Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Serikali ya Tanzania imeuhakikishia Umoja wa Posta Afrika (PAPU), msimamo wake usioyumba kwamba, itaendelea kuunga mkono na kusaidia mikakati ya umoja huo kwa maendeleo ya Sekta ya Posta Afrika.
Msimamo huo wa Serikali umetolewa
leo Juni 11, 2024 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), wakati akihutubia Mkutano wa 42 wa
Baraza la Utawala la PAPU, unaofanyika makao makuu ya umoja huo jijini Arusha.
"Kwa heshima kubwa,
napenda kuthibitisha msimamo usioyumba wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika kusaidia mipango mbalimbali ya PAPU," amesema Mhandisi
Mahundi aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo.
Mhandisi Mahundi ameutaka mkutano huo wa PAPU, kutafakari njia zitakazowezesha mageuzi ya posta Afrika, ili kuendana na maendeleo ya kasi ya biashara mtandao (e-commerce), pamoja na mabadiliko makubwa ya teknolojia ya mawasiliano na dijitali.
Naibu Waziri huyo amesisitiza
kwamba barani Afrika, posta inafanya kazi kubwa ya kutoa huduma za kuaminika,
uhakika na zenye tija kwa biashara kubwa, ndogo na za kati (MSMEs).
“Ni vizuri kwamba wakati
dirisha la biashara mtandao likiwa limefunguka na kuja na fursa zaidi, tayari
baadhi ya Posta Afrika zimeanza kujishughulisha na kutoa huduma mbalimbali
katika mnyororo wa biashara mtandao,” amesema Maryprisca Mahundi.
Amesema, bado kila mtu anakumbuka matukio ya Septemba 3 mwaka uliopita, liliposhuhudiwa tukio la kihistoria la uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Ofisi za PAPU jijini Arusha, uliofanywa na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amebainisha kuwa tukio hilo la kihistoria la nembo hiyo ni kielelezo na uthibitisho wa uhakika wa uongozi wa dhati na wenye maono wa viongozi wa Tanzania kuhusu mikakati na malengo ya PAPU.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri
huyo, uzinduzi wa PAPU Tower ni alama ya juhudi za pamoja za nchi wanachama wa
umoja huo katika kuendeleza ugunduzi, kuimarisha mawasiliano na kukuza
maendeleo katika eneo lote la Afrika.
Mkutano huo wa Baraza la Utawala la PAPU, unatarajiwa kujadili maazimio na taarifa za vikao vya Kamati za Wataalam wa masuala ya posta vilivyoanza Juni 03 hadi 7, 2024, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Fedha na Utawala, Sera na Kanuni, Uendeshaji na Teknolojia pamoja na Mikakati.
Awali, akimkaribisha mgeni
rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nicholaus Merinyo Mkapa, amesema udhibiti
madhubuti wa maafa na hatari ni muhimu katika ulimwengu wa leo, hivyo Sekta ya Posta
lazima iwe thabiti na tayari kukabiliana na majanga ya asili, vitisho vya
mtandao na hatari zingine.
Mkapa amesema hatua hiyo inahusisha kuandaa mipango ya kina ya
udhibiti wa maafa na hatari, kuwekeza katika miundombinu salama na kutoa
mafunzo kwa wafanyakazi ili kushughulikia dharura kwa ufanisi.
Amesema mfumo thabiti wa Sera
ya Posta ni muhimu kwa ajili ya kuongoza sera za mahitaji ya sekta zinazokuza
uvumbuzi, ushindani na maendeleo.
0 Maoni