Mafanikio ya NHC mageuzi ya makazi Tanzania
-Yaja kivingine na Nyumba Bond
- Fursa mpya kwa wananchi kupata nyumba bora
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku likijidhihirisha kuwa chombo muhimu katika ajenda ya mageuzi ya miji na maendeleo ya sekta ya makazi Tanzania.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah |
Chini ya Serikali ya
Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, NHC limeongeza wigo
utendaji wake kupitia uwekezaji wa kimkakati kwenye sekta ya ardhi na majengo,
usimamizi bora wa miradi na uanzishaji wa ushirikiano mpya kati ya sekta ya
umma na binafsi.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC,
Hamad Abdallah anabainisha hayo, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu kwa
uamuzi wake wa kuingilia kati na kuikwamua miradi mikubwa kadhaa ya NHC iliyokwama,
ambayo sasa imeanza tena baada ya kusimama kwa karibu miaka minane.
Hamad aliyekuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari Abdallah amesema hatua hiyo ya Rais Samia imefungua njia ya maendeleo.
Anasema shirika lake limefanikiwa kupata faida ya jumla ya Shilingi bilioni 235.4 kabla ya kodi, huku Shilingi bilioni 36.8 ikipatikana katika mwaka wa fedha uliopita pekee, kwa mujibu wa ripoti zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hamad anabainisha kuwa
kufikia Juni 2024,thamani ya mali za NHC ilifikia Shilingi trilioni 5.5.
Mkurugenzi huyo wa NHC,
anaweka wazi kuwa katika kipindi hicho, mchango wa shirika kwa Serikali pia
umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Shilingi bilioni 134.4
zimetolewa kama kodi katika kipindi cha miaka mitano, huku Shilingi bilioni
9.85 zikitolewa kama gawio,” anasema Hamad.
Kwa mujibu wa Hamad, mwaka wa fedha 2024/25, NHC imelipa gawio Shilingi bilioni 5.5 ambalo liliweka rekodi na kutambuliwa rasmi na Rais kama mojawapo ya mashirika ya umma yanayofanya vizuri zaidi.
“Kwenye ujenzi, NHC
imejenga nyumba 5,399 zenye thamani ya Shilingi bilioni 659.5 kwa ajili ya
kuuza na kupangisha. Kati ya hizo, nyumba 3,217 zimekamilika, huku 2,182 zikiwa
katika hatua mbalimbali za ujenzi,” anasema.
Akitaja miradi mikubwa
iliyotekelezwa na NHC ndani ya miaka mitano kuwa ni pamoja na Morocco Square,
ambao umekamilika hivi karibuni, baada ya kuchelewa kwa miaka mingi, ikiwamo
pia miradi ya Kawe 711 na Golden Premier
Residence ambayo imefufuliwa kutokana na ufadhili kutoka serikalini.
Mkurugenzi huyo wa NHC
anasena shirika anloliongoza limekamilisha mikataba 67 ya kazi za umma, yenye
thamani ya Shilingi bilioni 458.2, ikiwemo miradi ya kimkakati ya kitaifa kama
vile Soko la Madini la Kimataifa la Tanzanite Mirerani, Kitengo cha Moyo cha
JKCI Dar es Salaam na majengo ya ofisi za wizara mjini Dodoma.
“Kwa kushirikiana na
sekta binafsi, NHC pia imeanzisha miradi ya ubia 21 yenye thamani ya Shilingi
bilioni 351, inayoongeza upatikanaji wa nafasi za biashara na makazi nchini
kote,” anasema Hamad.
Anabainisha kuwa mafanikio
hayo ya NHC yametambuliwa ndani na nje ya nchi, ikiwamo kupata tuzo ya Mjenzi
Bora wa Nyumba za Umma Afrika Mashariki, huku pia shirika likipongezwa kwa viwango vyake
bora vya uandaaji wa taarifa za fedha.
Hamad anaeleza kwamba kwa kupitia mpango wa ‘Nyumba za Samia’ unaolenga kujenga nyumba nafuu 5,000, na mpango wa ‘Nyumba Bond’ wa kuvutia uwekezaji wa umma, NHC inaelekea kuwa mhimili mkubwa wa kushughulikia changamoto ya uhaba wa makazi nchini.
Nyumba Bond
Katika mkutano huo na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya Habari, Hamad anatambulisha mpango wa ‘Nyumba Bond’, akieleza NHC inajiandaa kuzindua mpango huo mkubwa wa ukusanyaji mitaji kupitia uzinduzi wa ‘Nyumba Bond’.
