Nafasi 2,000 za ajira Serikalini hizi hapa
-CAG azitambua taasisi yenye uhitaji
-Ni taasisi 39 zimo balozi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Wakati wimbi la vijana kukosa ajira likishuhudiwa na kupigiwa kelele na makundi mbalimbali ya kijamii nchini, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imebainisha kuwepo kwa nafasi za kazi zilizo wazi zaidi ya 2,000 katika taasisi mbalimbali za Serikali na umma.
Ripoti hiyo Kuu ya
Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa mwaka 2023/24, iliyowasilishwa bungeni na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG), Charles Kichere hivi karibuni pichani juu, imezitaja
taasisi 39 zenye upungufu wa watumishi wa taaluma mbalimbali, baadhi zikiwa
ofisi za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi, Jeshi la Polisi, Hospitali za Rufaa
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Watumishi
wanaohitajika kwenye taasisi hizo jumla ni 4490, waliopo ni 2288 na upungufu ni
watumishi 2202,” imebainisha ripoti hiyo ya CAG.
Kwa mijibu wa CAG
taasisi kumi zinaongoza kwa kuwa na upungufu mkubwa wa watumishi Jeshi la
Polisi Tanzania Kitengo cha Matibabu likiongoza kwa kuwa na upungufu wa watumishi
500, huku waliopo sasa wakiwa 271 kati ya 771 wanaohitajika.
Ripoti hiyo
imeiorodhesha Hospitali ya Rufaa Bukoba kuwa ya pili kwa kuwa na upungufu wa
watumishi 296, huku Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Dar es Salaam ikiwa ya
tatu kwa upungufu wa watumishi wanaofikia 285.
Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Morogoro imeorodheshwa nafasi ya nne kwa kuwa na upungufu wa watumishi
234 na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikitajwa ya tano na CAG kwa kuwa
na upungufu wa watumishi 234.
“Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini ina mahitaji ya watumishi 342, waliopo ni 207, upungufu ni
watumishi 135. Tume ya Mipango ina upungufu wa watumishi 63, wanaohitajika ni
160 na waliopo sasa ni 97,” imebainisha ripoti ya CAG.
Kwa mujibu wa ripoti
hiyo ya CAG, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika imeoroheshwa kuwa ya
nane, ikiwa na upungufu wa watumishi 52, wakati Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Kusini ikitajwa ya tisa kutokana na upungufu wa watumishi 50, namba kumi ikiwa
ni Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iliyo na upungufu
wa watumishi 39 na upungufu
Tume ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano imetajwa ya kumi na moja kuwa ikiwa na upungufu wa
watumishi 34, ikiwa na watumishi wawili tu, kati ya watumishi 36 wanahohitajika,
huku Tume ya Pamoja ya Fedha ikiwa na upungufu wa watumishi 33 na Taasisiya
Ardhi Tabora imekutwa na upungufu wa watumishi 31 ikiorodheshwa ya 13 katika
jedwali la ripoti hiyo ya CAG.
Katika ripoti yake, CAG
ameiorodhesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa nambari14, ikiwa na upungufu
wa watumishi 24, ikifuatiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira
Tunduma iliyokutwa na upungufu wa watumishi 22.
CAG amekitaja Chuo
cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC) katika nafasi ya 16,
kikiwa na upungufu wa watumishi 18, kikifuatiwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
-Mawenzi ambayo pia ina upungufu wa watumishi 18,
Mahakama ya Rufaa za
Kodi imetajwa ya 18 kwa kuwa na nafasi za watumishi zilizo wazi kuwa ni 17,
Bodi ya Rufaa za Kodi ikifuatia kwa kubainika kuwa na upungufu wa watumishi 16.
Kwa mujibu wa ripoti
hiyo ya CAG kupitia kiambatanisho namba XV ambachoni jedwali, Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala ni ya 20, Taasisi ya Mafunzo ya Ufugaji Nyuki ina
upungufu wa watumishi 12 na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kibaya
ina nafasi zilizo wazi za watumishi10, kati ya 15 wanaohitajika, ambapo sasa
imeajiri watumishi watano pekee, ikitajwa kuwa namba 22.
Taasisi nyingine
zenye nafasi za watumishi zilizo wazi na idadi yake kwenye mabano ni kama
ifuatavyo; Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songe (9), Ofisi ya Rais
Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (8) na Mamlaka ya Maji Safi na
Usafi wa Mazingira Biharamulo (7).
Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Singida (7), Ubalozi wa Tanzania London, Uingereza (6), Wakala wa
Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), nafasi 5.
Ubalozi wa Tanzania
Paris, Ufaransa (4), Bodi ya Bonde la Ziwa Nyasa (3) Mfuko wa Usambazaji Maji
wa Losaa Kia (3), Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (3) na Mamlaka ya Maji Safi na
Usafi wa Mazingira Mpwapwa (2).
Ubalozi wa Tanzania
Roma, Italia nafasi 2, Ubalozi wa Tanzania Maputo Msumbiji (2), Ubalozi wa
Tanzania Riyadh, Saudi Arabia nafasi moja.
Nyingine ni Ofisi ya
Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (Fungu Na.4) nafasi moja, Bodi ya
Maji ya Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini (1) na taasisi ya 39 yenye nafasi
iliyo wazi ya utumishi ni Ubalozi wa Tanzania Muscat, Oman uliona na nafasi
moja.
Kwa mujibu wa CAG
taasisi hizo 39 za Serikali zina uhitaji wa watumishi 4,490, huku waliopo
wakiwa 2,288 na upungufu wa watumishi unaotakiwa kujaziwa kwa kuajiri watumishi
wapya ni 2,202.
Maoni
Chapisha Maoni