Dk. Biteko afungua Karibu Kilifair 2025, aagiza matumizi ya TEHAMA kukuza utalii
- Ataka Sekta Binafsi iendelee kuwekeza Sekta ya Utalii hasa huduma za malazi, kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko
Exuperius
Kachenje, daimatznews@gmail.com
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii sanjari na matumizi ya nishati safi na endelevu.
![]() |
| Wananchi wakiingia Viwanja vya Magereza, Kisongo kushuhudia Maonyesho ya Nane ya Utalii ya Karibu Kilifair kwa mwaka 2025 yanayofanyika kwa siku tatu,Juni 6 hadi 8,2025. |
Dk. Biteko (Pichani chini),amesema hayo Juni 6, 2025 viwanja vya Magereza,Kisongo jijini Arusha wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu -Kilifair 2025, yanayofanyika kuanzia Juni 5 hadi 7, 2025, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Utalii Endelevu, Kujenga Ustahimilivu na Ubunifu”.
“Ninaiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii mambo matatu;… kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii sanjari namatumizi ya nishati safi na endelevu.”
Dk. Biteko amesema kwa
mwaka huu pekee, maonesho ya Karibu Kilifair yamekutanisha waoneshaji zaidi ya
500 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na zaidi ya nchi 10 duniani, wanunuzi wa
kimataifa 1,000 kutoka mataifa zaidi ya 40 pamoja na maelfu ya wadau na
wataalamu wa sekta ya utalii.
“Hii ni dhahiri kuwa,
dunia inaiangalia Tanzania na Afrika Mashariki kuwa kitovu cha utalii. Tutumie
fursa hii kutangaza vitu tulivyonavyo,” amesema Dk. Biteko.
Ameshauri pia badala ya
kutangaza kwa kutumia majarida pekee, ishirikiane na mamlaka mbalimbali za
Serikali na Sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara za utalii
nchini ili kuchochea na kuvutia uwekezaji zaidi.
Katika maagizo yake, Dk. Biteko pia ameiagiza wizara
kuendelea kubuni njia mbalimbali za uendelezaji wa mazao ya utalii nchini kwa
kuzingatia mgawanyiko wa aina ya mazao na mtawanyiko wa kijiografia wa nchi.
Kwa upande wa sekta
binafsi, Dk, Boteko ametoa rai iendelee
kuwekeza katika sekta ya utalii hasa katika eneo la huduma za malazi, ili
kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko kwa kuzingatia uwepo wa matukio mbalimbali
ya kimataifa yanayoendelea kufanyika nchini.
Amesema Serikali
itaendelea kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali ili kuhakikisha ustawi wa
biashara za utalii nchini na maendeleo ya sekta kwa ujumla wake unanufaisha taifa,
huku akiwataka Watanzania kuendelea kuwa wakarimu na kuelezea taswira nzuri ya
nchi ili kuvutia wageni zaidi.
Kwa mujibu wa Dk.
Biteko, maonesho ya utalii ya Karibu– Kilifair yanaendelea kukuwa kimataifa na
kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la
kujadili fursa za biashara, kubadilishana uzoefu katika biashara za utalii na
masoko pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hiyo muhimu ya uchumi.
Amebainisha kuwa
Serikali inatekeleza programu mbalimbali za kimkakati za utangazaji utalii,
zikiwemo filamu za Tanzania - the Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo
zimeleta mafanikio makubwa kwa nchi.
Dk. Biteko amesema
Tanzania imeendelea kutambulika na kushinda tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo
maarufu duniani za World Travel Awards – WTA zinazotolewa na Taasisi ya World
Luxury Media Group Limited ya nchini Uingereza ambazo pia ni chachu katika
kuvutia watalii katika soko la kimataifa.
“Tuzo hii ni matokeo ya Tanzania ya kutangaza ubora wa vivutio vilivyopo nchini kama vile Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro kuwa mahali bora pa kutembelea barani Afrika kwa shughuli za utalii wa safari na maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar. Pia, Tanzania imepewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za World Travel Awards kwa Kanda ya Afrika zitakazotolewa mwezi huu Juni, 2025,” amesema Dk. Biteko.
Awali, akimkaribisha
Naibu Waziri Mkuu kufungua maonyesho hayo ya nane ya maarufu Karibu Kili Fair
2025, Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Dustan Kitandula
amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wenye maono na kukuza
sekta ya utalii nchini.
Kitandula amesema sekta
ya utalii inakuwa kwa kasi duniani katika nchi mbalimbali mfano Tanzania ambapo
kwa mwaka 2024 imeingiza mapato ya utalii dola za Marekani bilioni 3.9 pamoja
na kupata watalii 5,360,247 huku watalii wa ndani wakiwa 3,218,352 na watalii
wa nje wakiwa 2,218,352.
Amesema katika
kuendelea kuimarisha sekta hiyo nchini, Serikali imeridhia kujenga ukumbi
mkubwa wa kimataifa jijini Arusha kwa gharama ya shilingi bilioni 230.
Naibu Waziri Kitandula ameongeza kuwa Wizara yake imeendelea
kushirikiana na wadau ili kukuza biashara ya utalii nchini kwa kuwa na vikao na
wadau hao ambapo imefanya maboresho ya sheria ya ada na tozo kwa lengo la
kukuza sekta hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mhe. Paul Makonda amewapongeza waandaji wa maonesho hayo ya Karibu -
Kilifair na kusema kuwa ni kichocheo kikubwa cha uchumi mkoani humo, aidha
amewaomba waandaji kuongeza idadi ya siku za maonesho kufikia siku tano hadi
saba.
Akizungumza kwenye
maonyesho hayo, Balozi wa Shirikisho la
Ujerumani nchini, Thomas Terstegen amesema sekta ya utalii imesaidia kutoa
ajira na kuongeza mapato nchini Tanzania na kwamba nchi yake itaendelea kuunga
mkono jitihada mbalimbali za utalii katika nchi za Afrika Mashariki akieleza
kuwa kwa kushirikiana na EAC wamezindua
kampeni inayoitwa Visit East Africa Feel the Vibe, inayolenga kusaidia watalii
kutembelea nchi za Afrika Mashariki.
Naibu Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Andrea Murietha amesema kuwa Jumuiya hiyo
imeendelea kufanya jitihada za kutangaza utalii kwa kufanya kazi karibu na nchi
wanachama ili kuhakikisha manufaa ya utalii yanapatikama kwa usawa katika nchi
hizo.
Makamu Mwenyekiti wa
Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Henry Kimambo ameishukuru Serikali
kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.
“ Tunapokuwa na jambo kuhusu utalii
tunasikilizwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi Taifa tunaishukuru sana
Serikali kwa hili. Niiombe Serikali na wadau utalii kwa pamoja tuongeze nguvu
katika maonesho haya ili siku moja tushindane na yale ya Afrika Kusini,
tunaweza kufanya haya maonesho ya Karibu- Kilifair kuwa makubwa zaidi Afrika,”
amesema Kimambo.
Awali, Dk. Biteko
ametembelea mabanda mbalimbali ikiwemo Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii
ambalo limetangaza fursa mbalimbali za uhifadhi na utalii kwa ajili ya kuvutia
watalii na wawekezaji wa ndani na nje.
Ametembelea pia Banda
la Nishati (Energy Solutions) ambapo amejionea vifaa mbalimbali vinavyotumia
nishati ya jua pamoja na banda la Hal linanalotengeneza magari ya kusafirisha
watalii nayotumia umeme.



Maoni
Chapisha Maoni