Makamu wa Rais alivyotoa maagizo, NHC yafunguka
- Mkurugenzi Hamad aeleza NHC ilivyogusa kila mkoa Tanzania
- NHC ilivyong’ara mkutano wa Wenyeviti wa Bodi,
Wakurugenzi Arusha
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Phillip Mpango, ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuongeza juhudi
zake katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, lengo likiwa ni kuhakikisha
wananchi wote wanaostahili kupata makazi wanapata fursa hiyo kupitia shirika
hilo.Makamu wa Rais Dk. Isdor Mpango(Wa kwanza Kulia) akitembelea mabanda ya maonyesho ya shughuli zinazofanywa na taasisi za umma Viwanja vya AICC, Arusha hivi karibuni.
Dk. Mpango ametoa agizo hilo wakati alipotembelea banda la
NHC kwenye viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC),
wakati wa Kongamano la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma.
Alizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo lililofanyika kuanzia tarehe 23
Agosti, 2025.
"Nawaagiza muongeze juhudi za ujenzi wa nyumba za
gharama nafuu ili muwawezeshe wananchi wote wanaotamani au kuhitaji kumiliki
nyumba za NHC wapate nafasi hiyo," alisema Dk. Mpango.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hammad Abdallah, amelitolea majibu agizo hilo akieleza kuwa shirika hilo kwa sasa lina mpango mkubwa unaolenga kuhakikisha agizo hilo linafanyiwa kazi kwa ufanisi.
"Tuna miradi karibu kote nchini Tanzania kwa sasa
hivi," amesema Hamad, na kuongeza
kuwa hatua zote zinazohitajika zinaendelea ili wananchi waweze kumiliki nyumba
zilizojengwa na NHC kwa urahisi.
Kuhusu miradi ya NHC mkoani Arusha, Hamad ameeleza kuwa kuna
mradi wa nyumba 711 ambao tayari asilimia 20 ya nyumba hizo zimeuzwa na ujenzi
unaendelea. "Ni moja ya miradi ya muda mrefu iliyokwama, lakini
tunashukuru Serikali kwa kutuwezesha kuukwamua. Tulirudi kukopa na sasa ni
mradi ambao una tija kubwa kwa taifa," amesema.
Ameongeza kuwa mkoani Arusha NHC pia ina miradi mingine
ikiwemo Mradi wa Safari City ambao NHC imenunua ekari 500 za ardhi,
imetengeneza mpango wa jumla (master plan), inaweka miundombinu na kuuza
viwanja kwa wananchi.
"Awamu ya kwanza tulimaliza kuuza viwanja na sasa
tunaandaa awamu ya pili. Baada ya kuuza viwanja tulipata tija kubwa, sasa
tumekuja na mradi wa awamu ya tatu tayari tumeuanza ujenzi na tumeshauza
asilimia 25 ya nyumba hizo," amefafanua Hamad.
Hamad alimueleza Makamu wa Rais kuwa NHC inafanya miradi
mikubwa katika mikoa mbalimbali nchini, akikitaja mkoa wa Morogoro ambapo una
miradi miwili, Tanga kwenye mradi wa jengo kubwa la Mkwawani Plaza, na Iringa
kwenye Mradi wa Iringa Plaza.
"Kwa hiyo karibu
maeneo yote ya nchi tumeweza kuyagusa, Mheshimiwa Makamu wa Rais," amesema.
Mbali na Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene naye ametembelea
banda la NHC kwenye kongamano hilo. Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah,
aliongoza maonesho ya huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo,
zilizovutia viongozi na wadau wa sekta ya fedha na umma.
Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa mashirika ya
umma, wenyeviti wa bodi na watunga sera, kwa lengo la kujadili mbinu za
kuimarisha taasisi za umma na mchango wao katika maendeleo ya taifa. Banda la
NHC lilivutia wengi ikiwemo mawaziri, wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa taasisi
za umma na wananchi, wakionyesha dhamira ya shirika la kushirikisha wadau wengi
katika utekelezaji wa majukumu yake.
Katika kongamano hilo, NHC pia ilipata tuzo maalum kutoka
Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwa moja ya mashirika ya umma yaliyofanya
vizuri katika mwaka wa fedha 2023/24.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi wa NHC, Dk.
Sophia Kongelo na Mkurugenzi Mkuu,Hamad Abdallah.
Vigezo vilivyotumika katika utoaji tuzo ni pamoja na ukuaji
wa mapato ya ndani, kuboresha uwazi, rejesho la uwekezaji, udhibiti wa
matumizi, kuimarisha faida, kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali, ufanisi
katika matumizi, utekelezaji wa hoja za kikaguzi, uchapishaji wa taarifa za
fedha, na maboresho ya utoaji huduma kwa jamii.
Maoni
Chapisha Maoni