Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Vyuo vikuu vyatakiwa kulinda bunifu

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Vyuo vikuu nchini vimetakiwa kulinda bunifu zinazotokana na tafiti zinazofanywa na wahadhiri na wanafunzi  nchini kwa kuzisajili, ili ziweze kuleta manufaa kwa jamii na wabunifu kwa ujumla. 

Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Loy Mhando

Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Loy Mhando amesema hayo wakati wa kutoa elimu na mafunzo juu ya umuhimu wa kulinda na kuzisajili bunifu wanazofanya kupitia tafiti, ili ziweze kuwaletea faida katika katika Chuo cha Waislamu Morogoro (MUM) Aprili 16, 2024.

“Bunifu nyingi katika vyuo zinatokana na kazi za utafiti, zinafanyika kwa lengo la kutatua changamoto katika jamii, kazi ambazo hufanywa na wahadhiri na wanafunzi wanaojihusisha na shughuli za ubunifu zikiwemo uandishi, ambapo tafiti  zao huleta matokeo katika kutatua matatizo kwenye jamii,” amesema Loy.

Amebainisha kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaeleza umuhimu wa kufanya bunifu zinazolenga kutatua changamoto kwenye jamii, lakini pia kufahamu kwamba bunifu wanazotengeneza zinaweza zulindwa na BRELA kwa mujibu wa sheria kwani wakala hiyo inahusika na ulinzi wa bunifu kwa  kutoa hataza( Pattent ). 

Kwa mujibu wa Loy, BRELA pia inahusika na kulinda alama mbalimbali za huduma na  za biashara  akibainisha kwamba, bunifu zote zinazotolewa na chuo hicho zitalindwa pia kuwaletea manufaa zitakapokwenda kutumika maeneo mbalimbali.

Ameongeza kuwa, Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wabunifu, ndio maana imeweka mifumo stahiki, itakayomwezesha mbunifu kulindwa hivyo kumpa fursa ya kubuni zaidi na kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye jamii, akiwataka kutambua kuwa bunifu ni mali kama mali nyingine. 

Elimu hiyo inayotolewa na BRELA inalenga kuviwezesha vyuo kupata faida kutokana na tafiti, kwa kuwa vinawekeza nguvu nyingi ili kuwezesha kufanyika pia kuwawezesha wanafunzi wanapokuwa vyuoni kuwa na mawazo ya kujiajiri au kuona namna ya kujiendeleza katika tafiti na bunifu hizo kwani zitawapatia kipato.

Mafunzo hayo yameandaliwa na BRELA  kwa vyuo vikuu, vyuo vya ufundi pamoja na taasisi zinazohusika na uzalishaji katika nyanja mbalimbali, ambapo kwa Morogoro imetoa mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, na yataendelea kutolewa katika Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Chuo cha Ufundi VETA  na wabunifu mbalimbali akiwemo mbunifu wa vazi linalojulikana kama, 'Samia Suti' kwa kutumia Batiki wa Moro batiki.  

Mwisho.

Chapisha Maoni

0 Maoni