Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Kikokotoo sasa asilimia 40, Rais awapoza wastaafu

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Serikali imesikia kilio cha wastaafu kuhusu kikotoo, ikitangaza kwamba malipo ya mkupuo sasa yatakuwa ni asilimia 40 kutoka 33 ya awali kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa bungeni mjini Dodoma leo Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba(pichani juu), alipokuwa akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

“Serikali imesikia kilio cha watumishi na kufanyia kazi suala la masilahi..., Rais Samia ameelekeza kuongezeka kwa malipo ya mkupuo....; 

"Wastaafu waliokuwa wakipokea asilimia 25 hadi 33 kwa malipo ya mkupuo, sasa watapandishwa hadi asilimia 35 na walioathirika na mabadiliko yaliyojitokeza watakuwa sehemu ya mabadiliko hayo," amesema Mwigulu na kuongeza:

“Serikali itaendelea kuliangalia kwa karibu suala la masilahi ya wastaafu kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mifuko yetu.” 

Hatua hiyo ya Serikali inagusa watumishi walioshushiwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 50 hadi 33 mwaka 2017 na kuzua manung'uniko kutoka kwa wafanyakazi, wakitaka mfumo wa zamani urejeshwe, ambapo kwa muda mrefu waliodai malipo hayo hayaendani na hali halisi ya maisha.

Hata hivyo, swali linalobaki kwa wastaafu ni namna watakavyopokea mabadiliko hayo ya kikokotoo, ambacho sasa malipo ya mkupuo yameongezeka kwa asilimia saba.Kabla ya kutangaza ongezeko hilo la malipo ya mkupuo kwa wastaafu, Waziri wa Fedha alieleza:

"Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali imelipa Sh. bilioni 160.04 kwa ajili ya kugharamia upandishwaji wa vyeo kwa watumishi wa umma  126,814 wa kada mbalimbali. Hata hivyo, kumekuwa na kilio kikubwa kutoka kwa wastaafu kuhusu kikokotoo; 

Kama asemavyo Naibu Waziri wa Fedha Mheshimiwa Chande kuwa mara zote mtoto akilia, mama hujua kwa sauti kuwa hapo mtoto analilia nini. Akilia anasema hapo ameshiba, akilia anasema hapo ana usingizi, akilia anasema hapo nguo zimembana au akilia anasema apelekwe hospitali; 

Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan, imesikia kilio hicho na imekifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wastaafu wetu na wanaotarajiwa kustaafu; ...Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kuongezwa  malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliopo  sasa hadi asilimia 40."

Kwa mujibu wa Dk. Mwigulu hilo ndilo kundi kubwa la watumishi, wanaofanya kazi nzuri zaidi kwa taifa akiwataja walimu, kada ya afya, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na makundi mengine yalioko Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. 

"Rais ameelekeza kuongezewa zaidi kundi lililokuwa likipokea asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33, sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka wa fedha huu. Watumishi walioathirika na mabadiliko haya watazingatiwa katika mabadiliko haya. 

Chapisha Maoni

0 Maoni