini ya mwezi mmoja—ni muhimu kutengeneza nyaraka kama ‘roadmap’ au ‘plan of action’ zitakazotuongoza katika utekelezaji,” amesema Dk. Hashil.

Amesisitiza umuhimu wa kupanga muda wa utekelezaji wa kila jukumu walilonalo akieleza;. “Kitu kisipopangiwa muda mara nyingi hakitekelezeki. Tunapaswa kujua tunatekeleza nini na kwa muda gani, ili tukifika wakati husika tuweze kujitathmini.”

Katika hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Aliyah Juma, amesema tume yake ipo tayari kushirikiana na FCC kwa karibu hasa katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

“Tunalenga kushughulikia changamoto zote zilizopo sokoni kwa pamoja ili kulinda ushindani wenye tija na haki kwa pande zote. Sisi kama ZFCC tuko bega kwa bega kuhakikisha kile kilicho kwenye makubaliano kinatekelezwa kwa weledi na ufanisi,” amesema Aliyah.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni ishara ya mshikamano wa kitasisi na dhamira ya pamoja ya kulinda ushindani wa haki na maslahi ya walaji katika pande zote za Muungano.

“Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza nguvu na uwezo wa pamoja kukabiliana na changamoto za ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji, ambazo mara nyingi huathiri Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Khadija.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi