Jumanne, 5 Agosti 2025

Majangili wabanwa Ranchi ya Mwiba, Pori la Akiba la Maswa

Mwandishi Wetu,Meatu

 Ushirikiano baina ya Askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA) Taasisi ya Uhifadhi ya Mwiba Holdings na Askari wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Mara, umefanikisha kudhibiti watukio ya ujangili katika eneo la pori la Akiba la Maswa na Ranchi ya Mwiba.

Wakizungumza katika Maadhimisho ya Kimataifa la Walinzi wa Wanyamapori Duniani Agosti 5-2025 kwa lengo la kuenzi kazi nzuri inayofanyika na walinzi wa wanyamapori, Askari wa Wanyamapori, wamesema wanaadhimisha siku hiuo kwa mara ya kwanza wilayani Meatu, wakiwa na faraja kubwa kudhibiti ujangili.

Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi cha Kampuni ya Mwiba Holdings, iliyo chini ya Taasisi ya Friedkin Conservation Fund, waliowekeza katika Pori la Akiba la Maswa na Ranchi ya Mwiba,Steve Alexander amesema ushirikiano baina yao na TAWA umekuwa na manufaa.

Alexander ambaye ni mbombezi katika masuala ulinzi wa wanyamapori, amesema kutokana na ushirikiano huo sasa matukio ya majangili wakubwa wa wanyamapori yamedhibitiwa.

Amesema, ujangili uliopo sasa ni wa watu wachache tu kuvamia maeneo ya hifadhi, kukata kuni na mbao na wengine kutega wanyama wadogowadogo kwa ajili ya kitoweo.

“Lakini pia kulikuwa na changamoto ya ng'ombe kuingizwa hifadhini, ambapo takriban ngómbe 4,000 tuliwakamata na wafugaji kupewa elimu ya uhifadhi na wakalipa faini na kurejeshewa mifugo yao,”amesema.

Amesema wananchi wa Wilaya ya Meatu na Tanzania kwa ujumla wanapaswa kuendelea kulinda Maliasili zao, kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo kwani maliasili zimekuwa na faida kubwa kwa wananchi.

Askari wa Wanyamapori, Mange Gushaha alizipongeza taasisi za Mwiba Holdings na Friedkin kwa kuwawezesha kwa mara ya kwanza kusherehekea Siku ya Walinzi wa Wanyamapori Duniani akieleza wanaiona thamani yao.

“Jambo hili limetupa moyo sana kwani tumeona wamiliki wa kampuni na Serikali wanathamini kazi yetu na imetupa nguvu kufanyakazi nzuri zaidi,”amesema.

Askari wa Wanyamapori Ntungwa Sai amesema mafanikio makubwa wanayosherehekea katika Siku ya Walinzi wa Wanyamapori ni jamii kuelewa umuhimu wa wanyamapori, hivyo kuacha vitendo vya ujangili.

“Sisi kama walinzi wa wanyamapori, kazi yetu imekuwa rahisi kwani jamii imepewa elimu na imeanza kuthamini wanyamapori na mazingira na wakiona majangili wanatupa taarifa na tunashirikiana na TAWA kuwadhibiti,”amesema.

Askari wengine wa Wanyamapori, Elias Kija na Kyara Raimond, wamesema wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kulinda wanyamapori na wamepata faraja kubwa kutambuliwa kwa mchango wao na kufanyiwa sherehe.

“Hii ni mara yetu ya kwanza kufanya sherehe, tunaipongeza Friedkin Conservation Fund na Serikali kwa ujumla, kutambua mchango wetu na tunaahidi kuendelea kulinda rasilimali za Taifa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,”amesema Kija.

Kwa upande wake, Kyara amesema, wanyamapori katika eneo hilo wamekuwa na faida kubwa kwani ajira zinatolewa, shule zinajengwa, huduma za afya zinatolewa lakini pia maji yamechimbwa kwa ajili ya binaadamu na mifugo.

“Tutaendelea kulinda hii rasilimali hapa Meatu kwani faida zake ni nyingi sana na haki sasa katika shule ya msingi Makao wanafunzi wanapata chakula cha mchana bure kutokana na faida za uhifadhi,”amesema.

Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Joseline Mpelasoka amesema ushirikiano baina ya Mwiba, TAWA na umekuwa na manufaa makubwa sana katika kudhibiti matukio ya ujangili.

“Tofauti na miaka ya nyuma hivi sasa matukio yamepungua sana na ujangili uliopo ni mdogomdogo wa mkaa na nyama kwa ajili ya kitoweo nao tunapambana kuukomesha kabisa”amesema

Naye,Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura amesema ushirikiano baina ya wawekezaji na Serikali katika wilaya hiyo, umekuwa na manufaa makubwa.

“Tumedhibiti sana ujangili,lakini Mwiba imetangaza wilaya yetu kwani wameshinda camp bora ya Utalii Tanzania mwaka huu, hivyo tunawapongeza na tunawaita watalii zaidi kutembelea wilaya yetu ya Meatu”alisema.

Katika maadhimisho ya siku ya walinzi wa wanyamapori mwaka huu, Kauli Mbiu ni Walinzi Wanaoendeleza Uhifadhi wa Mabadiliko.

Siku ya Ulinzi wa Wanyamapori ilianzishwa Julai 31 mwaka 1992 nchini Uingereza na ilifatiwa na kuundwa shirikisho la Kimataifa la walinzi wa Wanyamapori(IRF) mwaka 2007 Julai 31 na ndio ilianza rasmi kuadhimishwa siku hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni