-Aliamua ya Chongolo, ameamua ya Kinana
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Sijui unakumbuka.. au najua? Kama hukumbuki au hujui, nitakuwekea sawa kumbukumbu kuhusu maamuzi makubwa, mazito mawili ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM), Rais Dk, Samia Suluhu Hassan ndani ya chama hicho tawala.
![]() |
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan |
Ni hivi, kumbukumbu zinaonyesha kuwa tarehe 29 ndiyo CCM ilitangaza maamuzi magumu ya Mwenyekiti wake huyo wa Taifa, yaliyobeba mustakabali wa chama hicho tawala ndani ya miezi minane, Novemba 29,2023 hadi Julai 29,2024.
Tarehe hiyo, ndipo alitangaza
kuridhia kujiuzulu kwa Daniel Chongolo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, mwaka
uliopita 2023 na mwaka huu 2024, ameridhia kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti wa
CCM, Kanali Mstaafu, Abdulrahman Kinana.
Taarifa ya CCM ya jana Julai
29, 2024 imeeleza kwamba Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan, ameridhia ombi la Makamu Mwenyekiti wake, Kinana kujiuzulu
wadhifa huo.
Ingawa hapakuwa na taarifa au tangazo kabla la kujiuzulu kiongozi huyo maarufu wa CCM, lakini taarifa hiyo ya CCM imemnukuu Dk. Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kuridhia kwake ombi la makamu wake kujiuzulu.
Ni tarehe 29 JulaI, 2024
ndipo kuliwekwa hadharani kujiuzulu kwa Kinana na taarifa ya CCM Julai 29, 2024
kupitia Katibu wake wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala.
Hata hivyo, hatua ya Dk Samia
kutangaza kuridhia kujiuzulu kwa Kinana imetangazwa katika tarehe sawa na ambayo
alitangaza kuridhia kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo
takriban siku 240 sawa na miezi minane iliyopita.
Ikumbukwe kuwa Novemba
29,2023 CCM kupitia aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul
Makonda ilitangaza kwamba Rais Samia ameridhia Katibu Mkuu wa CCM, Daniel
Chongolo kujiuzulu, ambapo sasa mrithi wake ni Balozi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kabla ya Mwenyekiti wa CCM
Taifa kutangaza kuridhia Chongolo, ilisambaa barua kwenye mitandao ya kujamii
iliyodaiwa kuandikwa na kusainiwa na Chongolo Novemba 7, 2023 kwenda kwa Rais
Dk. Samia Suluhu Hassan kuomba kujiuzulu wadhifa wake wa Ukatibu Mkuu wa CCM.
Novemba 29, mwaka 2023,
alijitokea Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM kwa wakati huo, Paul Makonda akawaambia
waandishi wa Habari: “Mwenyekiti wa CCM ameijulisha Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa kupokea barua ya kujiuzulu ya Ndugu Daniel Chongolo na kuridhia ombi
hilo.”
Chongolo ambaye sasa ni Mkuu
wa Mkoa wa Songwe, alihudumu wadhifa huo kati ya Aprili 30,2021 hadi Novemba
29,2023, ambayo ni miezi 31 sawa na takriban siku 926. Hatua hiyo ilidaiwa kutokana
na madai ya kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii, hivyo yeye kuamua
kuwajibika.
Lakini, kujiuzulu kwa Kinana
kumetajwa na Rais Dk. Samia ni kutokana na ombi la kiongozi huyo aliyehudumu
ndani ya CCM na Serikali katika nafasi tofauti za uongozi.
“Ni kweli nilipokuomba
utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama
ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia kalini kwa kuwa umeomba
sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako,”
inaeleza sehemu ya taarifa ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM,
ikimnukuu Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa amesisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kutumia
uzoefu na maarifa ya Kinana vitakapohitajika.
Kinana aliteuliwa na CCM kuwa
Makamu wa Mwenyekiti wake, Machi, 2022 ambapo amehudumu nafasi hiyo kwa miezi
28, sawa na takriban siku 840, akitanguliwa na Phillip Mangula.
0 Maoni