Mwandishi Wetu, WHMTH, Kigoma
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (pichani chini), ametoa siku 75, akizitaka kampuni za simu za Vodacom na TTCL kukamilisha ujenzi wa minara nane ya mawasiliano ya simu mkoani Kigoma.
Nape amesema anataka kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo Oktoba mwaka huu 2024, ambapo kimahesabu kutoka Julai 15, 2024 alipotoa agizo ni takriban siku 75, sawa na miezi miwili na nusu.
Nape ametoa maagizo hayo leo Julai 15, 2024 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma wakiwamo wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, pamoja na watoa huduma za mawasiliano, baada ya kupokea taarifa ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiliano Tannzania (TCRA), kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano na mradi wa ujenzi wa minara katika mkoa huo.
"Vodacom mna minara minne ambayo bado hamjaanza kujenga, tukubaliane hadi kufikia Oktoba mwaka huu 2024 iwe imekamilika, nimeshaongea na Mtendaji Mkuu sitaki ifike Oktoba tuanze kukabana koo, fedha mmeshapokea, malizeni ujenzi wa mnara, TTCL nao nataka Oktoba, 2024 pia kazi iwe imeisha, wana Kigoma waanze kunufaika na Uchumi wa Kidigitali," amesema Waziri Nape na kuongeza:
"Kukamilika mapema kwa ujenzi wa minara hiyo, kutawawezesha wananchi zaidi ya 108,126 walio na changamoto ya mawasiliano kwa sasa kwenye kata nane za Mkoa wa Kigoma kupata huduma hiyo ya mtandao."
Amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inahakikisha Watanzania wote wanaunganishwa kwa mawasiliano yenye sifa tano alizozitaja kuwa ni pamoja na upatikanaji, ubora, usalama, yenye matokeo chanya na anayoweza kumudu mtu yeyote hata wa kipato cha chini.
"Zimekuja shilingi bilioni 1.38 katika mkoa wako (Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye) kwa ajili ya ujenzi wa minara na tutafanya uchambuzi wa matumizi ya feha hizo. Niwaagize UCSAF na TCRA, kwa kuwa huu ni mkoa wa pembezoni, ni vizuri tukaongeza fedha ili maeneo yale ambayo yako wazi, katika miradi inayokuja tuongeze nguvu ili kuhakikisha tunawaunganisha Watanzania wote na hakuna atakayeachwa nyuma," amesema Waziri Nape..
Amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, wakurugenzi na wakuu wa wilaya kuwa wepesi wa kusaidia upatikanaji wa ardhi na kuidhinisha vibali kwa ajili ya ujenzi wa minara kwa wakati, ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano.
"..Wakati mwingine inachukua miezi sita kupata vibali, 'this is too much', ukiangalia hapa kuna minara haijajengwa na nilikuwa nazungumza na watoa huduma wanasema, hizi taratibu za utoaji vibali na ardhi za kijiji zinaleta shida, hii siyo sawa," amesema.
Waziri Nap pbia amemuomba mkuu huyo wa mkoa kuzungumza na TARURA na REA ili zitoe kipaumbele cha huduma za miundombinu ya barabara na umeme kwenye maeneo yote inakojengwa minara ili kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wake, hivyo wananchi wapate mawasiliano saa 24.
0 Maoni