Akifafanua Hamad anasema:
“Dhamana hii ya nyumba, inalenga kukusanya fedha kutoka kwa wananchi na
kuwawezesha Watanzania wa kipato cha aina zote kuwekeza moja kwa moja katika
maendeleo ya makazi.”
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHC, dhamana hiyo itakuwa chombo muhimu katika kuongeza
kasi ya upatikanaji wa makazi nafuu nchini, huku pia ikiwavutia wawekezaji kwa
faida nzuri.
“Nyumba Bond itakuwa
mfano wa kwanza wa aina yake Afrika Mashariki utakaotoa fursa kwa wananchi wa
kawaida, mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni za bima na wawekezaji wa taasisi
kuchangia moja kwa moja kwenye ajenda ya makazi ya kitaifa,” anasema Hamad.
Anasema kwa kutumia
uwekezaji wa umma kwenye miradi mikubwa ya ujenzi, NHC inalenga kuziba pengo la
makazi na kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi.
Hamad anaweka wazi kuwa
tayari NHC imeanza mashauriano na mamlaka za udhibiti, washauri wa kifedha na
wadau muhimu ili kukamilisha muundo wa dhamana hiyo.
Anasema kipaumbele kitatolewa kwa uwazi, ulinzi wa wawekezaji na kulingana na malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya Taifa, akiainisha kwamba uzinduzi wa dhamana hiyo ya miaka saba, unatarajiwa kufanyika mwakani baada ya kupitishwa na Bodi ya NHC.
![]() |
Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, katika mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, hivi karibuni. |
Anabainisha kwamba fedha
zitakazopatikana zitagharamia miradi kama vile ‘Nyumba za Samia’, miji ya pembeni
(satellite cities), na kukamilisha majengo ya kimkakati mijini.
“Mara tu Nyumba Bond
itakapoanza, itaongeza mtaji wa NHC na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika
maendeleo ya miundombinu. Huu ni mpango utakaoleta mageuzi makubwa katika namna
tunavyofadhili nakubadili makazi Tanzania," anasema Mkurugenzi Mkuu.
Rais Samia na miradi
ya NHC
Akizunguzia miradi
mikubwa kadhaa ya NHC iliyoanza tena baada ya kusimama kwa karibu miaka minane,
Hamad anarejea kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kufungua
njia ya maendeleo akisema;
"Miradi hiyo
ilisimama kwa sababu baadhi ya watendaji walishindwa kutekeleza majukumu yao.
Lakini Rais Samia alipoingia madarakani, alifanya uamuzi jasiri wa kufufua
miradi hii."
Miradi iliyochelewa na
sasa inaendelea ni pamoja na ujenzi wa majengo ya kibiashara na makazi chini ya
Morocco Square, Kawe 711 na Golden Premier Residence.
Mradi wa Morocco Square
sasa umekamilika kikamilifu na shughuli zinaendelea. Kawe 711 uko kwenye ujenzi
na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili mwakani.
Hata hivyo, Golden Premier Residence bado uko hatua za awali baada ya kusimama kwa miaka minane.
Kama Kawe 711, Golden
Premier Residence pia upo Kawe, ambapo pia kuna mradi mwingine—Nyumba za Samia.
Hamad anasema kuchelewa
kwa miradi hiyo kumesababisha kuongezeka kwa gharama kwa wateja wa NHC.
Hata hivyo, anakiri
kuwa kuchelewa kulisababisha gharama kupanda, lakini shirika halikupata hasara.
“Kama biashara nyingine
yoyote, tulipopata fursa ya kukamilisha miradi, tulirekebisha bajeti. Gharama
za ziada zilihamishiwa kwa wateja waliokuwa wamenunua au kupangisha nyumba
hizo,” anasema Abdallah.
Akitoa mfano wa Morocco
Square, alisema kuwa kama mradi huo ungekamilika miaka minane iliyopita,
gharama zingekuwa chini na wateja wangelipa kidogo.Sehemu ya Jengo la Morocco Sqare linavyoonekana.
“Kwa mfano, badala ya
mteja kulipa Shilingi milioni 300, sasa amelazimika kulipa Shilingi milioni
500,” alisema.
Hamad anahitimisha
kuwa mafanikio hayo ya NHC yanatarajiwa
kuchochea kukamilika kwa miradi mingine kama Kawe 711 na Golden Premier
Residence, hivyo kuendeleza ajenda ya Serikali ya makazi na maendeleo ya miji.
Maoni
Chapisha Maoni