Kuzindua Mfuko Mikopo Nafuu
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Rais Dk, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kufungua Kongamano na Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE2024), ambapo pia atazindua Mfuko wa Mikopo Nafuu na kutoa fedha kwa watafiti.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk, Amos Nungu |
Akizungumza
katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jijini Dar
es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Muhunda Nungu amesema Rais atafungua
kongamano hilo Desemba 2, 2024 ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini humo.
“Tutaanza
na Shilingi Bilioni 2.3 za kuwakopesha watafiti waliokidhi vigezo kutokana na
maandikowaliyoleta COSTECH, Rais atazindua mfuko huo. Fedha hizo ni kwa kuanzia,
tutaendelea kupata fedha kwa wadau na Serikali,” amesema Dk Amos na kufafanua;
“Kauli
mbiu ya Kongamano kwa mwaka huu ni; Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
katika Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Uchumi.”
Dk.
Nungu amesema kongamano hilo litafanyika hadi Desemba4,2024 likijumuisha
wabunifu, watafiti, wajasiriamali na watunga sera.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za afya na mazingira, COSTECH ina mengi ya kujivunia kuwashika mkono vijana wenye maono katika ubunifu na utafiti kwa kuwasaidia kifedha, kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za usaidizi pia zile za kimataifa.
“Tunao
mwongozo wa kitaifa ubunifu, tunaufuata, tunawasaidia vijana wetu wabunifu na
watafiti. Fedha za utafiti tunazotumia zinatolewa na Serikali, pia wafadhili.
Tunaamini Mfuko wa Mikopo Nafuu ukishazinduliwa pesa zitaongezeka, lakini pia
utakuwa wa uwazi, waombaji watahojiwa,” amesema Dk Amos.
Akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza COSTECH na
kuishauri ijifikirie zaidi katika kuboresha eneo lao liwe lakisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Makamishna wa COSTECH, Profesa Makenya Maboko, amesema wamepokea wazo hilo na kwamba watajenga majengo ya kisasa Dar es Salaam na Dodoma.
Amewaomba wahariri wa vyombo vya Habari kusaidia kusukuma mbele ajenda ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
" Imarisheni ushirikiano naCOSTECH ili kuhakikisha taarifa za sayansi, teknolojia na ubunifu zinaifikia jamii kwa ufanisi,"amesema.
0 Maoni