Mambo matano ya kipekee usiyoyajua Hifadhi ya Taifa Saadan
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Licha ya Tanzania kuwa na hifadhi 21 za Taifa
zenye vivutio mbalimbali vya utalii, Hifadhi ya Taifa Saadan imebahatika kuwa
na vivutio vya kipekee barani Afrika, hivyo kuitofautisha na nyingine.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani inayopatikana eneo
la mikoa ya Pwani na Tanga ina mambo
matano yanayoelezwa kuitofautisha na nyingine nchini, hata barani Afrika hivyo kuwa
ya kipekee.
Hifadhi hiyo iliyopo katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na wilaya za Handeni na Pangani Mkoa wa Tanga ina ukubwa wa takriban Kilomete za mraba 1,100 na ilianzishwa mwaka 2009.
![]() |
Ofisa Mhifadhi, Utalii, Hifadhi ya Taifa Saadan, Daud Gordon |
Akizungumza na wanahabari ndani ya hifadhi hiyo, Ofisa Mhifadhi, anayeongoza kitengo cha utalii, Hifadhi ya Taifa Saadan, Daud Gordon ameyataja mambo hayo kuwa ni makutano ya Bahari ya Hindi na nyika, uwepo wa mlango bahari wa Mto Wami unaoingia Bahari ya Hindi na mazalia ya kasa wa kijani.
Mengine ni wanyama na binadamu
kukutana kwenye fukwe wa Bahari ya Hindi wakivinjari na mbuyu wenye taswira ya Bikira Maria.
Gordon amesema upekee huo hauishii kwenye mambo hayo manne tu, bali pia Hifadhi ya Taifa Saadan ina makundi ya wanyama zaidi ya matano, wakiwamo wanyama wakubwa(Big Five), wanne kati ya watano ambaoni Simba, Tembo, Nyati na Chui, huku akikosekana Faru pekee.
Kwa mujibu wa Gordon, mbali na wanyama hao wakubwa wanne, wanyama wengine wakiwamo pundamilia, ngiri na nyani hufika ufukweni kupumzika, jambo ambalo ni adimu
katika hifadhi zingine duniani.
Alisema mbali na hayo, Hifadhi ya Saadani ina Msitu wa Zalaninge ulio na uoto wa asili, unaochangia upatikanaji wa mvua pamoja na miti ya mikoko inayosaidia viumbe hai kama kasa na dagaa Kamba kuzaliana kwa wingi katika eneo hilo.
Mmoja kati ya wanyama wanaovutia hifadhini, Twiga akijipatia chakula Hifadhi ya Taifa Saadan. |
“Hifadhi hii ina utalii wa aina nyingi, pia
tunasimamia Kituo cha Malikale chenye kumbukumbu ya biashara ya utumwa cha
Caravan Serai cha mjini Bagamoyo, eneo la magofu yaliyotumika kuhifadhi
watumwa, mbuyu uliotumika kunyongea watumwa, makaburi ya wamisionari wa kwanza kufika
eneo hili kueneza ukristo,” alisema.
Gordon aliongeza: “Pia tuna utalii wa dini, tuna eneo la Mti wa Mbuyu wenye sanamu inayoshabihiana na Bikra Maria ikiwa ya asili ambayo hakuna aliyeichora, bali imekutwa hapo. Huu ndiyo upekee wa Saadani.”
Magofu ya lililokuwa Soko la Watumwa lilipo eneo la Kijiji cha Saadan, mkoani Pwani. Picha zote na Exuperius Kachenje. |
Alisema ili kuendelea
kuimarisha hifadhi hiyo, wametenga maeneo tisa kwa ajili ya uwekezaji upande wa
huduma za malazi, utalii wa fukwe na michezo ya baharini.
Alieleza kuwa hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka
2005 kutoka kuwa pori la akiba ina malango makuu ya nchi kama Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA),
Bandari Kuu, miji ya kihistoria ya Bagamyo na Zanzbar na kufanya kufikia kwa
urahisi ikitumia usafiri wa anga, maji na barabara.
Lucas Mollel mmoja wa viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Alei Levorosi, Arusha Mjini alisema mambo mbalimbali aliyoyaona kwenye Hifadhi ya Saadani yamemuimarisha zaidi kiimani kwani ameshuhudia uumbaji wa Mungu usiokuwa wa kawaida na kumfanya apumzike mwili na akili hivyo akirudi Arusha atakuwa na nguvu mpya.
“Tuna kila sababu ya kumshuru Mungu, Arusha
kuna hifadhi na Wanyama wengi, lakini sijawahi kuona maji yapo karibu na Bahari,
ambayo hayana chumvi, haya ni maajabu, nimeona vifaa vilivyotumika kufunga
watumwa. Naziomba taasisi za dini na Serikali kuwaleta viongozi hapa Saadan ili
kupumzisha akili na kujifunza mambo ya kale, lakini zaidi kutafakari ukuu wa
Mungu,”alisema Mollel.
Mwisho
Maoni
Chapisha Maoni