-NHC yalipa mabilioni: Ni kupitia mnada wa wazi,
-Thamani ya NHC kuongezeka: Sasa kuboresha mandhari
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limenunua rasmi eneo la Urafiki na majengo yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China (Tanzania - China Friendship Textile CO LTD).
![]() |
Sehemu ya majengo ya kilichokuwa la Kiwanda cha Urafiki, ambayo sasa yanamilikiwa na NHC. |
Hatua hiyo, itaongeza ukubwa wa mtaji na thamani ya shirika hilo la nyumba, linalotajwa kuongoza kwa ukubwa wa mtaji na uwekezaji barani Afrika, huku NHC likitajwa pia kuidhinisha na kusaini mikataba ya miradi 21 ya ubia yenye thamani ya Sh.bilioni 271 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kukagua maeneo mbalimbali, ambayo sasa yatakuwa chini ya miliki ya NHC na kufafanua kuwa eneo hilo linajumuisha nyumba, maghala, viwanja vya wazi, viwanda na mali nyinginezo.
Habari zaidi za ndani kutoka vyanzo vingine, zinaonyesha kwamba mashine na mitambo ya kilichokuwa Kiwanda cha Nguo Urafiki, vimeuzwa kwa watu tofauti na NHC kwa njia ya mnada, kutumia mtindo wa mafungu. (LOT).
Katika ziara yake, Saguya ameelezea furaha yake na matumaini makubwa kuhusu hatua hiyo, akibainisha kwamba itasaidia kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa maeneo hayo ikiwamo kuboresha mandhari ya Dar es Salaam.
Mbali na kununua majengo hayo, NHC inaendelea kufanya ukarabati katika majengo yake 181 yenye vyumba 3,111 yaliyo katika mikoa mbalimbali nchini, huku ujeni wa nyumba 560 awamu ya kwanza eneo la Kawe Dar es Salaam ukiwa umefikia asilimia 60 na ujenzi wa jengo la Morocco Square ukikamilika na upangishaji hoteli ukifanyika kwa asilimia 100, maduka asilimia 94 na ofisi asilima 39..
Amesema kuwa NHC, imelinunua eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kutoka kwa mnada wa wazi kikiwa na thamani ya mabilioni ya fedha.
Amesema:"Kupitia umiliki huu mpya, Shirika la Nyumba la Taifa limejipanga kuboresha maeneo haya ili kuendana na malengo yetu ya kutoa makazi bora na ya kisasa kwa wananchi. Tumeanza kwa kulipima eneo lote na kutambua mipaka yote inayohusisha eneo hilo."
Kwa mujibu wa Saguya, eneo la Urafiki lina historia ndefu ya kuwa kituo muhimu cha viwanda na makazi, kikitoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
"Hivi sasa, NHC inapanga kufanyia maboresho makubwa eneo hili kwa kujenga miundombinu bora, nyumba za kisasa na maeneo ya biashara ambayo yatavutia wawekezaji na wakazi wapya, "amesema Saguya.
Ameongeza: "Shirika la Nyumba la Taifa linaamini kuwa mradi huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwa ujumla na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya makazi na maendeleo ya kiuchumi nchini. Katika mpango wa maendeleo ya NHC, eneo la Urafiki litawekewa mkazo maalum kwa ajili ya kuhakikisha kuwa linakuwa mfano bora wa maendeleo ya kisasa na endelevu."
![]() |
Baadhi ya maghala ya kilichokuwa Kiwanda cha Nguo Urafiki ambayo sasa ni mali ya NHC.Picha zote kwa hisani ya NHC. |
Saguya alihitimisha kwa kusema, "Hii ni hatua muhimu kwa NHC na kwa taifa letu. Tunawaomba wananchi na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zetu katika kuboresha na kuendeleza maeneo haya kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Wakati hayo yakiendelea, shirika hilo linaelezwa kukusanya Sh. bilioni 208.1 ambazo ni sawa na asilimia 76.1 ya lengo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China (Tanzania - China Friendship Textile CO LTD). Kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa China na Tanzania na kina historia ndefu na uhusiano wa muda mrefu.
Awali, kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya kampuni iliyokuwa inamiliki kiwanda hicho na wafanyakazi, jambo lililokuwa limewafikisha katika hatua mbalimbali za usuluhishi hadi kiwanda hicho kilipopigwa mnada ili kuweza kuokoa mali za Kampuni.
Hayo yalibainishwa wakati Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC), Hamad Abdallah, alipofanya ziara kutembelea miradi inayotekelezwa na NHC mkoani Dar es Salaam, kukagua na kuona maendeleo.
Hamad amefanya ziara katika miradi ya Samia Housing, Morocco Square, Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na eneo la Urafiki Dar es Salaam hivi karibuni.
0 Maoni