Exuperius Kachenje
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kutoridhishwa kwake na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kushindwa kufika kwenye matukio ya wadau wa habari ikiwemo kufungua Mkutano Mkuu wa Nane wa jukwaa hilo unaofanyika Dar es Salaam.
![]() |
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile (Aliyesimama) akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Nane wa Jukwaa hilo unaofanyika Novemba 6 hadi 9, 2024 jijini Dar es Salaam. |
Katika
mkutano huo wa Novemba 6 hadi 9, 2024, Waziri Silaa amewakilishwa na Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholaus Mkapa.
Kauli
hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alipokuwa akizungumza
kwenye ufunguzi wa mkutano huo leo Novemba 7, 2024 katika ukumbi wa NSSF Mafao
House, Ilala Dar es Salaam,uliobeba kauli mbiu; "Weledi kwa Uhimilivu wa
Vyombo vya Habari."
"Sisi
Wahariri hatufurahishwi na hatuwezi kuficha jambo hili, hatufurahishwi na
Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa,"
amesema Balile na kufafanua:
"Alialikwa kwenye Mkutano wa PST Arusha
hakwenda, aliakiwa kwenye Tuzo za Waandishi wa Habari hakwenda, alialikwa Mbeya
kwenye tukio la Wadau wa Habari hakwenda na sasa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la
Wahariri hakuja. Hali hii inaonesha kuwa
Waziri wetu hayupo tayari kushirikiana na Wadau wa Tasnia ya Habari."
Balile
amesema kwenye matukio ya aina hiyo ndiyo jukwaa sahihi kwa wadau kukutana na
Waziri na kuzungumza kwa pamoja masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa Tasnia
ya Habari, lakini inasikitisha kuwa Waziri hayupo tayari kwa ushirikiano.
Huku
akikumbuka tukio la aliyekuwa Waziri wa Habari enzi hizo Ramadhan Mapuri habari
zake kususiwa kuandikwa na vyombo vya habari, Balile ameongeza kuwa wakati wa
Waziri Nape Nnauye kwenye Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, wakati wowote alikuwa mstari wa mbele kwa muda wowote kuhudhuria
matukio mahimu ya wadau wa Tasnia ya Habari na ushirikiano huo ulikuwa na tija
kubwa kwenye tasnia.
"...Mfikishie
salam, Waziri wa Habari kondoo wake ni vyombo vya habari, sisi tupo tayari
kushirikiana na Serikali," amesema Balile akiomuomba Mkapa.
Hata
hivyo, Mwenyekiti huyo waTEF amemwomba waziri huyo kuwaambia mawaziri wengine
wawe na utaratibu wa kukutana na wahariri wa vyombo vya habari ili kuzungumza masuala mbalimabali
ya kitaifa kwa maslahi ya Tanzania.
"Rais
ameshakutana na wahariri mara mbili, Waziri Mkuu amefanya hivyo mara tatu,Naibu
Waziri Mkuu ameshafanya hivyo, pia Rais wa Zanzibar (Dk. Hussein Mwinyi), ameshakutana na wahariri,"
amesema Balile.
Akifungua
mkutano huo kwa niaba ya Waziri
Silaa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholas Mkapa, amesema Waziri wake
ametingwa na majukumu mengine ya Wizara na hivyo amemtuma yeye kumwakilisha.
Amesema wizara inaendelea kufanyia kazi madai mbalimbali ya wanahabari ikiwamo kuboresha sera na sheria zinazogusa utendaji wa vyombo vya habari nchini.
![]() |
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakifuatilia Mkutano wao Mkuu wa Nane wa Mwaka ukumbi wa NSSF, Mafao House Dar es Salaam. |
Akizungumzia
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu na Uchaguzi Mkuu mwaka
ujao,Mkapa amesema matukio hayo yatakuwa ni kipimo muhimu cha weledi kwa vyombo
vya habari na wahariri.
"Hakikisheni
mnasimamia na kutimiza sheria na misingi ya utoaji habari," amesema.
Awali,
akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, ameishukuruTEF kwa kuiunga mkono Serikali katika masuala mbali mbali ya
maendeleo ya taifa.
ReplyForward |
0 Maoni