Mwandishi Wetu, WHMTH, Shinyanga
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imetoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 4.27, kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano, kujenga minara 30 ya mawasiliano mkoani Shinyanga.
![]() |
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba akisoma taarifa kuhusu ujenzi wa minara ya mawasiliano unaotekelezwa kati ya mfuko huo na waau mbalimbali wa mawasiliano mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (Mb.), aliye katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga .
Mashiba amemweleza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (Mb.), aliye katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga kwamba, minara hiyo imejengwa katika Wilaya za Kahama Manispaa, Kishapu, Msalala, Shinyanga DC na Ushetu.
Kuhusu mradi wa mnara 758 inayojengwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, Mashiba amesema Mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa hiyo, inakojengwa minara 30, na ruzuku ya UCSAF iliyotumika ni Shilingi Bilioni 4.27.
Amesema hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024, minara 9 imekwishawashwa, na baadhi ya kata ambazo vijiji vyake vimenufaika ni Bokomela, Idahina, Lunguya, Mwalugulu, Mwanase, Busangwa, Shagihilu, Lyamidati na Solwa.
Mtendaji Mkuu huyo wa UCSAF amesema hadi sasa, minara iliyokwishawashwa katika mradi huo wa minara 758 ambayo itawanufaisha watu milioni 8.5 itakapokamilika ni 186.
Akitoa ripoti kwa Waziri Nape kuhusu mnara uliojengwa na Kampuni ya Halotel, mwakilishi wa kampuni hiyo, amesema tangu uwashwe Mei 27, 2024 tayari watu 200 wameanza kutumia simu, huku wengine wakiendelea kuuziwa simu janja na kampuni hiyo kwa mkopo.
Mwakilishi huyo wa Halotel amesema wamelenga kuendelea kukopesha na kuuza simu na laini ili kuwafikia wakazi zaidi ya 4,400 watu wazima wa vijiji vinavyohudumiwa na mnara huo wa 2G na 3G.
0 Maoni