Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Wanafunzi watatu kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii ni miongoni mwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali duniani wanaokutana jijini Nairobi nchini Kenya na kuchuana kuwania Tuzo ya 'Hult' kupitia mawazo yao ya kibiashara na ubunifu.
Wanafunzi hao kutoka Tanzania ni pamoja na Hellena Sailas, Maria Daudi, na Method Dallu ambao wamechaguliwa kuwania tuzo hiyo kupitia wazo lao la kibishara na ubunifu linalohusu utengenezaji na uzalishaji wa matofali kwa kutumia taka za plastiki.
Tuzo ya Hult Prize ni shindano kubwa zaidi la ujasiriamali wa kijamii kwa wanafunzi duniani, linaloendeshwa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa(UN), na timu za wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani.
Akizungumza na wanafunzi hao ambao wamewasili jijini Nairobi jana, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk. Joyce Nyoni amewapongeza kwa ubunifu huo na kuwatakia kila la kheri katika ushiriki wao.
Mashindano hayo yanalenga kutatua matatizo ya kijamii kwa kuanzisha biashara ya kijamii inayoweza kukua na kudumu.
Washindi katika shindano hilo watawasilisha miradi yao mbele ya jopo la majaji mashuhuri, viongozi wa biashara duniani, viongozi wa mawazo na watetezi wa mabadiliko ili kushinda dola milioni moja za Marekani na kuanzisha biashara zao.
0 Maoni